Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Eng. Atashasta Justus Nditiye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa, naomba nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa nafasi aliyotupatia kukutana mahali hapa kwa ajili ya kujadili mambo muhimu yanahusu nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, pili, nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa majukumu mengi sana anayofanya kwa ajili ya nchi yetu. Nimpongeze vilevile kwa majukumu mengi anayoendelea nayo na nashukuru kwa kuniamini niweze kumsaidia.

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee kabisa, nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Mhandisi Isack Aloyce Kamwelwe, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa support kubwa anayonipatia katika kutekeleza majukumu yangu. Nichukue nafasi hii vilevile kumpongeza sana na kumshukuru pacha wangu Naibu Waziri wa Wizara hii ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayehusika na Ujenzi, Mheshimiwa Eliasi John Kwandikwa bila kuwasahau watendaji wote nikianza na Mhandisi Dkt. Chamuriho (Katibu Mkuu wa Uchukuzi), Mhandisi Dkt. Maria Sasabo (Katibu Mkuu wa Mawasiliano) na Arch. Mwakalinga (Katibu Mkuu wa Ujenzi).

Mheshimiwa Spika, napenda kuishukuru sana Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kwa maelekezo na misaada mbalimbali wanayoipatia Wizara yetu katika kutekeleza majukumu yake. Nichukue nafasi hii niwashukuru Wabunge wote kwa ushirikiano, urafiki na ukarimu ambao wanaitendea Wizara yetu katika kutekeleza majukumu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawashukuru sana wapiga kura wangu wa Jimbo la Muhambwe lililoko Mkoa wa Kigoma, Wilaya ya Kibondo. Vilevile naishukuru familia yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipatia nafasi hii na mimi niweze kuchangia hoja iliyo mbele yetu. Kwa sababu ya muda nitajaribu kujieleza kwa baadhi ya hoja chache tu, kwa upande wa uchukuzi nitagusia masuala ya hali ya hewa lakini nitagusia miradi miwili mikubwa ya kimkakati ya reli ya kutoka Tanga - Musoma na Mtwara - Mbambabay. Nikipata nafasi nzuri nitagusia masuala mazima ya ATCL lakini kwenye mawasiliano nitazungumzia suala la usajili wa laini za simu pamoja na utendaji wa UCSAF.

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee, kwanza, nitoe pole kwa Watanzania wenzetu ambao wamepata madhara sehemu mbalimbali kutokana na mvua nyingi na kubwa zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Sasa hivi Mkoa wa Dar es Salaam na maeneo kadhaa ya Pwani yame-experience mafuriko ambayo yanaendelea, tunaona kwenye mitandao ya kijamii na sehemu mbalimbali na tunapigiwa simu hata na ndugu zetu kwamba hali si nzuri sana kwa Mkoa wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, niipongeze Mamlaka ya Hali ya Hewa imekuwa ikifanya kazi nzuri sana ya kuwaelimisha Watanzania juu ya athari ambazo zitatokea kwa siku zijazo kutokana na vifaa vya kisasa wanavyovitumia. Itakumbukwa kwamba tarehe 21 Aprili, 2019, Mamlaka ya Hali ya Hewa walitoa tahadhari kwamba Mikoa ya Kusini Lindi na Mtwara ingekumbwa na kimbunga cha Kenneth. Bahati nzuri tuliendelea sana kuhakikisha kwamba tunatoa tahadhari kwa wananchi lakini Mungu akatuepushia mbali kile kimbunga hakikuweza kutoa athari kubwa. Ilipofika tarehe 24 tuliwatahadharisha tena hata wenzetu wa Mikoa ya Simiyu na Shinyanga kwamba kuna kimbunga ambacho kingetokea kutokea misitu ya Congo kingeweza kuathiri maeneo ya Kahama na tulishuhudia kwamba kulikuwa na mafuriko yaliyotokea.

