Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

Hon. Hassan Elias Masala

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nachingwea

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji wa kwanza wa hotuba ya Wizara hii ya Viwanda na Biashara. Ya kwangu nilikuwa naomba nichangie katika maeneo makubwa manne.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la kwanza ambalo nilitaka nichangie ni eneo linalohusu Mamlaka ya Biashara - TANTRADE. Hawa ukisoma kwa mujibu wa kazi zao ambazo wanazifanya, kazi kubwa mbili za msingi kazi ya kwanza ni kufanya utafiti wa masoko, lakini pia mamlaka hii imepewa kufanya kazi ya intelijensia ya kujua kwa wakati tuliokuwa nao dunia inataka nini katika eneo la bidhaa. Sambamba na hili bado mamlaka hii imekuwa inafanya kazi kwa ajili ya kutangaza bidhaa zetu kupitia maonesho ambayo yamekuwa yanafanyika pale Sabasaba.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi hizi zote zinaenda vizuri, lakini bado naomba nijielekeze zaidi katika hizi kazi kubwa mbili. Kwa muda mrefu tumekuwa na wakulima lakini sehemu kubwa Watanzania tumekuwa tunajishughulisha na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali ikiwezo hizi bidhaa za mazao. Sasa yako maeneo ambayo kidogo nashangaa kuona namna ambavyo mamlaka hii inavyofanya kazi na namna ambavyo wakati mwingine ilivyoshndwa kusaidia nchi yetu katika kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitolee mifano katika maeneo makubwa mawili, mimi nina wakulima ambao wanalima zao la mbaazi. Zao hili kwa muda mrefu limelegelega kupata bei na kwa miaka ya karibuni mitatu iliyopita tumeshindwa kabisa kuuza mbaazi zetu, sasa kama mamlaka hii ingekuwa inafanya kazi yake ipasavyo na kama ingekuwa imetekeleza wajibu wake wa kufanya utafiti au uchunguzi juu ya masoko ya zao hili na namna ya kuishauri Serikali nafikiri wakulima wetu leo hii wasingekuwa wanapata changamoto ya wapi wataenda kuuza bidhaa zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo wakulima wetu wako njia panda wanashindwa kujua kama waendelee kuzalisha mbaazi au wabaki kama ambavyo walikuwa wanafanya zamani kutumia mbaazi kama mboga. Sasa naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa hebu atueleze mamlaka hii inatekelezwa ipasavyo na kama inatekelezwa kwa nini kwa miaka minne mfululizo tumeshindwa kupata jibu la uhakika juu ya hatma ya zao hili ambalo kwa baadhi ya wakulima wetu wamekuwa wanashiriki kulifanya na hatimaye tumeingia hasara ambayo kimsingi bado tumeshindwa kuwasaidia wakulima wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili, mwaka jana kwa maana ya msimu wa korosho nafikiri wewe mwenyewe utakuwa ni shahidi, Mawaziri wetu wamekuwa wanagongana juu ya bei ya korosho. Kama mamlaka hii ingefanya intelijensia yake ya kuchunguza bei katika soko la dunia, lakini pia kuchunguza uhitaji katika mahitaji ya kidunia, naamini kusingekuwa na mgongano wa bei ambao umesababisha leo hii wakulima wetu wengi washindwe kupata bei ambayo ilikuwa inatazamiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba kwa heshima na taadhima basi Mheshimiwa Waziri wa Biashara kaka yangu Mheshimiwa Kakunda aweze kutueleza, hawa watu wa TANTRADE ukiondoa kufanya maonesho ya biashara ambayo sasa hivi kwa sehemu kubwa ni kama wanachukua tu wachuuzi hata wauzaji wa mitumba wako pale uwanja wa Sabasaba wanafanya shuguli zao na mambo mengi ambayo yanakwenda pale kufanyika ya kutangaza dawa na vitu vyepesi vyepesi tu, ambavyo kimsingi mimi nilikuwa naona jukumu hili la msingi kama wangezingatia, kama wangewezeshwa basi naamini leo hii sisi tungekuwa tunajua tuzalishe tani ngapi za mbaazi na zitakwenda wapi kwa sababu tayari watakuwa wameshatupa bei na uelekeo wa mazao haya tutayapeleka wapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimwombe sana kaka yangu Mheshimiwa Kakunda atakapokuja kuhitimimisha basi atueleze na kama hawajajipanga katika uelekeo huo, basi hebu tuwasaidie na akiwasaidia hawa kuwaweka vizuri maana yake watawasaidia hata watu wa Wizara ya