Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Mussa Bakari Mbarouk

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, labda kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametujaalia afya njema ya kukutana katika Bunge letu hili na kuzungumza masuala ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda baada ya kusema hapo kwanza nitoe shukrani kwa Wizara yetu ya Ujenzi kwa taarifa ambazo walinipa kwenye Bandari yetu ya Tanga, kwamba kuna fedha zilitengwa na zimekwishafika kwa ajili ya kuongeza kina cha maji ya Bandari yetu ili Meli ziweze kufunga a long side nishukuru sana kwa hili takribani shilingi bilioni 1.8 kama sikosei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo jingine nipende kuzungumzia Bandari yetu ya Tanga; Bandari yetu ya Tanga ni Bandari ya muda mrefu na ya kihistoria lakini bado inafanyakazi chini ya kiwango. Sasa niiombe na kuishauri Serikali, Bandari ile pamoja na kuongeza kina, pamoja na pia taarifa nyingine kwamba baada ya ile green ya forty foot container kupata mpya lakini bado inahitaji ifanyekazi kama ilivyokuwa zamani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanini nasema hivyo? Zamani Bandari ya Tanga ilikuwa ikisafirisha mizigo mingi sana ya Kahawa, ya Pamba, ya Katani, Alizeti na vitu vingine sasa, sasa hivi Bandari ile imekuwa inafanyakazi chini ya kiwango. Niseme hata alipokuja Mheshimiwa Rais katika kuweka jiwe la msingi la uzinduzi wa bomba la mafuta nilimuomba basi angalau bandari zetu hizi zifanye kazi kwa kiwango angalau japo kukaribiana, kwa sababu gani nasema hivyo? Kama unakwenda Zanzibar ama kwa ndege, ama kwa meli utakuta kuna msururu wa meli zimekaa zinasubiri zamu ya kuingia Bandarini kupakua mizigo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niseme tu, kanini basi tusifanye category hizi za mizigo kwa mfano, Bandari yetu ya Tanga ichukue mizigo yetu ya Tanga, ichukue mizigo ya Moshi, Arusha, Manyara lakini hata Musoma na Bukoba na Nchi kama Rwanda na Uganda angalau ingekuwa inafanyakazi hivyo ingekuwa imerudia kufanya kazi katika kiwango chake kama ilivyokuwa zamani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Bandari nyingine pia labda ya Mtwara tuseme ingechukua nayo mizigo labda ya Mtwara yenyewe, Mbeya, Sumbawanga, Katavi huko, Malawi na kwingineko ingekuwa Bandari inafanyakazi. Sasa tumekuwa kama wafanyabiashara ya mayai ambao mayai yote tumeyatia katika chombo kimoja ukijikwaa tu ni kwamba umeshapoteza mtaji. Nashauri Serikali ifanye categories za mizigo; mizigo iwe kwa Kanda fulani, Bandari fulani itumike, Kanda fulani, Bandari fulani itumike lakini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo pia, zipo Bandari Bubu hatuwezi kukataa na hatuwezi kuepuka Bandari Bubu kwa sababu wananchi wetu ama wawe wavuvi au wasafirishaji wa vyombo vidogo vidogo wanazitumia. Mfano, Bandari ya Kipumbwi, mfano Bandari ya Kigombe hizi nasema zingeboreshwa zikajengwa kama ilivyojengwa Bandari ya Pangani pakajengwa Gati, pakawa pale na majengo kwa ajili ya kuchukua ushuru wa forodha, wakawepo wafanyakazi wa TRA tukakusanya mapato. Lakini kuendelea tu kuzitamka tu Bandari Bubu, Bandari Bubu hatuwezi kuziepuka. Ni vyema tungeweka Maafisa wa forodha pale wakawa wanapokea bidhaa zinazotoka Zanzibar kwa sababu hizo ndiyo ambazo mara nyingi tumekuwa tukizilalamikia kwamba zinapitishwa katika Bandari Bubu na kuikosesha Serikali mapato. Kwa hiyo, hilo nilikuwa nashauri Bandari ya Kipumbwi, Bandari ya Kigombe zifanyekazi na pia zitaongeza ajira kwa vijana wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo jingine nipende kuizungumzia barabara ya Pangani; barabara ya hii ni barabara ya kihistoria. Iliwekewa ahadi na Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Nyerere, Rais wa Awamu ya Pili, Rais Mwinyi, Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, Rais wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na sasa imeingia madarakani Serikali ya Awamu ya Tano. Kwa maneno ambayo yamekuwa yakisemwa mara kwa mara kwamba hii Serikali ya Awamu ya Tano ni sikivu na tumeona kwenye Bajeti fedha nyingi zimepelekwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa namuomba Mheshimiwa Magufuli autafune ule mfupa uliomshinda Fisi, kwanini? Barabara ya Pangani kama itajengwa itakuwa ni kichocheo kwanza cha kiuchumi kwa sababu gani? Wanaotoka nchi jirani kama Kenya kupitia Mombasa na sisi watu wa Tanga tutaokoa muda wa kufika Dar es Salaam, kama tunavyoijua Dar es salaam ni Jiji la kibiashara na biashara nyingi zinafanywa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa leo kusikia kupitia Bunge hili, pamoja na kwamba Mheshimiwa Waziri tumekwishanong’ona kidogo kaniambia fedha zimekwishapatikana, Mkandarasi amekwishapatikana, hiyo feasibility study ilikwishafanyika. Basi Serikali itoe nneo, itoe tamko ili ionekane kwamba lini barabara ya Pangani inaanza kujengwa rasmi. Naamini tamko litakalotoka hapa leo, Mheshimiwa Waziri utaona watu wa Tanga watakavyoshangilia, watakavyokuombea dua na vilevile pia watakavyonipongeza Mbunge wao ambae niliyekuwa naizungumzia mara kwa mara. Kwa hiyo, hapa nategemea kupata tamko la Serikali kwamba rasmi lini barabara itajengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, hata wale ambao walizuiwa ama kuendeleza mashamba yao au kuendeleza nyumba zao ambao wako pembezoni mwa barabara wamekuwa wakihoji kuhusu fidia pia nilitaka leo Serikali itoe tamko lini watu wale wataanza kulipwa fidia zao kwa sababu wamekubali kutokuendeleza mashamba na majengo kwamba wanataka barabara ijengwe ili tuweze kusogeza maendeleo ya wananchi. Kwa mfano, barabara ya Pangani kama itajengwa kuna mazao ya nazi, kuna mazao ya muhogo maeneo ya Kirare lakini kuna mazao mengine pia kama ya Matikitimaji n.k yataweza kusafirishwa kwa urahisi kupelekwa katika soko la Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine, barabara…

MWENYEKITI: Ahsante muda wako umekwisha.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: …naomba nazo pia changarawe zifanyiwekazi kwa sababu sikuona humu katika kitabu. Naomba mtakapokuja Mawaziri basi mtuelezee barabara za changarawe nazo zinajengwa lini kama vile kutoka Mabokweni kwenda hadi Daluni, Maramba na Korogwe. Ahsante. (Makofi)