Mheshimiwa Spika, hili najaribu kuwaelezea baadhi ya Wabunge ambao walithubutu kusema kwamba Mamlaka ya Hali ya Hewa inafanya utabiri kama waganga wa kienyeji, hiyo sio kweli. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania sasa hivi inafanya utabiri wake kwa asilimia 87.8. Katika hali ya kawaida tungepaswa hata kuondoa lile neno utabiri tuwe tunasema tu hali ya hewa kama mataifa yaliyoendelea yanavyofanya. Wakisema kitu kinatokea na sisi kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa tukisema kitu kinatokea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mvua kubwa zinazoendelea kunyesha Mkoani Dar es Salaam na maeneo ya Pwani ni sehemu ya mvua za masika. Nitoe wito kwa Watanzania wenzetu kwamba mvua hizi ni kubwa na zitaendelea kuwepo kwa kipindi chote mpaka mwisho wa mwezi huu. Tunaomba wachukue tahadhari na waendelee kufuatilia taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa. Tumejipanga kuhakikisha kwamba tunawahabarisha Watanzania ili wachukue tahadhari mbalimbali kujiepusha na uharibifu wa mali zao lakini pia na maisha yao.

Mheshimiwa Spika, ili kuwezesha Mamlaka ya Hali ya Hewa kutoa utabiri wa viwango vya kimataifa, Serikali imeendelea kuhakikisha kwamba mamlaka ina wataalam waliobobea katika masuala ya Hali ya Hewa. Aidha, Serikali imeendelea kuhakikisha kuwa Mamlaka inakuwa na vifaa vya kisasa vya kufanya uangazi (observation) na utabiri.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni Serikali imeingia mkataba wa ununuzi wa rada tatu za kisasa za hali ya hewa ambazo zitafungwa katika Mikoa ya Mtwara, Mbeya na Kigoma. Rada itakayofungwa Mtwara itasaidia kufuatilia vimbunga katika bahari ya Hindi, rada itakayofungwa Mbeya itasaidia kuhudumia wakulima kwenye mikoa inayozalisha chakula kwa wingi lakini na rada itakayofungwa Kigoma itasaidia katika kufuatilia na kutoa tahadhari ya matukio ya radi na taarifa muhimu kwa wananchi wanaofanya shughuli zao katika Kanda ya Ziwa Tanganyika na mwambao wa ziwa hilo. Ununuzi wa rada hizo tatu utaifanya Tanzania kuwa na jumla ya rada tano ikijumuisha na rada zilizofungwa Dar es Salaam na Mwanza.

Mheshimiwa Spika, nitaongelea kiasi fulani suala la ujenzi wa reli kati ya Tanga - Musoma. Hatua tuliyofika mpaka sasa hivi kwa upande wa Serikali ni kufanya upembuzi yakinifu lakini tumekwishafanya usanifu wa awali na wa kina, tumekwishajua gharama zinazopaswa. Hatua iliyoko sasa hivi ni kutafuta mwekezaji ambaye ataingia mkataba na Serikali kufanya mradi huo kwa njia ya PPP.

Mheshimiwa Spika, katika kufikia hatua hiyo kuna kitengo ambacho kiko Wizara ya Fedha ambacho ndiyo kinashughulika na mikataba hiyo. Watu wa Wizara ya Fedha wanatusaidia katika kuhakikisha kwamba mikataba itakayoingia na mwekezaji mbia inakuwa na tija kwa nchi yetu. Hatuko tayari kuona kwamba nchi yetu inaingia kwenye mikataba ambayo haina tija kwa wananchi. Sisi tumejipanga kuhakikisha kwamba mikataba yote tutakayoingia inakuwa na tija lakini inawasaidia wananchi kwa kizazi cha sasa, cha kesho na kinachokuja.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kuna wabia wamekuwa wakijitokeza mara kwa mara kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kutaka kuwekeza kwa njia ya PPP kwa reli ya Tanga – Musoma lakini pia kwa reli ya Mtwara - Mbambabay. Hata hivyo, masharti yao wakati mwingine yanakuwa ni magumu sana kutekelezeka na tumekuwa tukiendelea na mazungumzo nao kuhakikisha kwamba mkataba kati yetu sisi Serikali na wao basi unakuwa na tija kwa nchi yetu. Tusiumie lakini na wao wasiumie wapate faida kwa sababu tunategemea waingize hela zao katika shughuli hizo.

