Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuniwezesha kusimama hapa katika Bunge hili Tukufu na kuchangia hoja ya Wizara ya Viwanda na Biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masikitiko makubwa sana nieleze kuhusu bajeti katika Wizara hii, kwa miaka mitatu mfululizo sasa bajeti ya Wizara ya Viwanda imeendelea kushuka siku hadi siku. Mwaka 2016/2017 bajeti ilikuwa ni asilimia 42.37; mwaka 2017/2018 ilikuwa asilimia 30.64; mwaka 2018/2019 ilikuwa ni asilimia 24.28, hiyo ni fedha ambayo inapelekwa katika Wizara ya Viwanda na Biashara. Kauli mbiu ya CCM ya Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Dkt. Magufuli ni uchumi wa kati, Tanzania ya viwanda. Tanzania hii ya Viwanda inafikiwaje kwa bajeti ya aina hii? Hivi kweli tuko serious kabisa kwamba tunahitaji uchumi wa kati kwa Watanzania kama hata bajeti ya Wizara inayohusika na masuala ya viwanda na biashara bajeti inakwenda kwa kiwango hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niko kwenye Kamati ya Viwanda na Biashara na siku zote nimekuwa nikijiuliza hivi wenzangu Wabunge wa CCM ambao tuko nao kwenye Kamati, hivi mko serious kweli kabisa kwamba hii kauli mbiu ya Mheshimiwa Rais mnaishikilia kidedea? Maana kila Mbunge wa CCM akisimama hapa ni Stiegler’s Gorge, ni standard gauge ni ndege sijui hiyo haikuwa kauli ya Mheshimiwa Rais wakati anaomba kura. Haya yamejitokeza kila siku wanayasifia haya, hebu watuambie, hii Tanzania ya viwanda iko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu anayeonekana kinara wa Tanzania ya Viwanda ni Mheshimiwa Rais peke yake. Kila anapokwenda atasimamia suala la viwanda lakini hakuna anayemsaidia kwenye suala hili. Amezungumza Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani, hivi kweli Waheshimiwa Mawaziri waliopewa dhamana kwenye hii Wizara wanadhani wanaitendea haki. Hawaoni kwamba wanaenda tofauti na kauli mbiu ya Mheshimiwa Rais na kwenda tofauti na kaulimbiu ya Rais ni kukiuka maneno ya Mheshimiwa Rais. Hebu niwaombe sana tuwe serious kwenye hili, Wizara ya Fedha pamoja na fedha kuwa kidogo lakini hebu waangalie vipaumbele tumezidi kuwa na vipaumbele vingi, inafika mahali hata kile kipaumbele ambacho walikikusudia hakitekelezeki. Halafu tunaimba Tanzania ya Viwanda, Mheshimiwa Rais akienda kuzindua viwanda anafurahi, lakini unashangaa anafurahi leo, kesho TRA wanakwenda pale kila kiwanda kinakwenda kufungwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masikitiko makubwa sana tumeshindwa hata kuvilinda viwanda tulivyonavyo nchini. Leo viwanda vilivyopo nchini vinazalisha kwa ubora wa hali ya juu, lakini utashangaa hata Serikali yenyewe inapotengeneza miradi inakwenda kuagiza nje. Sasa hawa wanaotengeneza humu ndani nani atanunua bidhaa zao. Tunaagiza bidhaa nyingi kutoka nje, tunawapa zero rate, matokeo yake bidhaa zile zinazotoka nje zinakuwa bei ndogo kuliko bidhaa za ndani na humu ndani watu wanawachaji kodi, kuna umeme, kuna wafanyakazi, kuna regulatory authorities chungu nzima ambazo zote hizo wafanyabiashara hawa wanatoa fedha. Wanajikuta wanashindwa kufanya uzalishaji wa kutosha kwa sababu ya gharama za uzalishaji na leo bado sisi kama nchi tunaendelea kuendekeza kuingiza vitu ambavyo hata Tanzania tunazalisha tena kwa kiwango cha hali ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba nitoe wito kwa Serikali kama kweli tunataka Tanzania iendelee kuwa ya viwanda hivi viwanda tulivyonavyo hebu tuvilinde tuwalinde hawa wafanyabiashara wenye viwanda waliopo nchini kwa sasa, wenye moyo ambao bado hawajakimbia. Kama hali ikiendelea namna hii, kama kiwanda kilikuwa kinazalisha kwa asilimia 80, leo kiwanda kinazalisha kwa asilimia 15, kuna tija namna hiyo jamani, halafu tunasema hii ni Serikali ya viwanda, Serikali ya viwanda ipi jamani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamezungumza wenzangu lakini nami naomba nikazie, TRA ni mwiba mchungu sana kwa wafanyabiashara. Wafanyabiashara wamelalamikia sana TRA, sio rafiki tena wa mlipakodi, badala yake amekuwa ni adui mkubwa sana wa mlipakodi, badala ya TRA na mlipakodi kuwa marafiki, kukaa, kuzungumza na kuona ni kwa namna gani ambavyo wanaweza wakalipa kodi, TRA wamekuwa wababe, TRA hawataki kusikiliza, TRA inatukosesha mapato, TRA inasababisha maduka yanafungwa, TRA inasababisha viwanda vinafungwa. Leo nilikuwa namsikia mtu wa TRA anasema biashara zaidi ya milioni moja zimefungwa, huo ndio ukweli, kama kuna watu wamesikiliza clouds asubuhi, zimefungwa ndio!
