Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Andrew John Chenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. ANDREW J. CHENGE: Mheshimiwa Spika, nikishukuru sana kwa kunipatia nafasi hii ili nami nichangie kwa ufupi tu.

Mheshimiwa Spika nipongeze kazi nzuri inayofanywa na Wizara hii kwenye maeneo muhimu ya ujenzi wa barabara, mawasiliano na uchukuzi. Hongereni sana, naelewa rasilimali fedha ndiyo zinatusumbua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jana nimetoka Bariadi kuja Dodoma nimeona kazi nzuri inayofanywa kati ya Bariadi na Maswa, mkandarasi anaendelea na pesa imetengwa tena. Tungependa tukamilishe barabara hii ikiwezekana mapema mwaka huu au mwaka kesho tuweze kutoka moja kwa moja Dar es Salaam – Dodoma – Shinyanga – Mwigumbi –Bariadi – Lamadi – Musoma – Sirari - Nairobi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Bariadi imekaa katikati kwa ukanda wa Kaskazini Mashariki mwa Tanzania na ndiyo maana tunasema sana barabara, tulitegemea katika Mwaka huu ujao wa fedha angalau kipande cha Bariadi kuja Moboko-Mwanuzi mpaka Sibiti kingeliweza kufanyiwa feasibility study yaani upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Lakini naona siioni kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri hata kwenye majedwali yale ya kipande hiki hakipo, tunaendelea kuiomba Serikali kwamba tuunganishwe na mikoa jirani ya Singida na Arusha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine mkisoma hotuba za Wizara hii kwa miaka mitatu iliyopita barabara ya Kolandoto, Munze, Lalago mpaka Thibiti ilikuwa inaenda mpaka Matala - Mang’ola na Odiang Junction. Sasa hivi tunaongelea kasehemu kadogo tu, tumeanzisha mradi mzuri tu huu wa kutoka Karatu, Mbulu, Haydom, Sibiti, Lalago Maswa. Ningependa Serikali ituambie kwa kazi iliyofanyika kwa kipande cha kutoka Sibiti, Matala, Mang’ola na Odiang Junction ile sehemu tunaiacha au tunaendelea nayo? Ningependa nipewe majibu na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nije kwenye upande wa barabara, mimi kuna barabara nasema kwa sababu tunajua hali ya Tanzania iliyvyo kuna maeneo mengine ni ukame, mengine yana hali nzuri ya barabara, naendelea nashukuru Serikali nimeona upande wa barabara ya Kidatu – Ifakara - Tupilo kuelekea Malinyi - Londo mpaka Lumecha Songea nashukuru sana kwa sababu tukiweza kukamilisha barabara hii tunafungua njia ambayo eneo lenye utajiri mkubwa sana wa chakula na hali nzuri ya hewa. Lakini ningependa tuangalie pia uwezekano wa kutoka Ifakara twende Kihansi, twende Mlimba, twende Taweta, twende mpaka Madeke, twende mpaka Lupembe maana tukiyabeba haya yote unaifungua sehemu hiyo yenye utajiri na kuweza kupeleka chakula kwa haraka katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho naomba tunafanya kazi nzuri katika kupanua Bandari ya Dar es Salaam, napongeza Serikali lakini nasema mwaka jana nilishauri reli yetu ya kati hii tunayoijenga sasa hivi ni afadhali tukachukua mkopo wa muda mrefu kuliko hii ya mikopo ya masharti ya muda mfupi ambayo yatakuja kutuumiza, maana hata kabla hatujaanza kuitumia reli hii tutaanza kulipa madeni haya. Lakini tukichukua madeni ya muda mrefu na kwa masharti nafuu tunajenga reli hii tukamilisha yote kwa wakati mmoja ili tuweze kupata faida ya uamuzi mzuri huu unaofanywa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwa bandari ya Dar es Salaam itatusaidia kwa muda mfupi tu. Duban na Bellair na sasa Nakala lakini upande wa Lam na Mombasa wenzetu hawa wanaangalia mbali sana, tungependa na sisi Bandari hizi Mungu ametupa nafasi nzuri sana, Bandari ya Mtwara, Bandari ya Dar es Salaam, Bandari ya Bagamoyo Mbegani narudia kuishauri Serikali na Mwambani hizi kwa upande wetu wa Tanzania zikiweza hizi zikajengwa, hii ndio future ya Tanzania kuunganisha na nchi za Maziwa Makuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ningependa sana Bunge lako tuendelee kuishauri Serikali waone faida ya haya. Najua muda wangu ndio huo lakini nikushukuru sana kwa nafasi uliyonipa, naishukuru Serikali kwa haya wanayoyafanya, niungane na Mheshimiwa Serukamba kwamba tuangalie kwa haraka na sio kupoteza muda, sekta binafsi ishirikiane na sekta ya Umma kwa PPP katika kuyafanya mengi haya na tusiogope. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)