Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kupata fursa ya kuweza kuchangia hoja iliyowasilishwa na Wizara ya Afya, Jinsia, Maendeleo ya Jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja na kipekee naomba uniruhusu nimpongeze Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana Mheshimiwa Ummy Mwalimu na Naibu wake na Katibu Mkuu na Watumishi wote kwa ushirikiano ambao wamekuwa wakitoa kwetu sisi Wizara ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI na kimsingi Watanzania wote ni mashuhuda. Kazi kubwa ambayo inafanywa katika kuboresha afya za Watanzania haitiliwi mashaka hata Mtanzania mmoja. Kwa hiyo, naamini kwa moto huu ambao umeanza hakika Watanzania watarajie mambo makubwa mazuri chini ya uongozi wa viongozi wetu hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wako Wabunge wengi ambao wamechangia na karibu wote walikuwa wakipongeza. Kama kuna mtu ambaye hakupongeza basi labda amepongeza kimoyo moyo lakini hata upande wa pili nao ni mashuhuda kwamba kazi nzuri inafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna hoja ambazo zimeibuliwa na ambazo sisi kama TAMISEMI ni vizuri tukajibu kiasi. Katika hoja mojawapo ni pamoja na upungufu wa watumishi wa afya katika hospitali za Wilaya, vituo vya afya na zahanati. Tunakiri kabisa kwamba kuna upungufu, mpaka sasa hivi tunao watumishi wapatao 56,881 sawa sawa na asilimia 48, kwa hiyo tuna upungufu wa asilimia 52, lakini maelezo yapo ambayo yanajisheheni kwamba kwanini tunao upungufu kiasi hicho.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi sote Watanzania ni mashuhuda kwamba kama kuna sehemu ambayo uwekezaji umefanyika ni katika Sekta ya afya, vituo vya afya vimeongezeka, zahanati zimeongezeka, kwa vyovyote vile lazima ionekane kwamba kuna gap, lakini pia kuna sababu nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa mfano, katika wataalam ambao wanazalishwa tumekuwa na wataalam wachache sana hasa madaktari kuhusiana na masuala mazima ya meno, lakini hata kuhusiana na suala zima la mionzi lakini ziko jitihada ambazo zimechukuliwa na Serikali za makusudi kuhakikisha kwamba upungufu huu ambao unaonekana kwa sababu azma ya Serikali inayoongozwa na Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, afya ya Mtanzania ndiyo kipaumbele. Kuna jitihada za makusudi ambazo zinafanywa ili kuhakikisha kwamba kila Mtanzania anapata huduma ya afya tena kwa umbali usiokuwa mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumeomba na naamini kibali kitapatikana, tumeomba kuweza kuajiri watumishi 15,000. Lakini pia naomba nichukue fursa hii kupongeza Mfuko wa Benjamini Mkapa na wametusaidia wameajiri watumishi kama 300 kwa muda wa miaka miwili na sasa hivi wanafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi ambalo naomba nitoe maelekezo katika Mikoa yote, tuhakikishe maeneo yale na hasa ya pembezoni na vijijini ambako ndiyo kuna upungufu mkubwa, tuhakikishe kwamba wataalam hawa wanapelekwa kwa sababu kumekuwa na namna unakuta mijini wako watumishi wa afya wengi lakini ukienda vijijini unakuta wako wachache. Kwa hiyo, pale ambapo inatajwa upungufu, ukienda maeneo ya mjini hukuti upungufu kama ambavyo iko mijini. Nitoe maelekezo mahsusi tuhakikishe kwamba inafanyika redistribution ili maeneo yenye upungufu mkubwa yaweze kupelekwa hao wataalam.

