Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Victor Kilasile Mwambalaswa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami nichangie kwenye hoja iliyopo mbele yetu ambayo imewasilishwa na Mheshimiwa Waziri wa Fedha. Nampongeza sana, amewasilisha vizuri sana utekelezaji wa Mpango wa mwaka 2018/2019 na Mapendekezo ya 2021. Hongera sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kwenye uso wa dunia wanadamu tuko zaidi ya bilioni saba; na kadri miaka inavyosogea kwenda mbele, wanadamu tutazidi kuongezeka sana. Wanafalsafa wanasema, vitu ambavyo vitakuwa adimu sana miaka ijayo kwa kuanzia ni viwili; maji na chakula. Kwa hiyo, wanaendelea Wanafalsafa wanasema, mtu anayetaka kuwa tajiri miaka 20 ijayo, aingie kwenye kilimo leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naipongeza sana Serikali kwa kuweka kipaumbele kwenye uchumi wa viwanda. Naipongeza sana. Naomba kwa kuwa Tanzania tuna ardhi kubwa sana na nzuri sana, tuna mito na mabonde, naomba tuupe kipaumbele sana uchumi wa viwanda kwenye kilimo. Tuige mfano wa kile kiwanda cha sukari ambacho kitajengwa hapo Morogoro. Tuige, tuwe na uchumi wa viwanda kupitia kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna vyuo vya kilimo vingi sana. Tuna Chuo Kikuu cha Kilimo SUA ambacho kina wataalam wabobezi wengi sana ambao wanaheshimika Afrika na dunia nzima. Afrika ya Kusini wanawapenda sana wataalam wanaostaafu kutoka hapa SUA. Naomba Serikali iwatumie wataalam hawa. Tuwachukue, tuwafungie ndani, watupe Blueprint ya namna gani tutatumia ardhi yetu hii tuweze kupata mazao ya kilimo na kuweka viwanda vya kuchakata mazao yetu. Naiomba sana Wizara ya Kilimo, Wizara ya Uwekezaji, Wizara ya Viwanda, Wizara ya Fedha tuwatumie sana hawa wataalam wetu wa Chuo Kikuu cha SUA waweze kutupa Blueprint ya namna ya kutumia ardhi na maji yetu tuliyonayo tuweze kujikomboa kwa viwanda kuanzia kwenye kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwenyezi Mungu tena ametupa neema ya bandari. Naipongeza sana Serikali, sasa hivi Serikali inaboresha Bandari ya Dar es Salaam, Mtwara na Tanga. Bandari zetu hizi zinahudumia nchi karibu nane au tisa za Uganda, Rwanda, Burundi, Congo, Zambia, Zimbabwe, Malawi na zinginezo. Kwa hiyo, naomba uboreshaji huu tunaokwenda nao ulenge kushindana na bandari zingine ambazo ziko kwenye ukanda wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, umeona nchi jirani hapa juzi imeona Bandari ya Dar es Salaam inaboreshwa na mizigo mingi inapitia Bandari ya Dar es Salaam wakapunguza ushuru kwenye mafuta ili tuweze kushindana. Kwa hiyo, naomba uboreshaji huu wa bandari uendane na kujipanga sawasawa kwa kushindana na nchi ambazo tuanshindana nazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliona mwaka au miaka miwili iliyopita Bandari ya Dar es Salaam TPA waliweka ofisi yake kwenye nchi jirani ya Congo, jambo zuri sana. Hii inasaidia kufanya marketing ya shughuli zetu. Naomba hii iendelee kwa nchi nyingine zote ambazo tunazihudumia kibandari, tuweke ofisi zetu kule ili tuweze kuwahudumia, tuweze kushindana na wenzetu ambao tunashindana katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona vilevile kwenye mpango, Serikali inaendeleza ujenzi wa reli ya kati (Standard Gauge), inaendeleza kuboresha reli iliyopo ya meter gauge na vilevile ina mpango wa kuanza kujenga Standard Gauge ya kutoka Dar es Salaam kwenda Mtwara na kutoka Tanga kwenda Arusha mpaka Musoma, ni jambo zuri sana hilo. Hii Standard Gauge ya reli ya kati mwisho wa mwaka huu itakamilika kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro na inaanza Morogoro kuja Makutupora na itaendelea huko mpaka Tabora – Mwanza – Kigoma. Wenzetu nchi jirani ya Rwanda imeingia kwenye bandwagon hii, imeamua nayo kutafuta njia za kujenga kutoka Kigali kuja mpaka Isaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali sasa tui- entice Burundi nayo iingie kwenye mpango huu ili na wao wajenge kutoka Msongati kuja mpaka Uvinza halafu wajenge kutoka Msongati – Uvira kwenye nchi ya Congo. Hii reli ya SGR ili ilete faida kubwa kwa nchi yetu inahitaji kusafirisha mizigo zaidi ya tani milioni 20 kwa mwaka. Sasa tusipoitumia nchi ya Congo, itakuwa ni hasara. Kwa hiyo, naomba Serikali tuwa-engage Burundi nao waweze kutafuta fedha wajenge kutoka Msongati mpaka Uvinza na kutoka Msongati kwenda Uvira katika nchi ya Congo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuboresha hii SGR na meter gauge, ipo hii reli ya TAZARA ambayo yenyewe ni cape gauge. Naomba ili tuweze kuitumia vizuri bandari yetu tuiboreshe reli hii ya TAZARA na katika kuiboresha hii inahitaji tu kuiwekea umeme ili treni ziende kwa kasi. Naomba tuiboreshe reli hii na vilevile Serikali iwe na mpango wa kujenga Bandari Kavu pale Inyara ambapo tumekuwa tunaiongelea mara kwa mara. Bandari kavu ikiwepo Inyara unaweza kujenga reli ya mchepuko kutoka pale Inyara ikaenda mpaka Lake Nyasa tukatumia vizuri meli ambazo Serikali imezinunua kusafirisha mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda Malawi na Msumbiji. Kwa hiyo, naomba reli ya TAZARA na yenyewe iwemo katika mpango huu wa kutumia reli zetu na uchumi wetu wa jiografia kuweza kujiletea maendeleo hapa Tanzania na kuwahudumia jirani zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yangu yalikuwa hayo machache, naunga mkono hoja. (Makofi)