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tuone sasa, tunachokiangalia tuna- target kitu gani, tunataka kodi, lakini kama tunataka kodi na maduka yanafungwa kodi hizo tunazipata wapi? Tunataka kodi, viwanda vinafungwa kodi hizo tunazipata wapi? Leo viwanda vinapofungwa, ajira pia zinapungua, kwa hiyo tuone ni kwa namna gani tunavyoweza kuweka mfumo mzuri ama kuiangalia TRA kwa jicho la tatu, inawezekana wako watu ambao wana mpango wa kukwamisha hii nchi isiende mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nieleze kwa masikitiko makubwa sana kuhusiana na suala zima la viwanda vilivyobinafsishwa ambavyo vingi havifanyi kazi. Mara zote tumekuwa tukiipigia Serikali kelele mtueleze mna mpango gani na hivi viwanda vilivyobinafsishwa? Ukiuliza kwa watendaji wao wanafuata sheria na utaratibu lakini niwaambie Watanzania mikataba iliyoingia kuwauzia viwanda watu hawa ni mibovu ambayo inasababisha hivi viwanda sisi kama Watanzania tutashindwa tena kuvifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikumbuke kauli ya Mheshimiwa Rais amesema hawa watu ni wahujumu uchumi. Leo mtu amenunua kiwanda kazi anayofanya anapanda maua. Tumekwenda kwenye kiwanda kimoja Arusha, kiwanda kinazalisha vizuri sana, kinalipa kodi vizuri sana lakini eneo walilonalo ni dogo. Kwa muda mrefu sasa wanaiomba Serikali eneo la nyuma ya kiwanda chao ambapo kuna kiwanda kingine kinatumika kupanda maua ili waweze kuongeza uzalishaji kwenye kiwanda chao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili limeshindikana na tunamuuliza Waziri tatizo ni nini na wao nafikiri bado hawajajua tatizo kwa sababu Naibu Waziri hakuwa na majibu ya kutuambia. Hata tulipokuja kwenye kikao tunamuuliza Naibu Waziri wamefikia wapi kuhusiana na suala hilo hakuwa na majibu ya kutuambia. Leo katika Bunge hili tunaomba mtuambie Serikali mna mpango gani wa kuwapa TBL eneo hilo wanaloomba ili waongeze uzalishaji ili muendelee kupata kodi badala ya ilivyo hivi sasa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tangu suala la viwanda lipelekwe kwa TR, hili Waziri wa Fedha atuambie ni lini Waziri wa Fedha mtatusaidia kuturejeshea viwanda vyetu kwa sababu viwanda vyote viko chini ya TR? Kama viko chini ya TR, Wizara ya Viwanda haina mamlaka na viwanda hivi, kwa hiyo, kila tunavyowauliza majibu yao ni kwamba wao hawana mamlaka ya viwanda hivi. Ningeomba wakati wana windup Wizara ya Fedha ituambie viwanda vilivyobinafsishwa lini vitarudishwa Serikalini ili watu wanaovihitaji waweze kuvifanyia kazi?
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Hawa Mwaifunga.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)