Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati Hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020

Hon. Amb. Adadi Mohamed Rajabu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati Hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nashukuru sana kupata nafasi hii ya kuchangia hoja hizi za Wenyeviti wote wawili. Kabla sijaendelea, napenda kuungana na ndugu na Waheshimiwa Wabunge wote kumwombea ndugu yangu, rafiki yangu na jirani yangu ambaye alikuwa anakaa hapa ambaye ametangulia mbele ya haki. Tuzidi kumwombea ili roho yake iende peponi huko alikotangulia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Rais na Mawaziri na Maofisa wote ambao wameshughulika kwenye mapatano ya mkataba wa Barrick ambao naamini kabisa kwamba utatuongezea pato la Taifa katika siku za hivi karibuni. Mkataba huo ni mzuri na ni vizuri mikataba kama hiyo basi ikafanyika kwenye sekta nyingine na siyo madini tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, napenda kumpongeza Waziri na Maofisa wote kwa kuweza kugawa vizuri mapato na fedha ambazo wanazipata Wizaran, pamoja na kuwa hazitoshi, lakini wameweza kuzigawa katika mpango ambao ni mzuri na ambao unapaswa kupongezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, tumpongeze pia Kamishna Mkuu wa TRA ambaye anafanya kazi nzuri, anaendelea kuleta mapato mazuri na siyo siri kwamba mwezi uliopita tu wa Desemba, tumeweza kupata karibu shilingi trilioni 1.9 ambazo hatujawahi kupata katika nchi hii. Ni vizuri Kamishna Mkuu akaendelea na moto huo huo ili kila mwezi basi atupe mrejesho na kuonekana kwamba mapato yanaendelea kupatikana kwa uzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, pia napenda tumpongeza Gavana wa Benki Kuu ambaye ameweza ku-stabilize dollar. Mtakumbuka dola ilikuwa inaporomoka kwa kasi kubwa sana, lakini governor na maofisa wake wameweza kukaa vizuri na kui-stabilize mpaka sasa hivi iko kwenye kiwango ambacho kinaridhisha kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nampongeza sana TR, Msajili wa Hazina kwa namna ambavyo ameweza kusimamia mashirika haya na kuweza kutoa dividends ambazo hazijawahi kupatikana katika nchi hii. Ni sifa kubwa sana, nanyi mmeona mabilioni ya fedha ambazo mashirika haya yameweza kuyatoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati imeshauri mambo mbalimbali katika Wizara ya Fedha. Mambo mengi yamechukuliwa na mengine hayakuchukuliwa. Mengi yaliyochukuliwa matunda yake yameonekana, lakini yapo mengine ambayo hayakuchukuliwa na ningependa kushauri Wizara ya Fedha iweze kuyaangalia vizuri ili kuhakikisha kwamba basi wanayachukua kwa lengo la kukuza uchumi wetu na kuongeza pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi ambayo inabidi Serikali izidi kuifanyia kazi sana. Mradi wa Liganga na Mchuchuma, umekuwa ni kero. Siyo kero tu, Kamati tumejadili kwa kina na Mheshimiwa Waziri anajua kwamba viwanda vya chuma hapa nchini ambavyo viko 11 au
17 vyote vinachukua malighafi kutoka nje. Naamini kabisa mradi huu wa Liganga na Mchuchuma ungekuwa unafanya kazi, basi kusingekuwa na haja ya viwanda hivi kuagiza malighafi hizi kutoka nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu sana maamuzi ya mradi huu yafikie mwisho. Ni mradi mkubwa na utaona kwenye Mpango wa Maendeleo, Serikali ina mpango pia wa kujenga SGR ambayo itatoka bandarini Mtwara na kuweza kufika mpaka huko Liganga na Mchuchuma. Sasa ni vizuri Serikali ikaweka umuhimu na kuona kwamba mradi huu ni muhimu sana. Nimewahi kuona mradi wa makaa ya mawe kule Zimbabwe njia ya kwenda Victoria Falls, ni mradi mkubwa na unatoa ajira nyingi sana na uchumi wa nchi ya Zimbabwe unategemea sana mradi wa makaa ya mawe ambao uko kule Midlands.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri Serikai iliangalie, tumelipigia kelele sana na tunaomba basi uamuzi ufikiwe. Isitoshe, kuna mradi kwa mfano wa kiwanda kile cha General Tyre Arusha, kila siku hapa Bungeni tumekuwa tukiongea suala hilo. Ni vizuri ikafikia mwisho, maana sioni kitu gani ambacho NDC wanafanya kwenye ule mradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, tumekuwa tukipendekeza na hata kwenye bajeti iliyopita kuhusu ujenzi wa bandari ya uvuvi. Najua colleagues wangu wameongea hapa asubuhi na tukaambiwa kwenye bajeti kwamba iliyopita kwamba Serikali ina mpango wa kuanza kujenga bandari ya uvuvi, sasa sijui ni ujenzi huo umefikia wapi? Ni vizuri tukapewa ufafanuzi kutoka kwa Waziri mhusika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ilipata fursa ya kutembea kwenye baadhi ya nchi, tulikwenda Rwanda pamoja na Uganda ambapo kwenye hiyo study tour lengo lake ni kuangalia namna gani Treasury Single Account (TSA) inafanyakazi. Sisi tulikwenda Uganda na kwa kweli tuliona mpango huo unaendelea vizuri na unafanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi hizo ambazo zinafanya, tulijiongeza na kwenda kutembea mjini na tuliona mambo ya ajabu ambapo tulikuta bidhaa nyingi sana ambazo zinapita hapa hapa kwetu, zinakwenda mpaka Kampala na Kampala kule unakuta Watanzania wengi na sio Watanzania tu, pamoja hata na wa nchi jirani wanakwenda Kampala kwa ajili ya kununua wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wengi wa nchi jirani walikuwa wanakuja kwetu Kariakoo sasa hivi wamehamia kule Kampala. Sasa tuliongea na Mheshimiwa Waziri na tuliona kwamba ni muhimu tuangalie tumekosea wapi? Ni kitu gani ambacho tunatakiwa tukifanye? Kwa nini bidhaa zitoke hapa, zipite hapa, ziende Kampala na watu wetu wa hapa watoke hapa waende kununua kule wazirudishe hapa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hapa kwenye transit kuna ushuru ambao unatakiwa ufanyike na tumemshauri Mheshimiwa Waziri atengeneze Kamati ndogo iweze kukaa na kuona kwamba huu ushuru utafanya nini ili tuweze kuwa vizuri? Kwa hiyo, naamini kabisa Mheshimiwa Waziri atalichukua hilo na kuweza kuona kwamba tunafanya nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti,...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Adadi. Kengele ya pili imelia.

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja ya Mwenyekiti.