Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. George Malima Lubeleje

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpwapwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia hoja hii. Kwanza kabisa naipongeza Serikai ya Chama cha Mapinduzi, inafanya kazi nzuri. Katika utawala wa Rais Mheshimiwa Dkt. Magufuli wa miaka minne, lakini kazi na miradi iliyotekelezwa ni mingi sana, kwa hiyo, tunampongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala la miradi. Kwa kweli Serikali inaleta miradi mizuri sana, lakini suala la utekelezaji ndiyo tatizo. Miradi ya maji kama alivyosema Mheshimiwa mwenzangu, tatizo la maji ni kubwa sana vijijini. Sasa Serikali inapopanga kutekeleza miradi ya maji vijijini, basi ile miradi ikamilike. Sasa mradi unachukua miaka mitano mpaka 10. Miradi ya World Bank, hatuna taarifa zake kwa sababu fedha zinatoka nje, lakini miradi ambayo inafadhiliwa na Serikali yetu hapa hapa, kuna miradi kama mitano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Kijiji cha Bumila, Kijii cha Iyoma, Kijiji cha Mima, Kijiji cha Mzanse, miradi imechukua miaka minne, huu wa tano sasa haikamiliki. Ndiyo maana nilimWomba Mheshimiwa Waziri wa Maji aende awaeleze wananchi kwa nini ile miradi haikamiliki? maana mimi nimesema mpaka nimechoka na inaonekana kama mimi sifuatilii hii miradi. Serikali inafanya kazi nzuri sana, lakini naomba jamani mtekeleze hii miradi ili wananchi waweze kupata huduma ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni barabara na madaraja. Kwanza naishukuru sana Serikali, nilipiga kelele sana kuona barabara ya Mpwapwa hadi Kongwa ijengwe kwa kiwango cha lami na Serikali katika bajeti ya mwaka 2019/2020 imenitengea fedha kama shilingi bilioni sita kuanza na kilometa tano. Sasa najiuliza, kutoka Kongwa Junction mpaka Mpwapwa ni kilometa 50, sasa hivi kila mwaka nikipata kilometa tano ina maana kukamilika kwa barabara ya Mpwapwa – Kongwa itachukua miaka 10. Naiomba sana Serikali watenge fedha za kutosha ili barabara hii iweze kufanyiwa matengenezo na ikamilike kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara ya kuanzia Mbande kwenda Kongwa Junction. Barabara hii inatengenezwa kwa kiwango cha lami, lakini matengenzo yake yameanza mwaka 2012 mpaka sasa mwaka 2019, yaani hata kilometa saba hawajafika na hii barabara inakwenda kwa Mheshimiwa Spika. Sasa nauliza, miaka tisa, hii miaka yote wanatengeneza, kuna tatizo gani? Wakandarasi hawalipwi au kuna tatizo gani? Kwa hiyo, naomba sana hawa wakandarasi, Serikali iwalipe haraka ili waweze kukamilisha hii miradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la Umeme Vijijini (REA). Naishukuru sana REA imefanya kazi nzuri sana. Katika Jimbo langu karibu vijiji 62 vimepata umeme. Vijiji ambavyo havijapata umeme ni kama vijiji vitano tu havijapata umeme. Kwa hiyo, nilikuwa naiomba sana Serikali, hivi vijiji ambavyo vimebaki basi Serikali ijitahidi kukamilisha miradi hii ili wananchi waweze kupata huduma ya umeme. Huduma ya umeme ni maendeleo, huduma ya umeme ni uchumi wa nchi yetu. Kwa hiyo, naomba Serikali ikamilishe miradi ya umeme katika vijiji vile ambavyo vimebaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kilimo. Ni kweli taarifa ya Mheshimiwa Waziri inasema kwamba kuna baadhi ya Mikoa imepata chakula lakini kwa kweli Mkoa wetu wa Dodoma haiwezekani mtu akasimama akasema wananchi ni wavivu, hapana! Wananchi wa Mkoa wa Dodoma wanafanya kazi nzuri sana lakini bahati mbaya sana mvua zimekatika mwezi wa pili. Kwa hiyo, mimea yote ilikauka, hakuna kitu hata kidogo walichovuna. Kwa hiyo, Mkoa wa Dodoma una upungufu mkubwa sana wa chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Serikali iuangalie Mkoa wa Dodoma kwa jicho la huruma ili wananchi hawa ambao wameathirika sana na mvua ambayo haikunyesha na wana chakula kidogo sana. Kwa hiyo, Serikali ijiandae kwa ajili ya kusaidia wananchi ambao wana tatizo kubwa sana la njaa mwaka huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi nichangie haya machache. Bada ya kusema haya, naunga mkono hoja hii kwa asilimia 100. (Makofi)