Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

Hon. Richard Phillip Mbogo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi. Kwanza nianze kumpongeza Waziri wa hii Wizara, Mheshimiwa Hasunga na Manaibu wako, Omary na Innocent na Watendaji wote katika Wizara hii ya Kilimo kwa kazi ambazo mnazifanya ili kuweza kuwanyanyua Watanzania ambao ndio wengi wako kwenye ajira hiyo kwa asilimia 65 kama ulivyoweza kueleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mchango wangu nianze kujielekeza kwenye zao la tumbaku pamoja na mazao mengine ya biashara. Kama wachangiaji wengine ambavyo wameweza kusema, kwenye tumbaku. uzalishaji unaenda unashushwa na wanunuzi, mpaka sasa imefikia tani 50,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi kushusha huku kunatokana na soko ambalo wenyewe ndiyo wanalijua, lakini linaathiri sana wakulima wetu, ambao wameshaingia katika hiki Kilimo, lakini sambamba na ushushaji wa uzalishaji; hivi karibuni nilikuwa na swali la msingi tarehe 30 Aprili, kuhusiana na tozo kwa hawa wanunuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka juzi 2017 tulifanya mabadiliko ya sheria tulikuwa na Amendment of the Local Government Finance Act, (Cap 290) tuliweza kushusha produce cess kutoka asilimia tano mpaka tatu. Kwa kiwango hicho ambacho tulishusha maana yake ni nini? Tulitoa discount ya asilimia 40; na hii imepelekea kushusha mapato kwenye halmashauri zetu kwa sababu hii ni produce cess iko kwa buyer. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kushuka huko kwa mapato imesababisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye halmashauri zetu umekuwa ni hafifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niiombe Serikali, mlisema kwamba mtafanya utafiti, haihitaji tuangalie utafiti, sisi tumeshafanya. Kwanza discount tu ya asimilia 40 hata kama uzalishaji uko pale pale, tayari mapato yameshuka, kwa hiyo tumeathirika na vitu viwili.

Mheshimimiwa Mwenyekiti, lakini pia, bado makampuni yanayonunua tumbaku katika Mkoa wa Katavi, tukienda Mbeya, Chunya pamoja na Ruvuma Kampuni ya Premium imegoma kulipa tozo hizi kwa sababu wanaidai Serikali kwenye marejesho ya VAT refund (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na tangu mwaka jana tumekuwa tukifatilia, sasa tuombe Serikali ije na tamko ni lini, Kampuni hii italipwa, na uhakiki tunajua kufanyika ni rahisi, ili halmashauri zetu na vyama vya msingi viweze kulipwa, maana haya tuna payables na receivables sasa na wao kwa kweli wamesimamia mahali ambapo wako sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusiana na masoko ya mazao ya wakulima, mazao ya chakula na mazao ya biashara. Mikoa ya Katavi, Rukwa na Songwe, Mbeya mpaka Ruvuma tumekuwa tunazalisha sana mazao na hususan mahindi. Kuna vikwazo vilitokea, hasa kwenye ufungaji wa mipaka; na takwimu hapa wameonesha kwamba tuna ziada, na mkulima ambaye anahangaika ananunua Mbolea, analima hatimaye anahitaji apate bei nzuri ambayo atakuwa na fedha, na aweze kukidhi mahitaji yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iweke wazi mipaka watu waweze kuuza; na kama ilivyoelezwa na Waheshimiwa Wabunge wengine, kwamba kuna sehemu nyingi na hususan kwenye nchi jirani ya Congo DRC. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la uzalishaji wa tija. Serikali ije ituambie, kwa nini tuna uagizaji mkubwa wa malighafi za viwanda kwenye mafuta na ngano? Kwa nini tunaingia ngano asilimia 95 na tano, ndiyo ambayo inanunuliwa hapa Tanzania? Kwa nini iko hivyo na tunavuka kwenda wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la utafiti. TARI iwezeshwe ili waweze kufanya utafiti; kama ni mbegu tuwe na mbegu zilizo bora, na mazao. Kwa mfano mahindi mengine sasa hivi ukishavuna baada ya mwezi mmoja tu yanaanza kubunguliwa. Sasa hebu twende na utafiti wa kutumia hizi taasisi zetu ambazo zipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni kuhusiana na kilimo cha mara mbili katika mwaka, yaani cha umwagiliaji. Tuna miradi, kwa mfano Kata yangu ya Ugala katika Jimbo la Nsimbo, kuna mradi wa umwagiliaji mpaka sasa hauna ufanisi. Serikali mpitie upya tuone nini kifanyike ili wananchi waweze kufaidika.

Vilevile kutokana na mazingira; hivi tukichimba visima na ambavyo tuka-reserve maji haiwezekani kutumia katika umwagiliaji? Kama nchi ya Israel wana ile drop irrigation na sisi tuna maji ya visima hakuna uwezekano ili tuondokane na kugombana na Mheshimiwa January Makamba kuhusu uharibifu wa mito? Tuwe na option nyingine ya pili kwa maeneo machache, likiwa kama ni pilot study. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Suala la Financing. Tanzania Agriculture Development Bank ipanue ku-finance na kukopesha watu. Masuala ya vikundi hayana tija; kuna msuguano watu katika kuungana. Sasa waone namna gani ya ku-finance mtu mmoja mmoja na in a long term na katika interest ambayo itakuwa iko ndogo. Maana tukiwezesha tukawa na commercial farming, maana yake tutazalisha kwa tija na tutakuwa na ziada ambayo tutaweza kuuza katika nchi hata Kenya. Kenya wanachukua mahindi Tanzania, wanauza South Sudan, kwa nini sisi tusiuze moja kwa moja?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tukiongeza uzalishaji katika nchi yetu, tutaweza kuongeza na kunyanyua uchumi. Tunaona GDP kwenye Kilimo ina 90 percent kwa data za 2013 lakini kwenye Pato la Taifa tuna 28.7 percent. Kwa hiyo kilimo kwa ardhi tuliyonayo itaenda kuongeza sana. Pia uje utuambie mradi ule wa Mkulazi – Morogoro umefikia wapi? Isiwe kwa suala la uzalishaji wa mazao yanayotokana sukari, yaani miwa, pia mazao mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa. (Makofi)

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naunga mkono hoja.