Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kunipa nafasi, kwanza naomba nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye ametujalia zawadi ya uzima na kuweza kuendelea na shughuli zetu hapa za kuwakilisha wananchi wetu. Kwanza kabisa naomba pia nichukue nafasi hii kuishukuru sana na kuipongeza Serikali ya Awamu Tano kwa kuwa taarifa zote tulizosomewa hapa zote zinaonesha ufanisi na hali chanya ya kuweza kuinua uchumi wa nchi yetu na hivyo tuna kila sababu ya kuipongeza Serikali kwa sababu mikakati yote ambayo tumeelezwa na kamati zote ni mikakati chanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo, nitachangia maeneo mawili tu. Naomba nianze kwa kuchangia kwenye suala zima la mfumuko wa bei. Kunapokuwepo na mfumuko wa bei hali hii inaondoa utulivu baina ya wananchi wetu na kwa hivyo hii hasa inatokana na upungufu wa chakula nchini. Kama kuna upungufu wa chakula ni wazi kwamba kutakuwa na mfumuko wa bei. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kipindi kilichopita cha 2017/2018 na 2018/2019 kwamba mfumuko wa bei ulipungua kutoka asilimia 5.3 hadi asilimia 3.5, kwa hivyo, ni hali nzuri. Kwa dalili tunazoziona tunamshukuru Mungu ni kudra zake pale ambapo mvua zinakuwa nyingi na hazileti madhara, lakini tunavyoangalia hali tunavyokwenda pamoja na mvua nyingi zinazonyesha lakini huenda ikaweza kuleta athari na kupunguza chakula hapa nchini. Hivyo Serikali isibweteke iweze kuona ni namna gani itajizatiti kuhakikisha kwamba hakutakuwa na mfumuko wa bei na hali ya chakula itakuwa nzuri nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza Serikali pia kwa kuunda chombo cha NFRA, NFRA ni chombo ambacho ni muhimu sana katika kuweka akiba ya chakula ili kuweza kuweza kutumia wakati wa uhitaji na hata pengine kuuza nje. Hivyo tunaiomba Serikali iweze kukijengea uwezo chombo hiki ili kutekeleza majukumu yake ya kununua chakula cha kutosha na hali hii ya kuwa mazao ya kutosha inaweza ikatusaidia katika masuala matatu. Kwanza, italeta utulivu kwa wananchi watakuwa na chakula cha kutosha; lakini vilevile inaweza ikasaidia kuhamisha wananchi kuwa na soko la uhakika mahali ambapo watauza mazao yao. Chombo hiki kitakaponunua mazao ya kutosha na huko tunakoelekea kwenye Serikali yetu ya viwanda tunaweza tukatumia mazao haya haya reserve ambayo itakuwa ziada ili kutumia katika kusindika mazao ya kilimo katika kuanzisha viwanda vya ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali hii si ya kubweteka kama ambavyo nilisema lakini Serikali itenge bajeti ya kutosha kuweza kuimarisha chombo hiki cha NFRA lakini vilevile na bodi ya mazao ya mchanganyiko. Naamini kwamba connection ya NFRA na mazao haya ni kuonesha ni jinsi gani kilimo ni muhimu katika kuinua uchumi wa nchi yetu. Kwa hivyo ni vizuri Serikali nayo ikatupia jicho suala zima la kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo nilitaka kuchangia ni deni la Taifa. Tofauti na mfumuko wa bei ambapo umepungua kwa kipindi kilichopita, lakini deni la Taifa limepanda kidogo kwa asilimia 2.1. Hili tunaambiwa imesababishwa na masuala mbalimbali moja ikiwa mahitaji ya kugharamia miradi ya maendeleo na hasa pale ambapo inatumia mikopo vilevile ahadi ya misaada kutoka nje. Tunavyojua tunazo sheria mbalimbali zinazoenda sambamba na kutumia fedha za Serikali na hivyo nilikuwa naishauri Serikali pale ambapo tunahitaji kutumia fedha hizi kwa ajili kugharamia miradi mbalimbali sheria za fedha na kanuni na taratibu mbalimbali zitakapozingatiwa na Serikali nina imani kwamba suala hili la deni la Taifa litakwenda likipungua na hasa pale ambapo Serikali itazingatia matumizi haya ya fedha za Serikali ambapo hakutakuwa na ubadhilifu na itazingatia hata mikataba ya kimataifa pale ambapo tunaona kwamba tunakiuka taratibu zile za kutumia fedha za Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la kuchangia mwisho mwisho ni pale ambapo unarudia michango mingine ambayo wenzangu wamesemea. Niliandaa kuchangia maeneo haya mawili na naomba sana Serikali izingatie yale ambayo nimeshauri na ahsanteni sana kwa kunisikiliza. (Makofi)