Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ludewa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuongea na kuchangia hotuba. Kwanza naipongeza Serikali kwa kazi nzuri ambazo inazifanya hususan maeneo yetu ambako tunatoka. Kwa hiyo, nashukuru. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuishukuru Serikali hasa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Eng. Kamwelwe, Waziri wetu na Manaibu wake pia Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara nzima, nianze kuiongelea barabara ya Itoni – Njombe – Ludewa – Manda. Barabara hii imewekwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na barabara hii kwa kweli ina urefu wa kilometa 211.6 mpaka kufika kule Manda. Itajengwa katika lots nne na kwa sasa imeanza ujenzi wa lot Na. 2, Lusitu - Mawengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii, hivi tunavyoongea toka ilipoanza kujengwa ilipaswa iwe imeisha lakini mpaka sasa barabara hii haijaisha. Kwa hiyo, naiomba Serikali sasa ijaribu kufanya jitihada za haraka ili kipande hiki korofi kiishe.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna eneo la Lusitu kwenda pale Itoni, lot Na. 1, kwa kweli kipande hiki kinasumbua sana. Hivi ninavyozungumza, malori mengi sana yamekwama kwenye maeneo ya Njomlole kule, maeneo ya Luponde na kusababisha adha kubwa ya usafiri mpaka ikapelekea wiki iliyopita baadhi ya wenye magari kutokupeleka magari Ludewa kwa sababu ya adha hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba sasa Serikali angalau itufikirie kwa kipande cha kutoka Itoni kwenda Lusitu na wakati huo huo ile barabara ya Mawengi - Lusitu ikifanyiwa jitihada kubwa. Kwa sababu nakumbuka Mheshimiwa Waziri alikuja mwezi wa Nane akaona na akatoa maagizo, lakini inaonekana kama yale maagizo hayakufanyiwa kazi kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuipongeza Serikali kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya kutoka Mkiu – Liganga – Madaba na ule wa kutoka Mchuchuma kwenda Liganga. Kwa kweli barabara hizi ni muhimu, upembuzi umefanyika. Sasa naiomba Serikali iweke jitihada kubwa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa lami ya barabara hizi kwa sababu barabara hizi ndiyo zinakwenda kwenye ile miradi ambayo tunaita ni flagship projects ya Liganga na Mchuchuma. Kwa hiyo, naiomba Serikali ifanye jitihada za haraka kwa sababu ya umuhimu wa maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naishukuru Serikali kwa kuiweka kwenye mpango wake wa Bajeti wa kuifungua barabara inayopita kando kando ya Ziwa Nyasa; barabara kutoka Lupingu – Makonde - Lumbila mpaka Matema. Kwa hiyo, naiomba Serikali sasa iweke misisitizo mkubwa kwa sababu eneo hili la Ziwa Nyasa ni eneo la Kitalii na pia ni eneo la kiulinzi na usalama. Kwa hiyo, ninaamini kwamba kazi hii mtaifanya na mtaifanya kwa kutumia nguvu kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie daraja la Mto Ruhuhu. Daraja la Mto Ruhuhu lilipaswa liishe toka mwaka 2017, lakini mpaka leo hii daraja hili halijaisha na daraja hili lipo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Kwa hiyo, tunaomba basi mwaka huu hili daraja likamilike ili lipitishe wananchi ambao wanatoka Ludewa kuelekea kule Nyasa, kwa sababu kwa mwaka 2018 tu, tayari wananchi zaidi ya watano wameliwa na mamba kwenye mto huu huu kwa sababu ya kutokuwepo kwa daraja pale. watu wanapita kwa mitumbwi na wakati mwingine hata ile Panton iliyopo pale inakuwa haifanyi kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali na kusisitizia kwamba ikiwezekana hili daraja liishe mwaka huu kama ambavyo Mheshimiwa Waziri ameniahidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuipongeza Mamlaka ya Bandari Tanzania kwa kazi inayofanya kule Ziwa Nyasa. Tumeona Mheshimiwa Nditiye akiwepo pale na bahati nzuri na Mkurugenzi Mkuu wa Bandari tumekuwa tukiwasiliana mara kwa mara. Kwa hiyo, nashukuru kwa kunipa tu vile vituo vya kupakia na kupakua abiria na mizigo ili kuweza kuwarahisishia wale wananchi wanaoishi Kanda ile, usafiri wa kutoka eneo moja kwenda eneo lingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile napenda kushukuru Wizara kwa ajili ya minara ya mawasiliano ya simu. Minara hii tayari imeshajengwa na iliweza kuwaka kwa siku tatu tu lakini mpaka sasa hivi imezima. (Makofi)
Kwa hiyo naomba sasa Wizara kupitia mawasiliano kwa wote, kazi waliyoifanya ni kubwa na kazi waliyoifanya ni nzuri, niwapongeze na nimpongeze Mheshimiwa Engineer Ulanga na timu yake yote na nimpongeze Mheshimiwa Waziri, kazi hii ni njema lakini wale watu wanasubiri kwa kiasi kikubwa mawasiliano kwa sababu mawasiliano yamekuwa ni tatizo kubwa kwao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niiongelee kidogo TTCL ni Shirika letu, Shirika la nchi na la umma, kuna haja ya kuweka utaratibu mzuri ili iweze kushindana na taasisi nyingine hasa kwenye eneo la manunuzi. Manunuzi inavyoonesha kwamba inachukua muda mrefu kiasi ambacho hawawezi ku- compete na wenzao. Wenzao wao private sectors wao wanafanya mambo yao kiurahisi, kwa hiyo kuna haja ya Serikali sasa kuipa uwezo wa kujiendesha yenyewe na hizi sheria za manunuzi tuweze kuzirekebisha ili hili shirika liweze kujiendesha vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)