Kilimo ku-forecast bei, lakini pia kupanga mipango mizuri ambayo haitaenda kuwaumiza wakulima wetu kama ambavyo sasa hivi inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ambalo naomba nichangie, ni eneo lingine linalohusu watu wa SIDO. Nilikuwa najaribu kupitia hapa katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri, kuna huu Mfuko wa Maendeleo ambao unakopesha wakulima wa NEDF. Naomba nimpongeze sana na nilikuwa nafuatilia hapa takwimu za mikopo midogo midogo ambayo imekwenda kwa wajasiriamali. Hata hivyo, concern yangu kubwa ambayo nataka tuweze kushauriana vizuri ni tuone namna gani mfuko huu wa SIDO unavyochangia na unavyosambaa kuwafikia wale wanyonge walioko maeneo ya mbali kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa napitia takwimu nyuma za hiki kitabu nione katika Mkoa wa Lindi mathalani, Wilaya ya Nachingwea, ni wajasiriamali wangapi wadogo wadogo ambao wamenufaika na Mfuko huu wa SIDO, lakini ni kiasi gani cha fedha ambacho ndani ya miaka hii miwili, mitatu kimeenda kwa wakulima. Niwapongeze kwa sababu fedha nyingi zimekwenda, lakini uwiano wa namna ambavyo tumewafikia wajasiriamali wadogo wadogo kidogo unanitia mashaka. Sasa naomba kipaumbele chetu kijielekeze kwa kadri ya uzalishaji tunaoufanya na namna ya kuwezesha wajasiriamali wadogo kwa shughuli za uzalishaji wanazozifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunao mamalishe lakini pia tunao watu wadogo ambao wanafanya kazi ya ubanguaji wa korosho kule kwetu. Haya makundi yote kama tungeweka utaratibu mzuri wa kugawa hizi fedha naamini tungeweza kuwafikia wanyonge wengi sana walioko kule chini badala ya kukopesha tu katika maeneo makubwa au maeneo ya mijini ambako hawa ndiyo wamekuwa wanajua fursa na wamejua kuzichangamkia na kuacha wakulima wetu wadogo wadogo amabo wako katika maeneo yale ya mikoani na wilayani kule chini. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri naomba sana watakapokuja kuhitimisha watuwekee utaratibu mzuri ambao utapelekea hata wale wakulima na wajasiriamali wadogo wadogo walioko chini wapate kunufaika na Mfuko huu wa Maendeleo kwa ajili ya kukopesheka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la tatu ambalo nataka nichangie ni eneo la mradi wa matrekta ya URSUS. Naomba nipongeze mradi huu wa matrekta ya URSUS ambao uko pale Kibaha. Mheshimiwa Waziri pamoja na Wizara yake tunatambua jitihada kubwa ambazo wamekuwa wanazifanya, lakini bado naomba tuone namna ambavyo mradi huu unavyoweza kuwafikia pia walengwa ambao ni wakulima walioko katika maeneo ya pembezoni. Kibaha ni center, mkulima anayetoka Mtwara, Ruvuma, Lindi ni nadra sana kufahamu fursa inayoweza kupatikana kupitia mradi huu wa matrekta. Matrekta haya ni bora na tulitamani sana yangewafikia wakulima wetu ili waweze kuzalisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii ukienda kwenye baadhi ya maeneo trekta ni ya kugombaniana. Wakulima hawana access ya kupata vyombo hivi kwa ajili ya kulima kilimo cha kisasa. Sasa naomba Mheshimiwa Waziri ikimpendeza hebu tuone utaratibu wa kufungua center katika baadhi ya maeneo. Kwa mfano tunaweza tukaweka center ya Kusini ambayo itajumuisha mikoa mitatu ya Lindi, Mtwara, Ruvuma kule at least wakaweka sample ya matrekta na utaratibu wa namna ambavyo wakulima wetu wanavyoweza kukopa au kuweza kuyapata haya matrekta kwa gharama nafuu zaidi, tofauti na ilivyo sasa hivi mtu wa kutoka kule mbali aweze kuyafuata haya matrekta Kibaha au maeneo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi mradi mkubwa ambao tunategemea kukopa matrekta ni wa SUMA JKT ambao bado haufanyi vizuri sana. Hata hivyo, kupitia mradi huu naamini Serikali kama mtaweka mazingira mazuri, basi wakulima wetu wengi watapata access ya kufikia na kuweza kuchukua matrekta ambayo yatawasaidia katika uzalishaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la mwisho ambalo nilitaka….

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, kengele ilishagonga.

MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)