Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kwa Mwaka 2019

Hon. Rev. Peter Simon Msigwa

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Iringa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kwa Mwaka 2019

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, binafsi nianze kwa kuipongeza kwa sehemu Kamati kwa kazi nzuri ambayo wameifanya, na kazi kubwa ya Kamati hii, hii ni oversight committee, hasa baada ya kupata ripoti ya CAG ambaye ndio jicho letu la Bunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na mambo mengi ambayo mmetupa Kamati Mwenyekiti, kuna mambo mengi ya msingi ambayo sisi kama Wabunge na kama wasimamizi wa rasilimali za Taifa hili tunataka tuyapate majibu kama Wabunge. Na wajibu wetu sisi kama Bunge ni kuisimamia Serikali na kwa bahati nzuri sana Serikali hii imejipambanua sana kwamba haitaki fedha zitumiwe hovyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nina maswali kadhaa ambayo ninamini kwamba Kamati yako haijatutendea haki kama Wabunge. Baada ya Ripoti ya CAG kuna mambo mengi sana ambayo CAG aliyaona. Kwa mfano kwenye ripoti yako sijaona masuala ya flow meter; ripoti ya CAG ilionesha kwamba haifanyi kazi, na Mheshimiwa Rais pamoja na Waziri Mkuu wamekwenda mara kwa mara na inaonekana flow meter hii kule bandarini haifanyi kazi; kwa nini kwenye Kamati yako hujatupa ripoti hii tukaweza kujua kuna kitu gani kinachoendelea?

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Ripoti ya CAG, CAG alihoji masuala ya uniform za polisi, na kwenye ripoti yake CAG alisema kukosekana kwa nyaraka za kuthibitisha uletaji wa mzigo, niliomba hati ya kupokelea shehena ya mizigo bandarini ukurasa wa 311, Mheshimiwa Waziri aliyekuwa Waziri wa Mambo ya ndani hapa aliweka rehani mpaka Ubunge wake. Nilitegemea Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati hii, hizo gharama za ripoti na ile sintofahamu…

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utaratibu.

KUHUSU UTARATIBU

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana. Ninashangaa kwa kweli kuona Serikali inashindwa kujibu hoja, hizi hoja ni kitabu cha Serikali, tunafanya kazi ya Umma, nikushukuru kwa kutoa uamuzi ambao ni sahihi kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu niliyokuwa naizungumza ni kwamba haya ni mambo ya msingi, nimezungumza hii flow meter ilionekana kuna wizi mkubwa, na Rais alizungumza. Kwa nini Kamati haijatuambia Wabunge tuone huo wizi umedhibitiwa vipi?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nilienda kwenye hoja nyingine kuhusiana na CAG alidai documents zinazohoji nani aliagiza sare za polisi. Hizo bilioni 16 zinalipwaje, mlipwaji ni nani, tenda ilikuaje? Ninahoji ni kwa nini Kamati – bilioni 16 siyo hela ndogo – kwa nini Kamati haijaleta hapa tuone huyo mtu alilipwajelipwaje kwa sababu CAG alionesha haya mambo. Haya mambo ni kama yanapotea gizani, ni mambo ya msingi ambayo Serikali inataka tutunze hela na ni kweli ni haki yetu kusimamia hela, haya ni mambo ya msingi hayahitaji kufichwa. Watanzania wanapaswa wajue, Bunge hili linapaswa lijue.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Lugola alisema ataweka rehani Ubunge wake hapa. Mwenyekiti naomba atuambie hivyo vitu vyote CAG alivyovidai vimepatikana? Na juzi hapa tumesikia Rais anasema amelipwa sijui bilioni 10; amelipwalipwaje? The Government moves on paper, amelipwaje huyu mtu, kwa namna gani? Kamati haijatuletea.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, kwenye masuala ya TPA kule bandarini; TPA inataka kuvunja mkataba wakati mkandarasi yule ameshalipwa zaidi ya asilimia 70 na walimleta mtaalam kutoka nje asimamie, ni kwa nini wanataka kuvunja mkataba? Tunataka tujue haya mambo ili Bunge tusimamie vizuri Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, watu wa NIDA; CAG alishasema vile vifaa vya BVR havifanyi kazi, vilikuwa sio compatible na windows ili vitoe vitambulisho vya uraia pamoja na vya kupigia kura lakini inasemekana sasa hivi vile vitu havifanyi kazi na wameagiza vitu vingine tena vipya hivi vingine vyote vinatupwa nje. Hizi ni hela za Watanzania tunataka tujue haya mambo yanakwendaje, yanafanyikaje haya mambo kienyejikienyeji na hili ni Bunge na Mheshimiwa Rais amesema watu wanafanya mikataba bila Bunge kujua. Haya masuala sisi hatujui yanafanyikaje? Masuala ya e-passport tulizungumza sana hapa Bungeni mauzo ya passport wakati mwingine yanaonekana kwamba kuna faida inaonekana. Hii passport chanzo chake kilikuwaje, tuliingia mkataba na nani? Tulitumia kiasi gani? Tunalipaje, tender ilikuwaje? Passport moja gharama yake ikoje? Sasa litakuwa Bunge la aina gani ambalo haliwezi kuhoji mambo kama haya.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati ni oversight committee ambayo inapaswa isimamie pesa za walipa kodi, wana wajibu wa kutuambia mambo makubwa kama haya ndani ya Bunge lazima tuyajadili, hatuwezi tukawa tunashughulika na mambo ya Simba na Yanga hapa tunaacha mambo ya msingi haya ya hela ya wananchi. Hatukuja kwenye Simba na Yanga pamoja na kwamba mimi mpenzi wa Simba. Tumekuja hapa kuhakikisha tunasimamia kodi za wananchi, hela ya wananchi, si ndiyo mtazamo wa Mheshimiwa Rais kwamba hela ya nchi isiibiwe, haya mambo makubwa Kamati inaweza kuachaje ili yasijadiliwe kwa upana wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ningeomba Mwenyekiti anapokuja kuhitimisha hapa, kuna mambo ya msingi ambayo ni lazima Bunge lijue, hizi ni hela nyingi, mabilioni ya Watanzania ambayo yanapaswa tuyajadili kwa kina ili Bunge lichukue nafasi yake. Hii mikataba mingi imeenda kimyakimya, kiholela holela Wabunge tunapita tu tunaondoka na sasa hivi tunamaliza muda wetu, tukienda kuulizwa kwa wananchi tutaenda kusema nini. Naomba Mheshimiwa Mwenyekiti atakaposimama hapa atuambie kwa nini kwenye ripoti yao hawajatuambia masuala ya e-passport, masuala ya NIDA, masuala ya nguo za Polisi; na nasikia kuna baadhi walienda wakachungulia tu watuambie walipata hizo documents, walienda kuchungulia tu makontena, kama walioneshwa mlangoni tu kule ndani labda kulikuwa na baiskeli tutajuaje sisi, kama walidanganywa zimetoka China inasemekana zimetengenezwa hapa hapa Tanzania, tunataka hayo mambo tujue, ndiyo wajibu wa oversight committee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ningeomba Mheshimiwa hoja yangu ni kwamba pamoja na kazi nzuri waliyoifanya na mambo mengine, lakini kuna mambo ya msingi ambayo Taifa la Watanzania wanataka wayajue na yapatiwe majibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. (Makofi)