Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Mussa Bakari Mbarouk

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Spika, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu na pia kuwatakia Waislamu wote Tanzania na duniani kwa ujumla, Mfungo mwema wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Mheshimiwa Spika, barabara ya Pangani ni miongoni mwa barabara za kimkakati na ni miongoni mwa barabara inayounganisha Mikoa na Wilaya. Pangani road inaanza Mkoa wa Tanga na kupitia Wilaya za Muheza, Pangani na Chalinze Mkoa wa Pwani na Dar es Salaam. Pia barabara hii inaunganisha nchi za Afrika Mashariki kwa barabara kuu itokayo Mombasa - Kenya kupitia Tanzania na hadi Nchi za Kusini mwa Bara la Afrika.

Mheshimiwa Spika, barabara hii imewekewa ahadi na Marais wanne ambao sasa ni wastaafu ambao Julius K. Nyerere, Mzee Ally Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete. Pamoja na fedha kupatikana (bajeti) upumbuzi yakinifu tayari na mkandarasi ameshapatikana, naiomba Serikali itoe tamko ni lini barabara ya Pangani itaanza kujengwa rasmi?

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa barabara kwa changarawe. Barabara zifuatazo katika kitabu cha bajeti na sijaziona, naomba zitengewe fedha:-

(i) Barabara ya Mabokweni-Maramba-Daluni-Korogwe;

(ii) Barabara ya Kirare-Mapojoni-Mkembe;

(iii) Barabara ya Amboni-Mleni-Rubawa-Pangarawe;

(iv) Barabara ya Pongwe-Marungu-Geza; na

(v) Barabara ya Fuweni-Mondura-Mwarongo.

Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali iongeze fedha katika bajeti hii ili barabara hizi ziweze kupitikana wakati wote wa mwaka.

Mheshimiwa Spika, Bandari ya Tanga ni miongoni mwa bandari za kihistoria duniani. Kama tunavyojua, bandari ni lango kuu la biashara lakini haitumiki ipasavyo pamoja na kufanyiwa ukarabati wa shilingi bilioni 1.8 na crane ya 40Ft mpya bado kuna upungufu wa vifaa vingi.

Mheshimiwa Spika, nashauri bandari hii ipatiwe fedha za kutosha kwa ajili ya vifaa bora na vya kisasa. Serikali na Mamlaka ya TPA ifanye utaratibu wa kupanga aina za mizigo (categories) kwa kila mandarin. Bandari ya Tanga ichukue mizigo ya Tanga, Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Musoma na Bukoba bila kusahau mizigo ya Uganda, Rwanda na Burundi. Bandari ya Mtwara (Mtwara Corridor) ichukue mizigo ya Mtwara, Mbeya, Sumbawanga, Katavi, Kigoma, Iringa bila kusahau mizigo ya Zambia, Malawi na Congo DRC. Bandari ya Dar es Salaam ni kuipa mizigo mikubwa sana. Dar es Salaam Port kwa kuifanya ishughulikie mizigo yote inayotoka nchi za nje matokeo yake meli zinasubiri muda mrefu sana na kuwa ni sababu ya baadhi ya makampuni ya meli kuikimbia Bandari ya Dar es Salaam na kushushia mizigo Mombasa port, Beira na Maputo. Hivyo, naiomba Serikali ifanye categories za mizigo na Bandari zote za Tanga, Zanzibar, Dar es Salaam na Mtwara zifanye kazi kwa faida.

Mheshimiwa Spika, Bandari Bubu ziboreshwe. Bandari Bubu Tanzania ni jambo lisiloepukika kwa kuwa Watanzania wanafanya kazi za usafirishaji kupitia maji (bahari, mito, maziwa). Bila kuathiri huduma hii kwa wananchi ni vyema Bandari Bubu zikafanyiwa tathmini na zinazokidhi vigezo zikarasimishwa (kuboreshwa) na kuwa chanzo cha mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Tanga tunazo Bandari Bubu katika maeneo ya Moa, Jasini, Monga, Tongoni, Mwarongo, Marungu (Tanga Mjini), Kigombe (Muheza), Kipumbwi na Mkwaja. Nashauri Bandari Bubu za Kigombe (Muheza) na Kipumbwi (Pangani) ziboreshwe kwa kujengewa majengo bora ya TRA, TPA kwa ajili ya kukusanya mapato ya Serikali ya forodha na kodi mbalimbali. Bandari hizi zikiboreshwa zitaongeza mapato ya Serikali na pia itaongeza ajira na kuongeza mzunguko wa fedha kwa wananchi (wafanyabiashara) wa maeneo husika.

Mheshimiwa Spika, minara ya simu/mawasiliano. Moja ya vigezo vya maendeleo ni mwasiliano ya uhakika. Yapo maeneo katika Jimbo/Jiji la Tanga hakuna mawasiliano ya uhakika. Unapotaka kuongea na simu lazima upande ju ya mti, kichuguu au katika maeneo maalum hali inayopelekea wananchi kupata shida ya mawasiliano hususani katika kipindi cha dharura yoyote inapotokea au hata katika shughuli za biashara. Maeneo hayo baadhi ni Kata za Marungu, Tongoni, Mzizima, Mabokweni, Kiomoni na Maweni. Naishauri Serikali kwa kushirikiana na Makampuni ya simu (Tigo, Airtel, Zantel, TTCL na Vodacom) kuongeza minara.