Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Buyungu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi hii. Pia naomba niungane na wenzangu niipongeze Serikali nzima kwa maana ya Rais na Serikali yote ambayo imetuletea Mpango huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo machache ambayo nataka niishauri Serikali kwa sababu tunapojadili Mpango maana yake ni kuboresha rasimu hii, ndiyo process ya budgeting inaanza hivyo. Nianze na suala zima la disaster preparedness. Nimeona katika Mpango ambao Waziri ametuletea, nadhani ukurasa wa 85, sikumbuki vizuri lakini napenda nijikite hapo kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajenga miundombinu, tena ya gharama kubwa; viwanja hivi vya ndege, barabara, madaraja, miundombinu ya umeme, mabwawa makubwa kama haya ya Stiegler’s Gorge; miundombinu yote hii inataka pesa nyingi. Nachotaka kusema kwa kuwa tunajenga miundombinu hii lazima pia tuwe na utamaduni wa kuilinda miundombinu yetu tunayoijenga kwa gharama kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitazama siku za nyuma Serikali ilikuwa na lugha ya maintenance sasa hivi ni kama lugha hiyo inaanza kupotea. Kwa mfano zamani tulikuwa na Public Works Department inajenga barabara lakini kila mwaka kulikuwa na periodic maintenance na wanapita wanatengeneza; ile yote ilikuwa ni kuhakikisha kwamba miundombinu hii inayojengwa kwa gharama kubwa inatunzwa na inalindwa ili baadaye tusije tena kutumia pesa nyingi za bajeti ambazo tumepanga kwa ajili ya maendeleo kutengeneza miundombinu ambayo imeharibika. Kwa kufanya hivi tutaokoa gharama kubwa au kuepusha ile pesa ambayo imepangwa kwa bajeti ya mwaka huu tunaanza kuitumia kwenye kurekebisha miundombinu ambayo imeharibika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna majanga mengi, yako mafuriko ambayo kama tumekuwa tunafuatilia yamegharimu Serikali pesa nyingi, watu wamekufa, hata Kenya mambo haya yamewapata; yapo majanga yanayotokana na moto, yapo matetemeko, zipo radi, lakini vyote hivi vinapotokea lazima viigharimu Serikali, lazima Serikali irudi tena kwa sababu huwezi kuacha kitu kimekwishatokea ukasema tukiache kwa sababu hakimo katika mpango wa maendeleo. Kwa hiyo, nachotaka kuishauri Serikali yangu ni kwamba lazima tujenge utamaduni wa kuwa na utayari wa kupambana na majanga yanapojitokeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano huu mradi mkubwa ambao tunaujenga wa Stiegler’s Gorge, mradi huu kwa kweli ni mfano mzuri. Ukitazama mradi kama huu tungekuwa na approach kama hii katika miradi mingi maana yake katika kuwa prepared kwa kujenga miradi hii siyo lazima kuweka bajeti tu kwa ajili ya kusubiri janga litokee maana majanga ni matukio, matukio ndiyo hayo majanga. Hata hivyo, katika utamaduni ule wa wa kusanifu miradi,kwa mfano, unajenga mradi wa bwawa, unatengeneza mradi ambao ni multipurpose, mradi kama wa Bwawa la Rufiji, utafua umeme, utatoa maji ya kunywa, maji ya kumwagilia; mradi huo unaweza kutengeneza flood control kwa maana ya kwamba hata haya mafuriko mengine ambayo yanajitokeza utakuwa umeyapunguza kwa kiasi kikubwa. Kwa hiyo, approach hii ya kutengeneza miradi ambayo ni jumuishi inaweza kutufanya tukawa tayari kupambana na majanga kila yanapotokea. Kwa hiyo, natamani kuona kwamba katika miradi tunayoijenga tunajiwekea utaratibu wa kujikinga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ni-declare interest; niko katika Kamati ya LAAC, nimetembelea miundombinu mingi midogomidogo; ujenzi wa madarasa, ujenzi wa health centers, public buildings nyingi, lakini sehemu zote ambazo nimepita kama nimeona nyingi labda ni moja au mbili, hata kukumbuka tu kuweka kitu kidogo kama mtego wa radi, hatukumbuki. Kila wakati unasikia radi imepiga darasani watoto wamekufa, walimu wameumia lakini unakuta hata kitu kidogo kama hicho tu; kuweka mtego wa