Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

Hon. Vedastus Mathayo Manyinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba nitumie nafasi hii kwanza kukushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye hotuba ya Kamati ya Miundombinu pamoja na Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi binafsi nawapongeza sana watu wa miundombinu na naipongeza sana Serikali kwa namna ilivyoweza kutoa fedha za kutosha kuhakikisha kwamba barabara na bandari zetu nyingi zinaweza kufanya kazi. Ndiyo maana kwa ushahidi ukiangalia katika bajeti iliyopita ilikuwa shilingi trilioni 4.2 lakini kwa mwaka huu tumeenda almost 4.9. Hongereni sana kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na haya mafanikio makubwa ya Serikali lakini bado yapo mambo ya kimsingi ambayo yanahitaji kuangaliwa na hasa katika kipindi hiki. Wote tunatambua hiki ni kipindi ambacho katika nchi nzima mvua nyingi zimenyesha na kutokana na hali hiyo, barabara nyingi sasa zimeharibika kwa maana ya miundombinu. Kutokana na hali hiyo, hata zile barabara ambazo zilikuwa zimejengwa ambazo zilikuwa na hali nzuri zimeendelea kuharibika.



Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kupata ufafanuzi kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu kwamba hivi wamejipangaje? Maana leo ukienda kwa mfano kule Musoma Jimboni kwangu nadhani mafuriko yameongoza kuliko mahali pengine popote pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye zile Kata kama za Nyakato, Bweri, Kitaji mpaka kwa bahati mbaya sana kumetokea maafa katika Jimbo langu kutokana na haya mafuriko, sasa ile miundombinu yote imeharibika. Napenda kufahamu Kamati ilijipangaje katika kusimamia Serikali kuhakikisha kwamba katika hiki kipindi kifupi tunarudisha ile miundombinu iliyokuwepo katika hali yake maana vinginevyo hali itakuwa mbaya zaidi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ambalo ningependa kulielewa sambamba na hilo ni kwamba Serikali imekuwa na utaratibu mzuri wa kutenga fedha ambazo zinatengeneza hasa barabara katika kiwango cha lami. Fedha hizi zimekuwa zikipatikana aidha kutoka Serikalini na nyingine kupitia misaada kutoka maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake kwenye zile barabara za Manispaa pamoja na Halmashauri zinazojengwa kwa kiwango cha lami, wote tunatambua kwamba Halmashauri zetu hazina uwezo wa kuendelea kuziimarisha. Sasa kutokana na hali hiyo, zile barabara za lami zinapokuwa zimeanza kuharibika maana yake zinaachiwa hata yale mashimo tunashindwa kuyaziba. Kwa hiyo, badala ya kutumia fedha kidogo kwenye kutengeneza zile barabara, matokeo yake zile barabara zinaendelea kuharibika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo mifano hai, siku moja kamati yako ikipata nafasi ikaja pale Musoma Mjini, kuna barabara kama ya Shabani, kama yale mashimo yangeweza kuzibwa ile barabara ingeendelea kupitika, lakini leo hii ukienda pale tunatamani tu bora ile lami yote iondolewe ibaki kuwa barabara ya vumbi kuliko ilivyokuwa barabara ya lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ukienda kwenye ile barabara yetu ya Mkenda ambayo ndiyo kioo cha mjini, nayo imeanza kutoboka, Halmashauri haina uwezo wa kuziba yale mashimo. Matokeo yake baada ya miezi sita ile barabara yote itakuwa haipo na nguvu kubwa iliyotumika itakuwa imepotea bure. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vinginevyo, binafsi naishukuru Serikali kwa maana ya toka mwaka juzi 2018 tumeweza kupata fedha za kutosha. Maeneo mengi sasa pale Musoma Mjini tumejenga kwa kiwango cha lami. Ila kwa bahati mbaya sana, yale maeneo ambayo yapo usoni mwa Mji wa Musoma ndio yameendelea kuharibika. Kwa hiyo, ni imani yangu kwamba atakaposimama atapata nafasi ya kutuambia wamejipangaje kwenye fedha za kuboresha barabara zinazoharibika? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, napenda kuchangia kuhusu uwanja wa ndege. Tunatambua Serikali imefanya juhudi kubwa na nzuri za kuendelea kuboresha viwanja vya ndege. Nimesikitika wakati nasoma hapa kwenye taarifa yake kwenye viwanja vya ndege ambavyo vinajengwa, Kiwanja cha Musoma hakimo, lakini kimekuwa kikisemwa na tuliona hata katika bajeti kwamba kitajengwa, lakini nimeanza kupata mashaka makubwa kwanza baada ya kuona hapa kwenye hii hotuba hakimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nakumbuka toka mwaka jana mwanzoni uthamini ulifanyika. Kwa kawaida sisi wote tunatambua kwamba uthamini unachukua miezi sita baada ya hapo una-expire. Sasa madhara ambayo wale watu wa Musoma wameyapata toka uthamini ufanyike, zile nyumba zao sasa ziliwekwa X, hakuna watu, wapangaji wamekosekana wala hakuna shughuli zinazoendelea na wale watu bado hawajalipwa fidia. Halafu tunapokuja kwenye vitabu, hapaoneshi juhudi zozote za Serikali kwa ajili ya kujenga ule uwanja wa ndege wa Musoma. Sasa hata tunapata tabu kubwa katika kusafiri, lazima tuje Mwanza ili tuweze kusafiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu atakaposiamama atuambie, ule uwanja wa Musoma unajenga ama haujengwi? Kama haujengwi ni vizuri wakaenda wakafuta zile X na wakawaelimisha watu ili waweze kuendelea na maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nigusie kidogo kwenye suala la bandari. Katika hili, mimi binafsi naiomba Kamati yako ipate nafasi wakati wa ziara za Kamati itembelee pale Mjini Musoma. Pale tunayo bandari ambayo nayo ilishakufa kwa sababu hakuna meli inakuja wala hakuna activity yoyote inayoendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, tulikua pale na mwalo wetu wa Mwigobero. Ule mwalo ndio watu wetu walikuwa wanafanya biashara ndogo ndogo, mitumbwi yote na samaki walikuwa wanagoa pale na biashara mbalimbali zilikuwa zinafanyika pale. Kilichotokea, watu wa bandari walikuja pale na wakatuambia wakati huo kwamba wanategemea watusaidie kuboresha ile bandari na wakasema wataiboresha bandari ifanane na ile Bandari ya Kirumba. Nasi tukafurahi tukaona kama ingeweza kutusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo ile bandari wameichukua na hakuna kinachoendelea na wale watu wote waliokuwa wanafanya biashara pale wamefukuzwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa, malizia.

MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Kwa hiyo, naomba Kamati yako nayo ikiweza kupata nafasi ya kuja pale, itatusaidia kutatua hilo tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana, ahsanteni sana. (Makofi)