Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Eng. Christopher Kajoro Chizza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buyungu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Nitaongelea mambo mawili tu. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Mawaziri na viongozi wote wa Wizara hiyo kwa kuleta hotuba nzuri sana.

Mheshimiwa Spika, nataka niongelee mambo mawili tu; moja ni Mfuko wa Barabara; la pili ni kasi ya ujenzi wa barabara za lami hususan katika Mkoa wa Kigoma.

Mheshimiwa Spika, kabla hatujaingia kwenye uchumi wa kati na uchumi wa viwanda bado Watanzania tunategemea kilimo na tutaendelea kutegemea kilimo kama ndiyo mhimili wa uchumi wetu. Wataalam wanasema asilimia 60 ya upotevu wa mazao hutokea katika level ile ya postharvest, yaani miundombinu hafifu ya kuhifadhi mazao, lakini pia miundombinu hafifu ya kusafirisha mazao kutoka shambani kwenda sokoni (farm to market roads). Hapa ndipo ninapotaka kusisitiza umuhimu wa Mfuko huu wa Barabara. Nikitazama kwa mfano mkoa wangu wa Kigoma wote kwa pamoja tumetengewa shlingi milioni 694 ndizo ninazoziona kwenye kitabu hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, barabara hizi ambazo ndizo zinatarajiwa zinategemewa na wakulima watoe mazao yao wasafirishe sasa waje kwenye truck road tunazojinga, kupeleka sokoni, bado bado sana. Kwa kweli tunahitaji mfuko huu upate pesa, TARURA wapate pesa tuwajengee wakulima miundombinu ya barabara waweze kutoa mazao yao kwenda shambani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niunganishe hapa hapa kwamba katika Jimbo langu kule tumejenga soko la kisasa, la Kimataifa katika Kijiji cha Muhange, soko ambalo litatufanya sisi tuunganishe tufanye biashara na wenzetu wa Burundi. Soko hili ili liweze kufanya kazi vizuri sasa, ni muhimu barabara ile inayojengwa kutoka Nyakanazi kwenda mpaka Kigoma ipate barabara ya kiungo kutoka Kakonko kupita Kinonko, kwenda Gwarama, kwenda mpaka Muhange sokoni ili sasa wananchi wetu waweze kufanya biashara na ndugu zao wa Burundi kwa kutumia barabara nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakwenda haraka kidogo. Miundombinu hii tunayoijenga sisi watu tunaotoka Kigoma; kuufungua Mkoa wa Kigoma tunahitaji sasa miundombinu hii ijengwe kwa kasi kubwa ili mkoa huu uweze kuwa hub ya biashara hususan katika baadhi ya nchi za maziwa makuu. Tatizo tulilonalo kama nilivyosema awali ni usimamizi au ucheleweshaji wa ujenzi wa barabara hizi.

Mheshimiwa Spika, barabara ya kutoka Nyakanazi, mpaka Kabingo pale kijijini kwangu mpaka hivi tunavyozungumza tangu mwaka 2014 ni asilimia 60 tu ambazo zimetekelezwa tangu 2014. Tumeikagua tukiwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu tukakuta hata Mkandarasi mwenyewe yuko nje ya mkataba (out of contract) kwa siku 986. Naiomba Wizara isimamie kwa karibu Mkandarasi anayejenga barabara hii Nyakanazi mpaka pale Kabingo ili aweze kuongeza kasi ya utekelezaji. 2014 - 2019 asilimia 60, kwa kweli tunaendelea kuchelewa sana.

Mheshimiwa Spika, naomba tu nimalizie kwa kuishukuru Serikali. Nimeona katika kitabu sasa, mmesema kutoka Kabingo kwenda Kasulu kwenda Kibondo Kasulu hadi Manyovu, Benki ya Maendeleo ya Afrika imetutengea shilingi bilioni 15 ili tuweze kujenga kilomita hizi 260 za barabara hii. Huu ndiyo mwendo ambao kwa kweli kama tutatekeleza, hii itapelekea kufungua…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)