radi kwenye jengo ambalo ni la public, kwenye makanisa yetu, hatukumbuki kuweka vitu kama hivyo. Kwa hiyo, nataka nijikite hapo, kwenye suala la disaster preparedness Serikali kwa kweli hata kama sio lazima kuweka kitengo na kukigharamia sana lakini kila sekta basi angalau ijikite katika kujiandaa na kupambana na majanga yanapotokea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka nizungumzie ni suala la kugharamia kilimo. Kilimo ndiyo kila kitu lakini Wabunge wengi wamelalamika, fedha tunazotenga kwa ajili ya kilimo bado hazikidhi mahitaji. Fedha tunazotenga kwa ajili ya miradi ya umwagiliaji, tuna
23.4 million hectors, tumefanya hekta laki sita tu lakini fedha tunazotenga kwa ajili ya shughuli ni ndogo na bado tunataka twende katika uchumi wa viwanda, ili tujenge uchumi wa viwanda lazima kilimo nacho tukipe msisitizo. Tutenge fedha za utafiti kwa ajili ya pembejeo, tutenge fedha za kilimo kwa ajili ya maghala, kujenga silos ili kilimo hiki kikue kiweze kutusaidia kutoa inputs kwa ajili ya viwanda hivi tunavyotaka kuvijenga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi ni wanachama wa SADC. Nakumbuka mwaka 2003 kulikuwa na mkutano Maputo, pale Maputo nchi zote wanachama walitoka na Azimio la Maputo 2003 (Maputo Declaration). Maputo Declaration iliazimia na sisi tulisaini kwamba kila nchi mwanachama itenge asilimia 10 ya bajeti yake kwa ajili ya kugharamia kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sio lazima kwa mwaka mara moja utenge asilimia 10 lakini kuanzia mwaka 2003 mpaka leo natamani kuona on an incremental basis towards ten percent, kwamba kila mwaka tumeongeza kiasi gani ili angalau tufikie asilimia 10 ya bajeti zetu kwenda kwenye kilimo. Hilo namuomba Mheshimiwa Waziri na Waziri wa Kilimo waliangalie kwa sababu ni sisi wenyewe tulikubali kwamba tutatenga asilimia 10 kupeleka kwenye kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa bado niko kwenye kugharamia kilimo, naomba nizungumzie suala la Mfuko wa Kuhimili Bei za Mazao. Asubuhi nimemsikia Naibu Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Bashe, alisema vizuri tu kwamba intervention ya Serikali kwenye masuala haya ya masoko ya mazao haitakuwa tena kama ilivyokuwa. Nami nakubaliana naye kwa sababu lazima turuhusu soko liji- regulate lakini masoko ya mazao ni very fragile. Matatizo yanapotokea lazima tuwe na utaratibu wa kuhimili mtikisiko wa bei hizi, hasahasa bei zinapoanguka katika masoko ya dunia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka mwaka fulani tulikubaliana kwamba tuanzishe Mfuko wa Kuhimili Bei za Mazao. Tukasema tuanze na mazao mkakati manne ya kahawa, korosho, tumbaku na pamba. Nakumbuka Wabunge wengi walikubaliana na jambo hili lakini tangu tumelizungumza na nafikiri mpaka leo sijapata mrejesho kwamba hivi uanzishaji wa utaratibu huu wa Mfuko wa Kuhimili Bei za Mazao angalau kusaidia wakulima ku-absorb shocks umefikia wapi?
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Malizia Engineer.
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwa jambo moja tu, nalo ni suala la usimamizi wa miradi (contract management). Hii culture ya usimamizi wa miradi (contract management) bado inatugharimu. Narudia tena kusema niko katika Kamati ya LAAC lakini mambo nayoyaona huko hasa kwa miradi midogomidogo Serikali inaingia hasara kubwa sana kutokana na poor contract management. Miradi mingi inaingia kwenye gharama ambazo sio za lazima, inaingia kwenye variation orders ambazo siyo za lazima. Yote hii inatokana na miradi ambayo haiwi managed vizuri. Kwa hiyo, ipo haja kabisa kusimamia suala hili la kusimamia miradi kwa ajili ya kuokoa fedha na gharama za Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yangu yalikuwa haya machache, sisi tunasema kusema mengi sio kuyamaliza, mengine tutaendelea kuchangia, naunga mkono hoja. (Makofi)