Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati Hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020

Hon. Sonia Jumaa Magogo

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati Hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020

MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye hoja iliyo mbele yetu. Kabla sijaanza kuchangia nianze kwa kuwapongeza Wenyeviti wetu wa Kamati kwa wasilisho zuri. Nijielekeze sasa moja kwa moja kwenye kuchangia kwenye Kamati ya Uwekezaji ambayo ndiyo Kamati niliyopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua dhamira kuuu ya Serikali kuwekeza katika mashirika ya umma ni pamoja na kukuza uchumi wa nchi, kuchochea maendeleo ya sekta mbalimbali na kutengeneza ajira kwa wananchi. Pamoja na haya yote, tumekuwa tukushuhudia Serikali ikiwekeza fedha zake kwenye baadhi ya mashirika, lakini mashirika haya miaka yote yamekuwa yakizalisha hasara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sioni sababu ya kwa nini Serikali iendelee kuchoma pesa zake kwenye mashirika haya ambayo hayana tija. Kwa sababu Serikali imekuwa ikitoa mitaji yake kulingana na mahitaji ya mashirika yale, lakini unakuta mashirika mengine yanafanya vizuri sana na mashirikia mengine yanashindwa hata kutoa gawio kwa Serikali. Kwa hiyo badala kuendelea kuyaangalia haya mashirika ambayo yamekuwa yakizalisha hasara kila mwaka ningeishauri Serikali iangalie kwa upande wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitolea mfano wa Mkoa wangu wa Tanga, Mkoa wa Tanga tumejaliwa kuwa na viwanda vingi sana, lakini vile viwanda sasa hivi vimegeuka kuwa magofu, mfano tulikuwa na Kiwanda cha Chuma, Kiwanda cha Mbolea, Kiwanda cha Mkonge, Matunda na Chai. Hivi viwanda vyote sasa hivi havifanyi kazi. Iwapo serikali itaviangalia hivi viwanda na kuviwezesha nina imani vinaweza kuleta tija katika mapato na vilevile kuongeza ajira kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande mwingine nigusie mashirika yenyewe ambayo Serikali inaweka mitaji yake. Hizi taasisi unakuta zenyewe kwa zenyewe zinasababishana kurudurishana nyuma na kuweka ugumu katika utendaji. Hii ni kwa sababu utakuta taasisi moja inaihudumia taasisi nyingine kwa mkopo, lakini imekuwa ni ngumu sana zile taasisi kurejesha ile mikopo kwa wakati, hivyo kufanya ugumu katika utendaji wa hizi taasisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuchukulie mfano mashirika ya hifadhi ya jamii, haya mashirika sehemu yake kubwa ya uendeshaji yanategemea michango ya wanachama ya kila mwezi. Unakuta michango ile ya wanachama inakatwa vizuri kwenye mishahara wa mwanachama, lakini haipelekwi kwa wakati ama haipelekwi kabisa sehemu husika. Hii hupelekea Mifuko yetu hii ya Hifadhi ya Jamii kufanya kazi katika mazingira magumu sana. Hivyo, niiombe Serikali ingalie ni namna gani inaweza kusaidia haya mashirika ambayo yamekuwa yakitoa huduma na mwisho wa siku hayapati mrejesho wa fedha ili yaweze na yenyewe kutekeleza majukumu yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo ningezumzia suala la ubunifu; unakuta mashirika yetu haya yana fursa nyingi sana ambazo wanaweza kuzitumia na kupata kipato ambacho kingewasaidia kujiendesha wakati wanasubiri ruzuku za Serikali. Kwa kushindwa kutumia ubunifu wao wanakaa muda mrefu bila kutekeleza majukumu yao, kwa sababu ya kukosa ruzuku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sio hilo tu hata kwenye kujitangaza, sisi wenyewe kama Wajumbe wa Kamati tulikuwa tunakwenda maeneo mengine tunashangaa. Tunakuta bidhaa ambazo ni nzuri sana lakini sisi wenyewe hatufahamu kama zile bidhaa zinategenezwa mahali pale ama zinapatikana pale. Kwa hiyo kwa kujitangaza haya mashirika itasaidia kukuza kipato chao na kuweza kutoa gawio kwa Serikali.

Pia niipongeze Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa jitihada zao walizofanya na wanazoendelea kufanya na kupelekea kupata gawio zuri kwa mwaka 2018/2019. Pia niiombe Serikali iangalie yale yaliyoainishwa kama changamoto na Msajili wa Hazina ikiwemo mfumo hafifu wa TEHAMA, Sheria ya Msajili wa Hazina, ongezeko la mahitaji ya watumishi wenye utaalam na kukosekana kwa mfumo wa fedha za uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo pia ningekazia kwamba hii Ofisi ya Msajili wa Hazina iongezewe bajeti, kutokana na ukubwa wa kazi yake ili iweze kufanya kazi yake kwa ufanisi na tupate kile tunachokihitaji. Kwa upande kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina ningependa kushauri wafanye Audit Management za mara kwa mara kwa haya mashirika na taasisi ambazo Serikali inawekeza fedha zake. Kwa sababu tumeshuhudia hapa kuna mashirika yalikuwa yanasema kwamba hawawezi kutoa gawio, lakini baada ya kupewa siku 60 wameweza kupata, wengine wameanza kuleta gawio, kwa hiyo hii inaonesha kwamba wakati mwingine taarifa wanazotoa zinakuwa sio sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)