Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia Wizara ya Miundombinu. Umesema leo tujifunze kwa Mheshimiwa Abbasi kutokupiga kelele, tunasikika tu, ngoja nianze kujaribu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe pongezi zangu za dhati kwa Serikali na Wizara nzima ya Ujenzi pamoja na miundombinu, Mheshimiwa Waziri, Manaibu Waziri, Mheshimiwa Nditiye na kaka yangu Mheshimiwa Kwandikwa, tunawapongeza sana kwa kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizipongeze pia taasisi zote zilizo chini ya Wizara hii TPA, SUMATRA, TCRA, RAILWAY, TANROADS, TCAA, TASAC, CATCO, ATCL, UCSAF na zingine zote, kwa kweli wanafanya kazi vizuri sana. Nimeingia kwenye Kamati hii ya Miundombinu muda mfupi tu, nimeona kwa kweli kazi inayofanyika ni nzuri na ni kubwa, tunawapongeza sana na tunataka waendelee kumuuunga mkono Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaanza kuchangia naomba niongee kidogo kuhusu mdogo wangu Mheshimiwa Makamba, jana alichangia akasema kwa nini Serikali imehamisha kitengo cha Wizara kinachohusika na ununuzi wa ndege na kukipeleka Ikulu, wanaficha nini. Naomba tu nimwambie hayupo lakini najua taarifa atazipata kwamba Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kikatiba anayo mamlaka ya kuhamisha Wizara yoyote, kuhamisha Taasisi yoyote ya Serikali, kuipeleka popote anapotaka yeye. Anayo mamlaka ya kuanzisha leo mkoa mpya na kesho kuuvunja, anayo Mamlaka ya kumteua Waziri na kesho kumtumbua na anayo Mamlaka ya kuteuza Katibu Mkuu na kesho kuondoa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kama wanaona kwamba Mheshimiwa Rais alihamisha ile taasisi kwa kuficha kitu sidhani kama wanawaza vizuri, nadhani saa nyingine wanaropoka au wamechanganyikiwa, wakijua kabisa kama Mheshimiwa Makamba anajua kabisa Katiba ya Jamhuri ya Muungano inampa uwezo huo Mheshimiwa Rais. Mfano tulikuwa na Wizara ya Nishati na Madini akazitenganisha, anaficha kitu gani yote hiyo ni kutaka efficiency, kazi zake ziende vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, TAMISEMI ilikuwa chini ya Waziri Mkuu ameihamishia Ikulu anaficha nini? Yote hiyo ni kutaka kazi zisimamiwe vizuri. Kwa hiyo, sisi tunaendelea kumpongeza Rais na tunamwambia aendelee kufanya kazi kadiri atakavyoona mafanikio yatakuwa makubwa na ni mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wanasema Shirika la Ndege halina faida wala maana yoyote. Nimeshukuru kaka yangu Mheshimiwa Abbas ameelezea vizuri faida zake, lakini shirika hili la ndege ni identity, ni utambulisho wetu Watanzania na lina faida kubwa sana. Faida yake si tiketi tu, Emirates, Ethiopia Airline, Quatar hawajawahi kupata faida kwenye tiketi wanapata faida kwenye mambo mengine, kwenye mzunguko kama alivyosema kaka yangu Mheshimiwa Abbas, siwezi kurudia, ndivyo faida inavyopatikana. Kwa hiyo, mambo haya ya kusema ndege hazina maana, ndege zina maana kubwa, naipongeza Serikali yangu imeweka bajeti ya kuongeza ndege nyingine, naomba iongeze ili tuendelee kufanya vizuri jambo ambalo wao hawakutegemea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kelele zilizopigwa nchi hii ni shirika la ATCL kufa. Leo Mheshimiwa Rais amejitokeza kulirejesha shirika hili ni lazima alisimamie kikamilifu ili isije tena ikajitokeza hali ile kama ilivyokuwa mwanzo. Kwa hiyo, mimi naungana naye mkono kuhamisha kitengo hicho kukiweka Ikulu ili usimamizi wake uwe wa karibu zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika legacy atakazoziacha Mheshimiwa Rais wetu ni pamoja na Shirika la Ndege na reli. Leo reli ya Dar-es-Salaam – Morogoro ya Standard Gauge inayojengwa imeshafika asilimia 50, lakini pia kuna Phase II inayojengwa na yenyewe inaendelea vizuri na tunaomba Mungu iendelee vizuri na iishe ili na sisi Tabora tuingie sasa Phase III. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Uwanja wa KIA kuna hangar ilijengwa muda mrefu, niiombe Serikali iboreshe hangar hiyo ili ndege zetu sasa ziweze kutengenezwa Tanzania. Tuna hangar kubwa mpaka dreamliner inaingia. Kwa hiyo, sioni tena sababu ya kuchukua ndege kuzipeleka nchi za nje kwenda kutengenezwa, tuna ma-engineer zaidi ya 60 ambao wana uwezo wa kutengeneza ndege.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwombe Waziri na Serikali kwa ujumla ihakikishe imeboresha hangar ile ndege zetu sasa zifanyiwe ukarabati ndani ya nchi yetu na sio kupeleka nje. Hiyo iambatane pia na Uwanja wa Ndege wa KIA uendelee kukarabatiwa, uongezwe parking na mambo mengine kwa sababu uwanja ule sasa umeshakuwa mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jana pia waliongelea kuhusu bandari. Mimi niipongeze Mamlaka ya Bandari, kazi ni nzuri, sasa mizigo inatoka haraka siyo kama ilivyokuwa mwanzo, kwa kweli wanajitahidi kwa kiwango kikubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nimesikia Mkurugenzi wa Bandari amelaumiwa kwa kuwafanyisha watumishi kazi mpaka saa 7.00 za usiku; mimi nimpongeze sana, dunia nzima watu wanafanya kazi saa 24 sehemu kubwa kama zile. Yeye ni kupanga shift zao kwamba nani ataingia mpaka saa 10.00, nani ataingia mpaka saa 5.00 ya usiku na nani ataingia mpaka alfajiri ili kuweka mambo sawa na ili bandari yetu iende na wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi kubwa inayofanywa ya kupanua hizi bandari inabidi ziende na wakati. Kwa hiyo, kitu cha muhimu ni kupanga shift na nawapongeza sana. Yule aliyekuwa analaumu kwa nini wanafanya kazi mpaka saa 7.00 ya usiku nadhani hajatembea, atembee duniani, dunia nzima watu wanafanya kazi saa 24. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naongea kuhusu SUMATRA. SUMATRA kuna kitengo kimeanzishwa kinaitwa VTS (Vehicle Tracking System) ambapo sasa hivi mabasi yetu yamefungwa kifaa hiki akitembea mbio au akifanya nini anaonekana moja kwa moja kule Dar es Salaam. Haya ni maendeleo makubwa sana ya Serikali ya Awamu ya Tano, tunaipongeza Wizara ya Ujenzi na Mawaziri na Manaibu wote kwa kazi hii nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Muda wako umeisha Mheshimiwa, kengele imeshagonga. Ahsante sana.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)