Mheshimiwa Naibu Spika, wewe mwenyewe ni shuhuda, tukiwa hapa wakati Mheshimiwa Waziri wa Utumishi aliwasihi Wabunge kama kuna kituo chochote au zahanati yoyote ambayo inalazimika kufungwa kwa sababu eti hakuna mtumishi, aliwaomba Waheshimiwa Wabunge waandike barua ili tuweze kujaza pengo hilo na amini Waheshimiwa Wabunge walitenda haki katika hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja pia zimeibuliwa kuhusiana na Community Health Workers, hoja ya msingi tunaiunga mkono lakini ni vizuri tuka-balance hizi equation. Si rahisi pamoja na nia njema ya kuhakikisha kwamba tunawaajiri hawa, lakini itakuwa si busara pale ambapo tuna kituo cha afya au tuna zahanati ambayo tunashindwa kuifungua kwa sababu hakuna mhudumu wa afya tukaenda kuwaajiri hawa. Kwa hiyo, pamoja na nia njema ni vizuri tukatumia structure iliyopo, tunao Maafisa Ustawi wa Jamii ni rahisi kuweza kuwa-train na wakaweza kuwasaidia watu wetu lakini azma kwa siku za usoni tutahakikisha kwamba nao watu wanaweza kuajiriwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wamelisema vizuri kuhusiana na suala zima la lishe. Hakuna namna pekee ambayo unaweza ukawekeza kuhakikisha kwamba unawapata Watanzania wenye brain nzuri kama hatuwekezi katika siku 1,000 za mwanzo. Wataalam wanatuambia kwamba tunaanza kuhesabu tangu pale ambapo mimba inatungwa mpaka mtoto anapokuja kuzaliwa na miezi ile miwili ndiyo muhimu sana katika kuweza kuhakikisha tunawekeza katika hicho.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumepokea, tunajua umuhimu wa jambo hili na ndiyo maana nina kila sababu ya kumshukuru Makamu wa Rais pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu, tumewekeana mikataba na Wakuu wa Mikoa wote Tanzania, Mikoa 26 kuhakikisha kwamba suala la udumavu linabaki historia na tumekuwa na utaratibu wa kupimana kila baada ya miezi sita na muelekeo ni mzuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge na sisi kwa nafasi zetu za uongozi ni mabalozi, tunapofanya mikutano yetu ni vizuri tukahakikisha kwamba elimu hii tunaifikisha kwa Watanzania wenzetu. Maana hakuna namna pekee ambayo unaweza uhakikisha kwamba watoto wetu wanakuja kushindana na mataifa mengine kama hatujawekeza katika umri wao wakiwa bado watoto wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niwasihi Waheshimiwa Wabunge limesemwa juu ya kujihakikishia afya kwa kila Mtanzania. Namna pekee na Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana atakuja aliseme kwa kirefu ni kuhakikisha kwamba Watanzania mwelekeo ni kujiunga na Bima ya Afya. Bima ya afya ndiyo mkombozi wa kuhakikisha kila Mtanzania anaenda kupata tiba pale ambapo anapatwa ugonjwa tena tiba ambayo ya kisasa kabisa. Haipendezi pale ambapo inatokea Mtanzania anaenda wakati anaumwa, anashindwa kupata matibabu eti kwa sababu hana fedha au hajajiunga na bima ya afya. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge sisi ni viongozi ni vizuri tukatoa hamasa kwa Watanzania, mataifa yote duniani utaratibu ndiyo huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Waheshimiwa Wabunge walichangia na alianza kusema Mheshimiwa Nachuma, akataja Mkoa wake wa Mtwara na hasa na maeneo yote ambayo ni mwambao mwa bahari. Kuna mazalia mengi sana ya mbu, akaomba ifanyike jitihada za makusudi. Sisi sote ni kwamba Tanzania tuna kiwanda chetu cha viuadudu ambacho kipo pale Mkoa wa Pwani na kipekee Mheshimiwa Rais naomba tumshukuru aliweza kuwekeza shilingi bilioni 1.3 na fedha hizo zikatumika katika kununua viuatilifu hivyo kwa ajili ya kusambaza halmashauri zote Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ni wajibu wetu Wakurugenzi wote Tanzania tuhakikishe kwamba hicho ambacho kilianzishwa na Mheshimiwa Rais kiwe endelevu kwa kuhakikisha kwamba tunatenga kwenye bajeti zetu fedha kwa ajili ya kuanza kununua viuatilifu kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunapambana na mazalia ya mbu. Lakini pia ni vizuri hamasa ikatolewa kuhakikisha kwamba mazalia ya mbu tunatokomeza. Wenzetu Zanzibar wameweza Tanzania Bara pia tunaweza, ni suala la kuamua na tukishirikishana sisi sote inawezekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, itoshe katika hayo ambayo sisi yamejitokeza tukaona tuyatolee ufafanuzi, naomba niendelee kuunga mkono hoja, ahsante sana kwa nafasi. (Makofi)