Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza natoa shukrani na sifa kwa Mwenyenzi Mungu kwa kupata nafasi hii kuweza kuchangia kwa maandishi katika Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa hongera na pongezi zangu kwa Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Morogoro miaka ya nyuma ulikuwa mkoa wa viwanda. Hivi ninavyochangia sasa hivi, viwanda vingi vya zamani vilivyokuwa vinafanya kazi, vimekufa, havifanyi kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha hoja yake, wananchi wote hususan wa Mkoa wa Morogoro atueleze hatima ya viwanda hivi ambavyo vimekufa na havifanyi kazi tena kama Kiwanda cha Ngozi, Ceramics na Magunia.
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa pongezi kwa Serikali kwa kuanza ujenzi wa viwanda nchini Tanzania. Pongezi nyingi kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa mkakati mkubwa wa ujenzi wa viwanda. Tanzania ya viwanda inawezekana. Viwanda vingi na hasa vidogo na vya kati vimeanza kujengwa katika mikoa yetu yote ya Tanzania. Naamini hata tatizo la soko la mikunde ikiwepo mbaazi, litapatikana hivi karibuni.
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa pongezi hizi kwa Serikali, kwani kiwanda cha mikunde/mbazi kimepewa kipaumbele, kimejengwa kiwanda cha kununua na kuchakata mikunde. Kiwanda hiki kimejengwa na wawekezaji kutoka India. Kimejengwa Kata ya Mtego wa Simba, Wilayani Morogoro Vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusu Mradi wa Mchuchuma na chuma cha Liganga. Mradi huu una manufaa sana kwa nchi yetu. Umechukua muda mrefu. Ni miaka wingi sana tangu mradi huu umeanza, mpaka sasa hivi Mheshimiwa Waziri katika hotuba yake anasema, mchakato wa kupitia upya mkataba kati ya NDC na Sichuan Hongda Group unaendelea. Sasa ni muda muafaka mradi huu ufike mwisho, kusudi uweze kuianufaisha nchi yetu, waanze kufanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, fursa za masoko kwa wajasiliamali wadogo na wa kati, akina mama/wanawake wengi wamejikita sana katika biashara ya usindikaji, nguo na kazi za mikono.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo wanalokumbana nalo ni upatikanaji wa soko/masoko ya uhakika. Mheshimiwa Waziri mkakati wa kuwatafutia masoko kwa uwazi na uhakika ni muhimu ili kuinua uchumi wa familia zao na nchi yetu kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri jambo hili uliangalie sana ili kuwasidia wananchi wanaojishughulisha wakiwa na nia moja ya kuinua uchumi wa familia zao na uchumi wa nchi yetu kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja.