Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Tunduma
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia katika hotuba hii. Tunapozungumzia biashara tunazungumzia uwekezaji wa ndani na wa nje, hivyo, kama ambavyo Serikali inasema kuwa inahitaji nchi hii iwe nchi ya viwanda, lazima ifahamu kuwa viwanda ni biashara na kama mazingira ya kufanyia biashara siyo rafiki, basi hata viwanda havitaweza kuwepo. Ni vizuri Serikali ikaelewa kuwa kama wafanyabiashara wa kawaida wanashindwa kufanya biashara basi tusitegemee wafanyabiashara kutoka nje kuja kuwekeza katika nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ifahamike kuwa biashara ni mawasiliano, kila kinachofanyika hapa kwetu kinajulikana karibu dunia nzima, hivyo, kama tumeshindwa kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji wa ndani tusitegemee kupata wawekezaji toka nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaposema kuwa biashara zinafungwa lazima Serikali itafute namna ya kuondoa tatizo na siyo kuendelea kukomaa bila kuondoa changamoto zilizosababisha biashara kufungwa kila mahali hapa nchini na kama tukiendelea hivyo basi tutegemee kukosa kukusanya kodi kama tunavyokuwa tunategemea siku zijazo. Hata hivyo, kibaya zaidi wafanyabiashara wengi wametimkia katika nchi jirani na kusajili biashara zao huko.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni Taifa gani ambalo linaweza kuendelea na kufikia uchumi wa kati kama wananchi wake hawana uwezo wa kulipa kodi na kodi zinalipwa kutoka kwenye faida? Pia kodi zinalipwa kulingana na ukubwa wa biashara, sasa kila wakati tunaishauri Serikali kuwa irekebishe baadhi ya sheria za kodi na tozo mbalimbali ili kufanya urahisi wa kufanya biashara ili mitaji ya watu ikue na kutoa nafasi kwa wafanyabiashara kuchangia pato la Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali hii haioneshi dhamira ya kuwa nchi ya viwanda, kama tunaweza kuidhinisha pesa ya maendeleo, shilingi bilioni 100 lakini pesa iliyotoka mpaka sasa ni bilioni 12 halafu unasema tuko tayari kuwa nchi ya viwanda, huo utakuwa uongo mchana kweupe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Taarifa ya Benki ya Dunia kuhusu urahisi wa kufanya biashara duniani, Tanzania sasa ni ya 137 kati ya nchi 190 duniani na changamoto zilizotajwa ni pamoja na kodi ambazo siyo rafiki kufanya biashara na ugumu wa kuanzisha biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali hii tangu imeingia madarakani imekuwa haiwaamini tena wafanyabiashara, imewapa majina mengi sana kama wizi, mara wapiga dili, yote hayo yanaonesha kuwa Serikali haitambui kuwa wafanyabiashara ni wadau muhimu kabisa katika Taifa hili na kama mpaka leo Watanzania wamewapa madaraka haya haitambui hilo, basi Taifa hili ni haki linavyoangamia kwa wafanyabiashara kuitwa majina haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, yapo matukio ambayo yametokea hivi karibuni kwa wafanyabiashara wa maduka ya kubadilishia pesa za kigeni kufungwa na pia kuondoka na pesa pamoja na vitendeakazi, Watanzania wanataka kujua je, ni kwa nini Serikali ilifunga maduka hayo na kuchukua pesa zilizokuwa katika maduka hayo na je hiyo ndiyo elimu kwa walipakodi hao?
Mheshimiwa Naibu Spika, tulitegemea taarifa kutoka Serikalini sababu ya kufunga maduka hayo ambayo yameanzishwa kwa mujibu wa sheria ya nchi na kama kulikuwa na tatizo Serikali inawasaidiaje hawa wafanyabiashara? Pia taarifa ilitoka kuwa Serikali kwa sasa imeelekeza wapi huduma ya kubadilishia pesa itatolewa? Je, katika nchi hii hakuna tena mtu kufungua duka la kubadilishana pesa za kigeni? Kama ndivyo katazo hilo liko kwa mujibu wa sheria ipi?
Mheshimiwa Naibu Spika, hayo yote ni mambo yanayoiweka nchi yetu katika mtazamo mbaya wa kuonesha jinsi Tanzania isivyokuwa nchi salama katika kufanya biashara. Pia kama kuna pesa zilizochukuliwa kutoka katika maduka hayo ya kubadilishana pesa ni shilingi ngapi? Je, ni wafanyabiashara wangapi wanafikishwa mahakamani na kwa kosa gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, tunashuhudia pia wafanyabiashara mbalimbali wakisota mahabusu kwa muda sasa, je, Serikali inajua kuwaweka ndani wafanyabiashara bila taarifa yoyote kwa umma ni kuendelea kuongeza hofu kwa wafanyabiashara mfano Yusuph Manji, Lugemalira na wengine wengi bila taarifa rasmi za wazi kwa umma ili umma ujifunze na kujua kinachoendelea juu ya wafanyabiashara hao? Je, Serikali inaweza kutufahamisha ni wafanyabiashara wangapi wako rumande kwa kosa la kutakatisha fedha? Je, Serikali imepata faida gani katika kuwakweka rumande wafanyabiashara hao?
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hali isiyo ya kawaida bado Serikali haikubali kuwa sasa Tanzania siyo sehemu salama kwa kufanya biashara, ukienda Kariakoo sasa utaona vyumba vimefungwa na vimebandikwa matangazo chumba kinapangishwa. Jambo hilo hapo awali halikuwepo kabisa na ni kwa sababu wafanyabiashara wameshindwa kufanya biashara. Kuna kikosi kimeanzishwa kinaitwa task force, hiki kinakaa nje ya maduka na kukamata mtu anayetoka kununua mzigo katika maduka na kuuliza risiti, baadaye huwanyang’anya mizigo na kuutaifisha na kumtoza mwenye duka faini ya milioni tatu au zaidi na muda mwingine hupokea rushwa ya kati ya milioni moja au milioni moja na nusu na kumalizana na mfanyabiashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo faini ya milioni tatu imeongeza rushwa kwa hiyo task force, lakini pia imepelekea wageni kunyang’anywa mizigo na sasa stoo za TRA Dar es Salaam zimejaa mizigo ya wafanyabiashara hao wageni na baada ya muda TRA huipiga mnada mizigo hiyo. Kitendo hiki kimesababisha wafanyabiashara kutoka Congo, Zambia na kadhalika kuacha kuja Dar es Salaam kununua.