Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlalo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, napenda kuchangia hoja hii kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya Mkinga – Maramba – Mng’aro, Mlalo hadi Lushoto ipo chini ya Wakala wa Barabara ya Mkoa. Barabara hii inaunganisha Wilaya za Mkinga na Lushoto, lakini pia na pacha ya kwenda Korogwe na wilaya jirani ya Same Mkoani Kilimanjaro.
Mheshimiwa Spika, mara zote kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo barabara hii tumekuwa tukiipitisha katika vikao vyetu vya RCC ili itengewe fedha kwa ajili ya upembuzi na usanifu wa kina (detailed design) mara zote inapofika katika ngazi ya Taifa, budgets inakatwa. Tunataka kujua kulikoni? Tanga - Lushoto tunakosea wapi? Barabara hii Lushoto - Mlalo yenye kilometa 45 ni muhimu sana na kiungo kikubwa cha uchumi kwa wananchi wa Usambara. Tunataka kujua kwa nini?
Mheshimiwa Spika, sisi tunaipanga barabara hii katika mipango yetu kwa kuzingatia vipaumbele. Tunapenda kupata taarifa rasmi kutoka Serikalini. Hivyo Serikali itoe umuhimu wa kipekee kwa barabara hii angalau hata ijengwe kwa kiwango cha lami hata kwa awamu za kilomita 10 kwa kila mwaka. Vinginevyo kutokana na jiografia ya Lushoto ilivyo, ikibaki kwa kiwango cha changarawe, Serikali inapoteza pesa nyingi sana katika periodic maintenance.
Mheshimiwa Spika, nchi yetu ina viwanda 14 vinavyochakata samaki katika Mikoa ya Mara, Mwanza na Kagera, lakini kwa bahati mbaya kutokana na kutokuwa na ndege za mizigo, minofu hii inasafirishwa kwenda Nairobi na Entebe hata Kigali ambako wenzetu wanapata mapato ya export.
Mheshimiwa Spika, hivyo, nashauri, pamoja na ndege za abiria, Serikali iweke mkazo kuanzisha mchakato wa kununua ndege za mizigo ili pia viwanja mbalimbali vinavyoboreshwa viweze kutumika kusafirisha mazao mbalimbali kwenda nje ya nchi kwa masoko.
Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali itazame upya gharama zetu za viwanja vya ndege ili viweze kuvutia hata ndege za mizigo kuweza kutua katika viwanja vyetu.
Mheshimiwa Spika, shirika letu la ndege ATCL linafanya vizuri sana lakini bado linakumbana na ushindani mkubwa kutoka mashirika ya ndege ya Kimataifa.
Mheshimiwa Spika, kwa bahati mbaya sana hata wenzetu katika Kanda ya Afrika Mashariki miradi hii wanaichukulia kama miradi ya kimkakati, hivyo kusimamiwa na Serikali nzima tofauti na hapa kwetu ambapo jukumu hilo imeachwa kwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi pekee.
Mheshimiwa Spika, Mashirika kama Emirates, Turkish, RwandAir ni sehemu ya kukuza utalii na biashara ya Kimataifa katika nchi zao. Mfano, RwandAir inatumika kuitangaza Kigali kuwa kituo cha utalii wa mikutano ya Kimataifa. Ethiopian Airways inajulikana kwa kuchangia pato la nchi hiyo kupitia sekta hii ya usafirishaji. Turkish Airline inasifika kwa kuifanya Uturuki kuwa kituo kikubwa cha biashara katika Bara la Ulaya na Bara la Asia. Qatar Airways imeubadili mji wa Doha na kuwa kituo kikubwa cha biashara cha Asia na kuhakikisha kuwa mji wa Doha unakuwa kiunganishi muhimu cha ndege zote za Kimataifa kwenda maeneo tofauti duniani.
Mheshimiwa Spika, kwa mtazamo na mifano hiyo, ATCL inawezaje kuhimili ushindani na mashirika haya ikiwa huko kwao yana misamaha ya kodi, hayalipi gharama za kutua viwanjani na uongozaji wa ndege yanaendesha au ni sehemu ya mfumo wa uendeshaji ya viwanja vikubwa vya ndege (mfano, Dubai Kigali, Doha na Addis Ababa) yanamiliki kampuni za kutoa huduma viwanjani (ground handling company), yanamiliki kampuni za kutayarisha vyakula vinavyotumika ndani ya ndege (inflight catering) na hata kumiliki shule za kutayarisha wafanyakazi wa karakana za utengenezaji wa ndege kwa mashirika mengine ya ndege. Kwa bahati mbaya gharama zote hizi hapa kwetu zimeachwa chini ya Shirika la ATCL.
Mheshimiwa Spika, gharama za uendeshaji wa ATCL ambazo zinatokana na utoaji wa huduma zinazotolewa na mashirika ya Serikali ambazo zinaweza kutazamwa kama walivyofanya wenzetu kwa mashirika yao.
Mheshimiwa Spika, tusipoitazama ATCL kama uwekezaji wa kimkakati wa Kitaifa wenye nia ya kuwezesha sekta nyingine, hapo baadaye tutakwama, suala linaweza kuchukuliwa kwamba ni biashara ya muda mfupi, lakini tukilipa mtizamo wa Kitaifa litakuwa na tija ambayo ndiyo dhumuni kubwa ya kulifufua Shirika hili.
Mheshimiwa Spika, hivyo, badala ya kung’ang’ania tozo la gharama za kutua uwanjani na uongozaji ndege (landing and air navigation charges) ni vyema kuitazama ATCL kama sehemu ya utoaji huduma hizo isiyohitaji kulipiwa.
Mheshimiwa Spika, mwisho, lakini siyo kwa umuhimu, uwanja wa ndege wa Tanga unapaswa kufanyiwa ukarabati ili nasi tuweze kusafiri na kusafirisha bidhaa zetu kwenda kwenye masoko ya Kimataifa.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.