Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

Hon. Kiswaga Boniventura Destery

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Magu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia hoja iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba niipongeze Serikali kwa namna ambavyo inaendelea na jitihada zake za kuhakikisha kwamba wawekezaji kwenye nchi hii wanapatikana. Japo zipo kasoro ndogondogo ambazo tunapaswa sisi Wabunge tushauri na tusikilizwe na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunamwona Mheshimiwa Rais anapokuwa na mahangaiko makubwa sana moyoni mwake, kadri ambavyo anachukizwa na mwenendo ambao unazuia uwekezaji wa haraka kwenye nchi hii kwenye viwanda vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa na viwanda vingi ambavyo tulivibinafsisha, ningeshauri Serikali iweze kuvipitia upya tuone kama vinafanya vizuri kazi iliyokusudiwa. Kwa sababu inaonekana kuna viwanda vingi havifanyi vizuri na viwanda hivi kama vikifanya vizuri tutaondoa kabisa tatizo kubwa la ajira lililoko nchini mwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda ambavyo vilikuwa vikileta uchumi kwa nchi hii, bado havijatazamwa vizuri. Tulikuwa na Kiwanda cha Zana za Kilimo kule Mbeya, tulikuwa na viwanda vya nguo mpaka leo havifanyi vizuri, tulikuwa na viwanda vya kapeti, vimeshakufa, tulikuwa na viwanda vya kutengeneza vifaa vya umeme nchini, vimeshakufa. Namshauri sana Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara, aweze kuvipitia upya viwanda hivi ili tuweze kuona kama vinaweza kuendelea kuzalisha kama vilivyokuwa vinazalisha zamani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapowekeza kwenye viwanda, tunaongeza ajira kubwa, tukiongeza ajira, watumishi wale wanalipa kodi, kwa maana ya PAYE, SDL pamoja na WCF. Kwa hiyo, huo ni mkusanyiko mkubwa ambao unaweza kuchochoe uchumi kwenye nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ziko kasoro nyingi ambazo wawekezaji wanazipata kupitia taasisi zetu nyingi ambazo wengine jana walichangia, ziko taasisi kwenye viwanda na uwekezaji wa jumla karibu 27 na kuendelea. Tungeshauri, taasisi hizi za Serikali ziunganishwe ziwe mlango mmoja, zipunguze bureaucracy ili wawekezaji waweze kuwekeza kwa haraka zaidi. Bila hivyo, tutakuwa tunaimba wimbo uleule bila mabadiliko kwenye nchi hii. Niishauri sana Serikali isikilize ushauri wa Wabunge wakati wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende pia kwenye service levy. Wakati sheria hii ya service levy inatungwa ilikuwa imejielekeza kwenye viwanda, wala haikujielekeza kwenye maduka ya jumla ya rejareja lakini leo biashara hizi zinakufa kwa sababu ya kutoangalia upana wa sheria hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wanatunga sheria hii, kwa mfano, Breweries, ikiwa pale Mwanza Ilemela, distributer wa Shinyanga, Geita, Singida na Tabora, akiuza bia yake watu wa Tabora, Singida, Shinyanga wana-claim madai yake Breweries Ilemela. Leo distributer wa Ilemela na Shinyanga, ukichukua bia pale kwa distributer wa Ilemela, ukapeleka Misungwi, unadaiwa service levy, hata yule mwenye bar ya kawaida naye anadaiwa service levy. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, mwenye biashara kwa mfano mfuko wa sukari, gharama yake ni shilingi 108,000, faida yake ni Sh.500, akitozwa service levy ni shilingi 324. Kwa hiyo, anabakiza kama shilingi 170. Service levy inatozwa kwa mauzo, mfanyabishara hawezi ku-declare kodi yote kwa sababu inachukua gharama kubwa kuliko ingetozwa kwa faida. Kwa nini tusibadilishe sharia ya service levy tukatoza kwa faida, tukiwa tumeondoa gharama za uendeshaji kama ambavyo tunatozo corporate tax. Tukifanya hivyo, tutawaondolea adha wafanyabiashara hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba ukae na wafanyabiashara, kama ambavyo Waziri Mkuu alikaa na wafanyabiashara kule Kariakoo, alibaini mambo mengi. Niombe pia Mawaziri mnaohusika, Rais alipokaa na wafanyabiashara na wachimbaji wa madini akaleta mapendekezo ya sheria hapa, leo tunaona ambavyo madini yetu yanalipa zaidi ya kile kilichokuwa kinalipwa, wakwepaji kodi wanaondoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapokaa na wafanyabiashara, wana manung’uniko mengi ambayo kwa kweli tukiwasikiliza na kuleta hapa marekebisho ya sheria, tunaweza kusaidia biashara nchini. La sivyo, hatutakuwa tumesaidia biashara nchini, tukiendelea kuwa na kodi nyingi ambazo hazina faida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama inashindikana service levy kutozwa kwa faida, basi ipungue iwe 0.1% badala ya 0.3%. Kwa sababu hata benki wamepewa waraka na Katibu Mkuu, Wizara ya TAMISEMI, wawe wanachajiwa 0.1%, kwa nini wafanyabishara wengine nao wasipate huo mwanya wa kuweza kutozwa kwa asilimia hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, OSHA ina msaada gani kwa biashara? Tulikuwa tunajua OSHA inasimamia usalama wa watumishi kazini lakini leo wamekuwa watozaji wa kodi, watu wenye viwanda, petrol station na hoteli, wanalalamika, kwa sababu badala ya tozo zile zingine za kawaida (WCF) ambapo ni mchango ambao unasaidia wakati mtumishi anapata tatizo, labda la ajali kama fidia wanatoza kwa mwaka, kati ya milioni moja mpaka milioni tano, wafanyabiashara hawa wanalalamika sana. Tuangalie tozo ambazo haziwezi kusaidia kwenda mbele…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbunge, muda wako umekwisha, ahsante sana.

MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.