Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Dua William Nkurua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyumbu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. WILLIAM D. NKURUA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Natoa pongezi kwa Serikali na Wizara kwa kazi nzuri wanazozifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu muda si rafiki, nakwenda moja kwa moja kwenye Jimbo langu la Nanyumbu. Hapa naanza na watu wa ujenzi; napenda niwakumbushe kwamba Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, alitoa ahadi ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami toka Nangomba mpaka Nanyumbu. Barabara hii ni barabara inayoelekea nchi jirani ya Msumbiji, ni barabara muhimu sana kwa uchumi wa Tanzania. Kwa hiyo naomba Serikali katika vipaumbele vyake iiweke barabara ya kutoka Nagomba hadi Nanyumbu kwa sababu wananchi wana imani sana na ahadi ile na ukizingatia kwamba viongozi hawa wanakuwa wakweli. Kwa hiyo, naomba Serikali iiweke katika mpango wake ujenzi wa barabara kutoka Nangomba hadi Nanyumbu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda Sekta ya Mawasiliano, naupongeza sana Mfuko kwa kazi kubwa inayofanya na kwenye Wilaya yangu ya Nanyumbu nataka niwape maeneo muhimu ambayo kwenye bajeti hii tuyazingatie. Kwanza kabisa nataka Kata yangu ya Napacho; kata hii ina shida kubwa ya mawasiliano, hasa kwenye Vijiji vya Mpombe, Ndekela, Mburusa, Napacho, Kazamoyo na Chimika, hawa watu mawasiliano ni magumu sana, naomba eneo hili tutafute eneo tuweke mnara, tukiweka mnara mmoja katika eneo hili tutahakikisha kwamba wananchi watapata mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Kata ya Likokona; kata hii pia haina mawasiliano, hata makao makuu ya kata mawasiliano ni magumu sana. Kwa hiyo naomba tutafute namna ya kuhakikisha kwamba Likokona na Vijiji vyake vya Msinyasi, Namaka na vitongoji vyake vipate mawasiliano ya kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile naongeza Kata ya Mkonona; kata hii ina Kijiji cha Mbangara Mbuyuni na Kitongoji chake cha Wanika, mawasiliano hayapatikani kabisa. Kwa hiyo naomba Serikali itupatie mnara kwenye kata hii ili wananchi wa kata hii nao wapate mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la mwisho kwa mawasiliano ni Kata ya Maratani katika Wilaya ya Nanyumbu. Kata hii pia ina Vijiji vya Maratani, Malema na Mchangani B, havina mawasiliano kabisa. Naomba tupatiwe mnara katika maeneo hayo kutokana na viwango vyao vya kutambua wapi tuweke mnara ili vijiji hivi nilivyovitaja vipate mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri; minara hii itakayojengwa ijengwe kwa viwango ambavyo tutapeleka mawasiliano kama ilivyokusudiwa kwa sababu kuna baadhi ya vijiji minara imejengwa lakini haifanyi kazi ilivyokusudiwa. Kwa mfano, ukienda kwenye Kata ya Sengenya, Kijiji cha Sengenya, kuna mnara pale lakini mnara ule hata pale kijijini haufanyi kazi vizuri. Kwa hiyo naomba Serikali tunapoweka hii minara tuhakikishe kwamba inafanya kazi tuliyokusudia.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda Kata ya Mkonona, Kijiji cha Marumba, kuna mnara wa TTCL pale, lakini mnara ule haufiki hata kilometa tano, Vitongoji vyake vya Namaromba network haipatikani kule. Kwa hiyo naomba tutakapokwenda kupeleka minara hii, vijiji hivi na vitongoji vyake viweze kupata network na wananchi wetu waweze kupata mawasiliano kama tulivyokusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu muda si rafiki, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)