Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii ili na mimi niweze kuchangia mpango wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuchangia Mpango huu leo Siku ya Ijumaa nikiwa mtu wa kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kutoa pongezi zangu za dhati kwa Serikali yangu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais, Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa kutekeleza mpango kwa asilimia karibia 80. Wamefanya kazi kubwa sana ambayo Watanzania wote wanaiona. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri, kaka yangu, Mheshimiwa Dkt. Mpango, Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na management nzima ya Wizara ya Fedha kwa kuratibu mpango huu na hatimaye kutekelezeka kwa kiwango kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mafaniko haya yamedhihirika wazi kwa kazi kubwa inayofanywa na Rais wetu pamoja na viongozi wote. Kwanza kabisa kwa kuongeza ukusanyaji wa mapato kwa kiwango kikubwa lakini pili Serikali hii imedhibiti matumizi mabaya ya fedha ambapo ilikuwa inasababisha fedha za Serikali zinazopatikana kutoonekana lakini leo hii Watanzania wote wanaona fedha yao inakwenda wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuweka nidhamu ya watumishi ya Serikali hatimaye kuzilinda hizi fedha na kuzifikisha mahali husika. Miaka iliyopita fedha hizi zilikuwa zinakusanywa lakini kiwango kikubwa zilikuwa zinaliwa na watu wachache lakini katika Serikali hii ya Awamu ya Tano hilo limedhibitiwa, maendeleo tunayaona, kazi inaonekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongee kuhusu miradi mikubwa iliyofanywa na Serikali kwa kutumia mpango huu wa Serikali. Serikali hii imeweza kujenga reli, wenzetu walikuwa wanabeza kwamba haiwezekani, leo Dar es Salaam – Morogoro reli imekamilika, inakuja Morogoro – Makutupora na kwenda Tabora – Kigoma – Mwanza – Uvinza – Kaliua – Kalema mpaka Rwanda. Pongezi kubwa kwa Serikali. Hiki kitu kitaacha legacy kubwa kwa Serikali ya Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, hakitasahaulika milele na milele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Dkt. Mpango katika mpango wake ni vyema akaweka bandari kavu pale Tabora kwa sababu Tabora ndiyo njiapanda ya safari zote hizi tunazozitaja hapa. Mabehewa yakitoka 20 au 30 Dar es Salaam yakafika Tabora yanakatwa
10 yanayokwenda Mwanza, yanakatwa matano yanayokwenda Kigoma, yanakatwa mangapi yanayokwenda Mpanda lakini pia tuna karakana kubwa ya ukarabati wa reli pamoja na vichwa vya treni. Kwa hiyo, nikuombe sana kaka yangu, Mheshimiwa Dkt. Mpango, pale Tabora kunafaa kabisa kwa bandari kavu kwa sababu ni njiapanda ya nchi zetu jirani za Maziwa Makuu za Kongo, Rwanda na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali yangu kwa ununuzi wa ndege, imefanya kazi kubwa sana. Nilikuwa napitia taarifa miaka 30 iliyopita kabla Rais, Dkt. John Pombe Magufuli hajaingia madarakani hatukuweza kununua hata ndege moja leo ndani ya miaka minne tumenunua ndege saba na ndege ya nane inakuja. Hii ni pongezi kubwa na histora kubwa ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeweza kuanzisha mradi mkubwa wa umeme ambao una megawati 2,100. Mradi huu ukikamilika naiona Tanzania imekuwa Malaysia, imekuwa Uturuki, naona maendeleo yatakayokuja kwa kasi kwa kupata umeme wa uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze elimu bure; watoto wetu kule vijijini sasa wanasoma, hata ukitafuta house girl kumpata ni shida. Yote haya ni matunda mazuri ya udhibiti wa pesa za Serikali, ukusanyaji wa pesa za Serikali hatimaye imeweza kuwasomesha bure watoto wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maji yametapakaa, hata kama kero bado ipo lakini kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano inaonekana. Watu wakumbuke tu historia kwamba ndani ya miaka 50 ilikuwa vipi na ndani ya miaka minne imekuwa vipi. Tumefanya kazi kubwa sana, tunastahili kumuunga mkono Rais, kumpongeza na kumtia moyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu, tumeunganisha mikoa, wilaya lakini sasa tunakwenda kwenye vijiji na mitaa. Vilevile viwanja vya ndege vimepanuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wakati tunachangia jana mpango hapa, Mheshimiwa Silinde, leo hayupo, alisema kuna mambo mengi hayajatekelezwa akasema hasa Bandari ya Bagamoyo haijajengwa na ipo kwenye Mpango. Mimi nimwambie, hatuwezi kutekeleza mradi ambao una masharti ya ajabu ajabu na ya hovyo. Masharti yanayosema tukianza kujenga Bandari ya Bagamoyo, Tanga isijengwe, Dar es Salaam isipanuliwe, Mtwara isijengwe, leo tukubali tu kwa sababu ni kwamba kipo kwenye Mpango; kwani Mpango ni Msaafu au ni Biblia, si kitu ambacho kinaweza kurekebishika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimtoe wasiwasi, miaka mitano bado, hii ni miaka minne. Hii nchi ni ya kwetu wote, Mheshimiwa Silinde ni mzalendo, ni Mtanzania, alete mwekezaji ambaye hana masharti Bandari ya Bagamoyo itajengwa. Hatuwezi kujenga bandari kwa masharti ya aina hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii ya Awamu ya Tano imefanya kazi kubwa sana wote tumeona lakini na mimi niongelee kidogo tu suala zima la Serikali za Mitaa. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge, kazi tunayoifanya hapa ni kazi kubwa sana, tunajadili Mpango wa Serikali utakaotupeleka kwenye bajeti yetu, itakayowasaidia Watanzania kupata dawa, kusomesha watoto wetu, kujenga vituo vya afya, kujenga barabara na kadhalika. Leo anainuka Mbunge anaanza kuongelea vyeo tu, yaani hapa ni vyeo tu, watu wanawaza vyeo hawawazi Watanzania. Mimi niwaombe sana tujadili Mpango wa Serikali tuisaidie ili iweze kutuletea bajeti nzuri itakayosaidia wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua sheria na taratibu zipo, sisi hapa ni Wabunge; kama kuna mtu kaonewa, kadhulumiwa aende kwenye vyombo vya sheria akatoe malalamiko yake na sheria itafuata mkondo wake na sio kuja kwenye Mapendekezo ya Mpango kuanza kuongea habari za vyeo tu. Tukae tukifikiria Watanzania na tusifikirie hivyo vyeo kwa muda wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe mapendekezo yangu kidogo kwenye Mpango wa Maendeleo. Niiombe Serikali kama inawezekana kipindi kijacho uchaguzi wa vitongoji, vijiji, Madiwani, Wabunge na Rais hebu ufanyike siku moja. Mimi nadhani itakuwa ni vizuri zaidi kuliko kupanga baada ya miaka minne uchaguzi huu, baada ya miaka mitano uchaguzi huu. Kwanza inaigharimu Serikali kwa sababu tunapitia uchaguzi mara mbili, tunaweka mawakala mara mbili na tunatoa semina mara mbili. Kwa hiyo, mimi naona hakuna haja ya kumaliza pesa za Serikali, ni vyema uchaguzi wote ukafanyika siku moja na mambo yakaisha na tutakuwa tume-save pesa ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wenzetu wameitwa na Mheshimiwa Jafo kupewa kanuni za uchaguzi waende wakazitangaze kwa watu wao wakawaeleweshe kanuni hizi zinataka kufanya nini hawakufanya hivyo kwa sababu pesa zao zote za ruzuku zimeshapigwa, hawawezi kusaifiri Tanzania nzima kwa wanachama wao kwenda kuwaelimisha kwamba uchaguzi unataka moja, mbili, tatu. Naibu Katibu Mkuu alikuwepo pale kwa Mheshimiwa Jafo wakati anatoa hizo kanuni, hawakuzifuata kanuni hizo. Sasa kama wameonewa basi niwaombe waende mahakamani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongee suala zima la tumbaku. Tumbaku ni zao linaloingizia Serikali Pato kubwa la Taifa kwa sababu linauzwa kwa fedha za kigeni. Niiombe sana Serikali iweke mkakati maalum na wa makusudi wa kuhakikisha inalikomboa zao hili la tumbaku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imejitahidi, Waziri Mkuu binafsi ameonesha jitihada kubwa sana katika suala hili lakini Wizara ya Kilimo na yenyewe pia imefanya kazi kubwa sana. Hatimaye tumepata mnunuzi anaitwa BAT (British American Tobacco). Nimwombe sana Waziri wa Kilimo mnunuzi huyu aje kwa muda husika ili tumbaku ile isikae muda mrefu na kuanza kuharibika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna kesi nyingi za FCC. Niiombe Serikali kumaliza kesi hizi ili sekta hii ya tumbaku iweze kufikia malengo iliyojiwekea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kidogo pamba na sisi Tabora tunalima pamba. Niishukuru Serikali kwa kuweka bei elekezi. Safari hii Serikali isingeweka bei elekezi naamini kuna wakulima wangeuza pamba mpaka 400, 500 na 600 lakini Serikali ikaingilia kati ikaweka bei elekezi pamoja na kwamba bei elekezi pia ina changamoto kidogo. Kwa hiyo, niiombe Wizara husika ianze kukaa na wadau wa pamba mapema kujadili mfumo bora na safi wa kuweza kununua pamba yao. Niombe hiki kikao cha wadau kisiwe mara moja kwa mwaka kiwe mara kwa mara ili kupata mawazo na ushauri mpya ili kuweza kuboresha zao hili la pamba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mpango niiombe Serikali tuna Shirika letu la TTCL. Shirika hili kwa kweli haliendi vizuri kutokana na ukosefu wa fedha, shirika hili linadai Serikali madeni mengi, zaidi ya…
(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Tambwe kwa ushauri wako mzuri.