Mheshimiwa Spika, vipande vya reli kutoka Tanga - Musoma na kipande cha reli kutoka Mtwara - Mbambabay na matawi yake ya Mchuchuma na Liganga bado yako kwenye mazungumzo na yako mahali pazuri. Itakapofikia mahali muafaka tutawaelewesha Watanzania kwamba sasa tunaingia mkataba kwa ajili kutengeneza reli hizo.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie kidogo suala la ndege zetu za ATCL. Serikali imenunua ndege hizo na kuwapatia ATCL ili wazifanyie biashara warudishe pesa kwa Serikali. Hivi karibuni kumetokea maneno ya manung’uniko kidogo kutoka kwa baadhi ya Waheshimiwa Wabunge kwamba nauli za ATCL zimekuwa kubwa. Ukweli ni kwamba si sahihi, nauli za ATCL bado zimeendelea kuwa ni nafuu kabisa na ndiyo maana Waheshimiwa Wabunge wengi huwa wanakuwa na option namba mbili baada kukosa tiketi za ATCL, ni kwa sababu huduma ni nzuri na nauli zao ni nyepesi.

Mheshimiwa Spika, katika hali ya kawaida tunakubali kuwa na ushindani, kuna ndege nyingine za Precision, ziko ndege za aina mbalimbali na zenyewe zinatoa huduma kwenye njia ambazo ATCL wanafanya kazi. Huwa wanaanza kwa bei nafuu lakini mwisho wa siku wanaenda kuwa na gharama kubwa sana ambazo wateja wao huwa wanakimbilia ATCL. Nakuomba sana tuwashawishi Wabunge waiunge mkono ATCL, ni shirika letu la ndege ili liweze kuendelea kutoa huduma nzuri na za uhakika na ndege zetu ni za uhakika.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo nikiri changamoto ya kuwepo kwa delay za ndege zetu. Nikiri changamoto ya kuwa na cancellation kwenye baadhi ya route. Hilo ni la kweli tumekwishalishuhudia na sisi kama Serikali tumeshatoa maelekezo kwa ATCL kwamba kuanzia sasa hivi ndege yoyote ambayo itakuwa na delay zaidi ya nusu saa tunahitaji tupate maelezo ya maandishi yakiambatana na vielelezo. Kama ni hali ya hewa basi tupate na taarifa ya hali ya hewa ambayo imeambatanishwa ku-justify maelezo ya delay ya safari husika. Hilo tumekwishaongea na watu wa ATCL na wanafanya kila linalowezekana kuhakikisha kwamba safari zote za ndege haziwi na changamoto mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, niongelee kwa harakaharaka masuala ya mawasiliano, kuna suala la usajili wa laini za simu. Ni kweli kuanzia tarehe 1 Mei, Serikali kupitia TCRA imeamua Watanzania wasajili laini zao za simu kupitia alama za vidole zikiambatana na kitambulisho cha NIDA.

Mheshimiwa Spika, kwanza nifafanue ni laini moja kwa kila mtandao. Kama una mitandao ya Tigo, Voda, Halotel, Airtel na TTCL unaruhusiwa kuwa na laini moja moja. Endapo utahitaji laini ya pili eleza tutakusajili.

Mheshimiwa Spika, nia ya kufanya hivyo ni kuhakikisha kwamba kwa kiasi kikubwa tunayadhibiti matumizi mabaya ya mtandao. Ukisajili laini zako tatu za Voda tukajua kabisa ni wewe umesajili maana yake ikitumika vibaya basi tutakuchukua halafu tutakupeleka kwa upole kabisa ili uweze kwenda kuwasaidia Polisi kutoa maelezo ya hicho kilichokufanya utumie mtandao vibaya, hatuna lengo baya.

Mheshimiwa Spika, suala la vitambulisho tumeamua kuchagua kitambulisho cha NIDA kwa sababu moja tu kwamba ni kitambulisho ambacho kinavuka mipaka yote Tanzania Bara na Tanzania Visiwani. Kitambulisho cha Mkazi wa Zanzibar tunakikubali, ni halali na kizuri na hakina tatizo lakini tunachokiona ni kwamba kile kinatumika kwa Mzanzibar, kikija huku Bara hakitumiki, kwa hiyo, hakiwezi kutumika kwa Bara lakini mitandao ya simu kama Halotel, Tigo na kadhalika inatumika Bara na Visiwani. Tukichukua kitambulisho cha kule peke yake hakitatusaidia kudhibiti uhalifu.

