Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kahama Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami naungana na Wabunge wenzangu kuchangia Muswada huu wa bajeti yetu ya 2019/2020. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Rais, Mawaziri, Naibu na Watendaji Wakuu wote wa Serikali kwa kazi kubwa sana wanazofanya na vile vile nawapa pole kwa kazi kubwa na mafanikio yanaelekea kuonekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuiondoa elimu ndani ya maendeleo, lazima twende nayo. Kwa hiyo, nasimama sehemu ya elimu peke yake. Suala hili la ajira tusijaribu kuitupia Serikali lawama, ni vizuri tutafute ufumbuzi ambao unaweza ukatusaidia aidha kuipunguza kwa nusu au kuimaliza kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanzia chini kabisa. Utaratibu huu wa watoto wa shule kwenda asubuhi, kama hatuna nafasi za kazi, ni vizuri tumwombe Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Naibu wake yuko hapa, aufikirie upya hasa kwa watu ambao ni wakulima, wafugaji na wafanyabiashara ndogo ndogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto wetu wanaamka saa 12.00 kwenda shuleni. Wakifika shuleni wanaanza kukimbia mchakamchaka. Baada ya mchakamchaka, saa 3.00 wanaingia darasani. Mpaka kuja kuanza masomo ni saa 4.00. Kwa nini watoto wasiende shuleni saa 5.00 wakiwa wamefanya kazi nyumbani ambapo tunatarajia kuja kuwarudisha huku wakimaliza University? Watakuwa wamefanya kazi nyumbani mpaka saa tano wataenda shuleni, watarudi kutoka shuleni saa 10.00 au saa 11.00.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli binadamu wote ni sawa, lakini Watanzania wote sio sawa, hilo ni lazima tukubaliane. Utaratibu huu wa kwenda asubuhi shuleni ni utaratibu wa Uingereza na nchi za Ulaya. Nchi za Ulaya bwana na bibi wanafanya kazi na hawana kazi nyingine pale nyumbani. Wanaondoka na watoto wao wanawaacha shule. Mume au mke anapowahi anampitia yule mtoto au watoto anarudi nao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile Ulaya kuna tishio la barafu. Barafu inaweza ikapiga London siku tatu, huwezi kurudi nyumbani au kutoka ndani. Kwa hiyo, kumwacha mtoto nyumbani au kumwacha anafanya kazi, hakuna kazi yoyote Ulaya ya kufanya, ni lazima uwapeleke shule. Sisi tunazo kazi za kufanya, kwa nini watoto wetu wasiende shuleni saa 5.00 mpaka saa 6.00 wakiwa wamefanya kazi huku?
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tuna watoto wanaosoma shule za kutwa za msingi zaidi ya milioni nne mpaka tano. Wakifanya kazi masaa manne nyumbani wakazalisha kilo moja moja ya mahindi, mtama au mpunga, tutakuwa tumeinua uchumi wetu lakini watoto wetu watakuwa wamepata elimu ya kutosha; ili watakapomaliza University, tunapowalazimisha wajitegemee, hawatakuwa na tatizo lolote la kurudi kijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, ni suala hilo hilo la elimu. Wizara ya Elimu, mara kwa mara namsikia Mheshimiwa Waziri anapambana na watoto watoro, lakini kwa utafiti na maoni tunayoyaona hapa, watoro ndiyo watu waliofanikiwa kwenye maisha. Kwa nini sasa Wizara ya Elimu isianze mtaala wa watoro? Iwe na mtaala wa watoro na mtaala wa watu wazuri. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivyo? Leo hii tumeshuhudia watu watoro wakifanya maendeleo makubwa sana. Leo tuna wanamichezo na wanamuziki na bahati nzuri na humu Bungeni tuna zaidi ya Wabunge 50 ambao ni watoro lakini wana mafanikio makubwa sana. Kwa ridhaa yako kama utakubali nitaje hata kumi… (Kicheko)
WABUNGE FULANI: Wataje.
T A A R I F A
MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Silanga.
MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumpa taarifa Mheshimiwa Kishimba yeye ni sehemu ya mtoro lakini alifanikiwa sana kuchenjua dhahabu pamoja na mwaka 1992 kuanzisha ununuzi wa pamba hapa nchini lakini alikuwa mtoro hakumaliza shule ya msingi. (Makofi/ Kicheko)
MWENYEKITI: Mheshimiwa jirani unasemaje na taarifa hiyo?
MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, yeah, naiunga mkono. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli maneno haya yanaweza kuwa kama ya utani lakini mimi nimekwenda darasani nimefika darasa la nne, nimeelewa kitu wanachofundisha huku kina faida maeneo fulani naenda kuanza shughuli zangu kwa nini mimi nakamatwa? Mimi nimeishia darasa la nne nikagundua ndani ya elimu kuna faida ya kitu fulani na kinaweza kupata faida muda huu, nikaenda kuanza procedure na kile kitu, kwa nini mzazi na mimi tukamatwe kurudisha shuleni tuendelee miaka 20 isiyo na faida? (Kicheko)
MBUNGE FULANI: Child labour.
MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu anayesema hapa ni child labour, je, old labour inasemaje? Maana utaratibu wote huu tunaohangaika ni wa Ulaya. Ulaya baada ya miaka 18 mtoto anakuwa mali ya Serikali na mzee baada ya miaka 60 unakuwa mali ya Serikali unatunzwa lakini sisi ni wewe na wanao sanasana university anachokunyan’ganya ni pesa na mifugo yako anakurudishia mtoto, inatupa wakati mgumu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ubaya gani Wizara ya Elimu ikawa na mitaala ya watoro na Walimu wa wale watoro wawe ni wale watu waliotoroka shuleni ambao wameonesha mafanikio. Kweli mimi ni darasa la saba lakini Christopher Columbus aliyevumbua America safari yake ilikuwa kwenda India lakini akapotea kwa utoro akavumbua America. Mbona wote tunaenda kuomba pesa America nani anayewakataa Wamerikani kuwaita ni watoro. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili la elimu ni lazima kabisa Wizara ya Elimu ifanye utafiti kwa vitu vingi sana. Leo hii VETA yetu kuna simu zaidi ya milioni 10 Watanzania wanazo lakini VETA haina mtaala wa kutengeneza simu. Leo tuna biashara mpya zimepatikana za madalali, hakuna Chuo cha Madalali lakini wako mtaani na wanaendesha shughuli zao wao VETA vitu walivyon’gan’gania haviko kwenye soko. Kwa hiyo, naomba sana sana Wizara ya Elimu waendelee kufanya mdahalo na wananchi ili tujaribu kujikwamua kwenye tatizo la ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, leo hii usipopeleka mwanao shule unashtakiwa lakini mtoto akipata kazi wewe hakutumii hela huwezi kumshtaki. Tunaomba Wizara ya Elimu na Wizara ya Ustawi wa Jamii watuletee sheria hapa ili mzazi anaposomesha mtoto wake anapomuomba pesa au anapopiga simu watoto hawapokei wawajibike kisheria. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunahangaika kweli Majimboni, wazee wanakwenda TASAF mtoto yuko Dar es Salam ana maisha mazuri, kila siku unasikia ana birthday, mzazi aliyetumia ng’ombe nyingi sana kumsomesha mtoto anateseka. Haruhusiwi kwenda Polisi kulalamika na haruhusiwi kwenda Dawati la Jamii haiwezekani. Tunaomba Mheshimiwa Waziri lete huo Muswda, mbona wewe wanapofika form six unawakopesha, unawawekea na riba wanapopata kazi unawakata, mimi mzazi nina kosa gani kumdai mwanangu. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini wazazi tujiandae kutoa radhi? Kwa nini mimi nijiandae kulalamika na kutoa radhi kwa nini Serikali isitusaidie, Mwanasheria Mkuu wa Serikali yuko hapa atusaidie, kwa nini tuwe tunalalamika, nitamlaani mwanangu, kwa nini nitoe radhi? Mwanangu nimemsomesha na nimemtunza kwa nini nijiandae kuja kutoa radhi badala ya Serikali kunisaidia sheria ndogo ili mtoto asipopokea simu, hakutoa pesa mimi niende Polisi ili apate Polisi Order anitumie pesa. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa zoezi hili Serikali wameanza wao wenyewe ruhusu na wazazi ili mtu unaposomesha shule nijue na mimi kwamba nina invest kuliko sasa hivi naambiwa tu kwamba elimu unamwachia urithi wa kwako wewe, sasa urithi gani huo huyo amepata maendeleo yake wewe unabaki unazubaa kijijini, hauna chochote. Maneno haya tunayaongea kama mzaha lakini wazee kule vijijini wana shida nyingi sana…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Profesa Kishimba kwa mchango wako. Huyo ndiyo Profesa Kishimba nilimuita. (Makofi)