Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kwa Mwaka 2019

Hon. Allan Joseph Kiula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kwa Mwaka 2019

MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi niweze kuchangia kwenye kamati hizi mbili ambazo leo ndiyo siku yetu ya kuwasilisha ripoti. Kwanza kabisa niwapongeze wenyeviti wa kamati hizi mbili kwa kazi kubwa waliofanya ya kutuongoza. Jambo la pili nimpongeze CAG kwa kazi kubwa aliyofanya kwa sababu kazi yetu imekuwa nyepesi kwani wao walifanya kazi kwa weledi wakatushirikisha na sisi tukatembea kwenye hoja ambazo waliziandaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo nipitie maeneo machache, eneo la kwanza ambalo nimeona ni muhimu kupitia ni suala la ukusanyaji wa mapato ambalo linafanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Hoja za TRA zimeelezwa katika kitabu ambacho mwenyekiti ameweza kukiwasilisha hapa kwenye ripoti hiyo. Kamati inachosisitiza ni kwamba TRA ni roho ya Serikali, ni roho ya nchi na bila mapato bajeti yetu tunayoipitisha inakuwa ni bajeti ambayo haiwezi kutekelezeka. Kwa hiyo, TRA ni chombo ambacho tunakitegemea sana kiweze kukusanya mapato na mapato hayo yagharamie bajeti ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ndivyo basi hayo mapungufu ambayo tumeyaona ya (outstanding taxes) kodi nyingi kutokukusanywa yanatakiwa kufanyiwa kazi. Hapa linahitajika suala la weledi, suala la uadilifu na suala la kufanya kazi kwa bidii. Kukusanya kodi ni kazi kubwa lakini wakiwa na watumishi wenye weledi kazi hiyo itafanyika na mara zote tumekuwa tukiona suala la mlundikano wa rufaa kwenye Mabaraza ya Rufaa. Kamati ndiyo tumesema kwamba Bunge liazimie kwamba hizo kesi zimalizike na fedha au kodi iliyofungwa huko iweze kukusanywa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo kama ipo kodi ambayo inaonekana haiwezi kukusanyika na ili vitabu vya TRA viweze kukaa sawa, basi hizo kodi zifanyiwe utaratibu wa kuweza kufutwa. Kwa mfano juzi tulipata wasilisho la kusudio la kufuta kodi ambayo inatokana na ile ada ya magari ya kila mwaka. Kwa hiyo, TRA wanayo kazi kubwa ya kuweza kuhakikisha kwamba wanarekebisha mahesabu yao lakini na kodi wanaikusanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo ningependa kulizungumzia ambalo tumelizungumza kwenye kamati yetu ni suala la Wakala wa Majengo (TBA). Hilo jambo ni kubwa sana, katika kupitia mahesabu yao na katika kuzungumza na TBA yenyewe tumeona kwamba wana miradi mingi ambayo haijakamilika na hata katika utendaji wao tunaona miradi mingine sasa wanaanza kunyang’anywa zinapewa taasisi nyingine. Hilo ni jambo ambalo linaashiria alama nyekundu kwa maana ya kwamba iko changamoto inabidi itatuliwe hapa. Pamoja na hayo yote, tunachoshauri pia labda hao TBA sasa wasipewe kazi nyingine mpaka wamalize hizi kazi zilizopo. (Makofi)

Nafikiri hilo litakuwa ni jambo kubwa na ni jambo zuri na ni jambo ambalo linaleta heshima kwa TBA yenyewe, lakini kama wameshika miradi midogo midogo na miradi haimaliziki hiyo haiwezi kuwa na sura nzuri kwa Taifa lakini pia hatuwezi kufuatilia matumizi mazuri ya fedha za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Nyumba (National Housing Corporation) na yenyewe kuna miradi mingi ambayo haijakamilika na miradi hiyo imesimama. Tumetembelea baadhi ya miradi kama ilivyoelezwa kwenye ripoti na tunaona sasa kwamba pesa ya umma au shirika lenyewe linakwenda kupoteza pesa nyingi. Miradi hiyo iliyosimama bado wakandarasi wako kwenye site na wakandarasi hao kwenye site wanalipwa pesa bila kufanya kazi. Sasa hatima ya National Housing ni nini? Hilo ndilo swali la kujiuliza, kwa hiyo tunaomba Serikali iingilie kati iweze kuona namna bora ya kuhakikisha kwamba baadhi ya miradi inakamilika, sio miradi yote ichaguliwe miradi ya kipaumbele ambayo inaweza ikamaliziwa na hizo nyumba zikauzwa au zikapangishwa kutokana na mpango ambao wao wameweka. Sasa hilo ni jambo muhimu sana kwa sababu hizo nyumba zitageuka kuwa magofu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona Serikali imetoa pesa nyingi kukarabati vyuo vya ualimu, tunaipongeza Serikali kwa kutoa pesa lakini pesa hizo nazo zimekwenda kwa utaratibu wetu wa force account. Sasa tunaona liko tatizo kidogo la usimamizi, jambo hilo ni kubwa, wasimamizi wanatakiwa wasimamie ili pesa isiweze kupoteza. Nia ya Serikali ni nzuri, lakini pesa zikienda tija hiyo isipoonekana na yenyewe inakuwa ni changamoto kubwa kwa sababu pesa ya Serikali ambayo ni kodi haiwezi kupotea hivi hivi. Kwa hivyo tunasisitiza kwamba pale ambapo tunaona usimamizi haukufanyika vizuri ambao hawakusimamia vizuri wachukuliwe hatua kwa sababu pia inakatisha tamaa kuona kwamba pesa zinatolewa halafu kazi iliyokusudiwa haifanyiki kikamilifu. Tunawapongeza na Wizara wamejitahidi kufanya kadiri walipoweza isipokuwa kwenye eneo la usimamizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Bandari tumeiona na yenyewe wamejitahidi, kwa nyakati tofauti bandari sasa hivi inafanya kazi kubwa tunaona pesa nyingi zinaingia na walitoa gawio juzi tuliona lakini suala la mifumo inabidi liandaliwe, mifumo iliyopo iweze kukamlishwa ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa na hayo machache ya kuchangia, naunga mkono hoja au wasilisho letu chini ya Mwenyekiti wetu mama Kaboyoka. Ahsante sana. (Makofi)