Mheshimiwa Spika, pia leseni za magari siyo kila Mtanzania aliyetimiza miaka 18 ni lazima awe na leseni ya gari. Kuna wengine hawana leseni ya gari, wale ambao hawana leseni ya gari wanahitaji kuwa na mawasiliano ya simu. Kwa hiyo, tumeona kwamba kitambulisho cha NIDA kitawasaidia kwa sababu kile ni kitambulisho ambacho kinamhusu Mtanzania yeyote aliyetimiza miaka 18.

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa hivi nipende kutoa taarifa kwamba kwa Zanzibar taarifa za NIDA zinasema zaidi ya asilimia 90 wameshapewa namba ya usajili wa vitambulisho vya NIDA. Masuala ya kupata kitambulisho yanaendelea taratibu lakini namba za usajili wamekwishapata. Kwa hiyo, tuna uhakika kwamba wataweza kusajili bila tatizo lolote.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Tanzania Bara tuko kwenye Watanzania milioni 16. Kwa hiyo, ukichanganya tuko mahali pazuri na bado tunaamini kwamba kwa miezi nane tuliyoitoa, Watanzania wengi watakuwa wameshasajili na wataweza kutumia huduma vizuri kwa usalama wao lakini kwa uchumi vilevile kuona kwamba zile message za tafadhali nitumie pesa kwa namba hii zinadhibitiwa kwa kiwango kikubwa.

Mheshimiwa Spika, Kuna Mheshimiwa Mbunge alizungumza kuhusu masuala ya picha za ajabu ajabu. Ni ngumu sana kama Serikali kumdhibiti mtu yuko chumbani kwake akaamua kujipiga hizo picha akaangalia mwenyewe. Huwezi kumzuia mtu kama huyo apige picha aangalie chumbani kwake afurahi kama inaweza ikamsaidia lakini anapoitoa nje ya chumba chake ikaanza kusambaa tutamkamata yule wa mwisho mpaka yule wa kwanza aliyejipiga zile picha akazituma kule. Nia na madhumuni ni kwamba mitandao ya mawasiliano itumike kwa faida kwa Watanzania wote bila kuathiri mtu mwingine yeyote ambaye hataki taarifa ambazo wewe unazo. Tumejipanga kuhakikisha kwamba tunadhibiti uhalifu wa kimtandao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa kuna suala la UCSAF na minara ya mawasiliano. Niliwahi kuzungumza kwamba tunafahamu changamoto ya minara ya mawasiliano kwa Waheshimiwa Wabunge na tumeendelea kufanya kazi kwa bidii sana kuhakikisha kwamba eneo kubwa sana la nchi yetu linapata mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa hivi asilimia 94 ya Watanzania wanawasiliana. Tunachokiangalia ni kwamba kuna mawasiliano eneo fulani. Changamoto ndogo sana tunayoipata sasa hivi ni kwamba kama kuna mawasiliano ya Halotel kuna Watanzania wanataka Voda au Tigo lakini sisi Kiserikali tunasema eneo fulani Kongwa wana mawasiliano kwa sababu wana mtandao wa Halotel labda na TTCL. Wakipata dharura watapiga simu, wakitaka kuuza mazao watapiga simu, wakitaka kufanya miamala kutoka Benki kwenda mitandao hiyo au kutoka mtandao kwa mtandao watafanya miamala. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba kila watu wanawasiliana na kwa hilo asilimia 94 ya Watanzania wanawasiliana na hizi asilimia 6 zilizobakia mpaka inapofika katikati ya mwaka ujao tunakwenda kutangaza mwezi huu vijiji 689 tutakavyovipelekea minara ya mawasiliano ili kuhakikisha kwamba Watanzania wanaendelea kuwasiliana.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuzungumza hayo, naunga mkono hoja asilimia 100, ahsante sana. (Makofi)