Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Tanga Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuwepo Bungeni leo na kuchangia Bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuiomba Serikali yetu sikivu kutoa msamaha (exemption) au kuruhusu taasisi ambazo wameagiza tende kama chakula kwa kutoa msaada kwa watu masikini wenye mahitaji. Naamini ombi langu litakubaliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie biashara katika Tanzania. Wafanyabiashara nchini Tanzania ni sawa na wale wanaofanya biashara katika nchi nyingine; na kazi ya biashara ni kununua na kuuza, pamoja na kulipa kodi katika idara husika, mfano TRA. Wafanyabiashara wa Tanzania wamekuwa kila mara wakilalamikia mifumo ya kodi ambayo siyo rafiki kwa wafanyabiashara wenyewe na biashara zao. Tanzania kuna utitiri wa kodi. Utitiri huu wa kodi unasababisha wafanyabiashara kujiona wanaifanyia kazi Serikali kwa kuwa katika mapato. sehemu kubwa ya mapato inabidi kulipia kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe wafanyabiashara kote duniani wanafanya biashara ili wapate faida baada ya kulipia gharama za uendeshaji kama mishahara ya wafanya kazi, gharama za umeme na maji, kodi na tozo mbalimbali (Serikali Kuu na Halmashauri), michango mbalimbali katika taasisi, fremu ya biashara ilipo biashara yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mfanyabiashara kuona hana anachopata katika biashara, anachobaki nacho anaona bora afunge biashara kwa kuandika barua ya kufunga biashara kwenda TRA ili wasiendelee kutozwa kodi.kufuatia jambo hili, mapato ya Serikali yanapungua na hatimaye wafanyabiashara wanahamia nchi jirani ambapo wanaona kuna masharti nafuu ya kufanya biashara. Mfano wafanyabiashara ya nguo, wanaona ni nafuu kufanya biashara nchini Uganda, wanaanzisha maduka ya jumla na rejareja kisha wafanyabiashara wadogo wanakwenda kufuata nguo Uganda.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni bidhaa kutoka Zanzibar kuja Tanzania Bara. Pamekuwepo na sintofahamu ya hali ya juu kwa bidhaa kutoka Zanzibar kwa kulipiwa kodi mara mbili. Kwa mfano, ukinunua sukari Kiwanda cha Mahonda ukija nayo Tanzania Bara unatakiwa uilipie tena kodi. Swali; je, nikinunua sukari Mtibwa Sugar, Kilombero, Kagera Sugar au Kilimanjaro TPC, kwa nini hailipiwi ushuru? Au tatizo ni kuvuka bahari?
Mheshimiwa Naibu Spika, bidhaa zinazotoka Zanzibar zinasaidia kupunguza ukali wa mfumuko wa bei na pia bei rahisi na hupunguza baadhi ya kero ya upungufu kwa baadhi ya bidhaa. Hivyo, bidhaa za Zanzibar ziwe huru. Hata sera ya kulinda viwanda vya ndani bado itafanya vizuri na haitaathirika kwa bidhaa toka Zanzibar. Ni ajabu hata redio na TV moja pia inabidi ilipiwe kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanga ulikuwa ni Mji wa viwanda tokea katika zaa za ukoloni, lakini hata katika miaka ya 1970 mwanzoni mwa uhuru hadi miaka ya 1993 ndipo mambo yalipoanza kuharibika, hususan baada ya kuanza kubinafsisha (privatization) mashirika na makampuni ya Serikali. Tanga kulikuwa na viwanda vifuatavyo: Steel Rolling Mill (chuma), Foma Detergent, Amboni Plastic, Sikh Saw Mills, Tanganyika Blanket, Mkumbara Cheapboard, TIP Soap Company, Tanga Dairy, Kiwanda cha Kamba Ngomeni, Tanzania Fertilizer Company, Tanga Nicolln (coconut oil production) na CIC Textiles.
Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda vyote hivi vimekufa, vimeuliwa kwa kuwauzia wafanyabiashara ambao hawana uwezo wa kuviendesha. Tujiulize, viwanda hivi viliajiri Watanzania wengi mno, leo Watanzania (wafanyakazi) wako wapi? Kutofanya kazi kwa viwanda hivi ni dhahiri mzunguko wa fedha, ajira na maisha ya watu wa Tanga yameathirika sana. Nataka kujua, Serikali (Wizara) imejipangaje kufufua viwanda hivi au kuvichukua kwa wawekezaji walioshindwa kuviendeleza viwanda hivi?
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni upatikanaji wa vibali/leseni. Ni rahisi kwa ngamia kupenya kwenye tundu la sindano kuliko kuanzisha viwanda Tanzania, kwa sababu kuna vikwazo na vipingamizi na visingizo vingi unapotaka kuanzisha kiwanda Tanzania. OSHA, TBS, TFDA, NSSF, EWURA, NEMC na SUMATRA, hivi vyote ni vigingi vinavyowaudhi/kusumbua wafanyabiashara wanaotaka kuanzisha viwanda Tanzania. Nashauri, hebu viondolewe na zibaki taasisi mbili tu badala ya utitiri wote huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni biashara ya usafirishaji mabasi. Jana, tarehe 14 Mei, 2019 wasafirishaji wa mabasi na madereva wameandaa mgomo wa kutosafirisha abiria nchi nzima kupitia vyama vyao kuwa kuanzia leo, tarehe 15 Mei, 2019 hawatafanya safari kwa mabasi yao na madereva hawataendesha mabasi. Hii ni kutokana na kero ya Traffic Police kuwatoza faini zaidi ya mara tatu kwa safari moja ya Tanga – DSM, Tanga – Arusha na mikoa mingine nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, wito wangu ni kwamba Serikali itambue kuwa wenzetu hawa (wasafirishaji) wanaisaidia Serikali kuwahudumia Watanzania, hivyo waondoe faini/vikwazo visivyo na ulazima.
Mheshimiwa Naibu Spika, biashara ya boda boda nayo ni miongoni mwa biashara zinazotoa huduma kwa Watanzania katika Sekta ya Usafirishaji. Ni moja ya sehemu ambapo imeweza kuondoa kero maeneo ya mijini na hasa vijijini. Changamoto ya biashara hii nayo inawekewa vikwazo na vikorombwezo vingi kama zilivyo biashara nyingine na kufanya mazingira ya biashara kuwa mabaya. Wamewekewa SUMATRA, TRA (mapato), Halmashauri na traffic sticker. Vyote hivi inabidi bodaboda alipie kodi na tozo. Ukiangalia kwa kina, nayo inaonekana ni usumbufu. Ingetakiwa walipe sehemu moja tu kama SUMATRA au TRA tu na kuondoa ukiritimba uliopo.