Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

Hon. Frank George Mwakajoka

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tunduma

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kutoa mchango wangu siku ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuko Bungeni kama Wabunge, nia na madhumuni ni kuishauri sana Serikali. Tunavyozungumza sisi upande wa Upinzani tuchukuliwe kama ni Wabunge ambao tuna haki na tunaishauri Serikali kama ambavyo Wabunge wa Chama cha Mapinduzi wanavyoweza kuishauri Serikali na kazi yetu kubwa ni kuangalia gaps ambazo mnashindwa kuziba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko kero nyingi sana za wafanyabiashara ambazo mwaka 2018/2019 Serikali ya Chama cha Mapinduzi ndani ya Bunge hili waliahidi kupunguza kero mbalimbali kwa wafanyabiashara. Huwezi kuamini, mpaka sasa hivi kwenye nchi hii bado kero za wafanyabiashara hazijatatuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana 2019 wakati wa bajeti hapa ilionyesha kwamba kuna kodi karibu 54 ambazo zilitolewa. Sielewi kodi hizi ambazo zilitolewa kama kweli Serikali ilifanya utafiti na ikakutana na wafanyabiashara, kama kweli ndiyo zilikuwa kero za wafanyabiashara. Hata hivyo, bado kuna kero kubwa sana kwa wafanyabiashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunakaa mpakani pale, tunaona jinsi ambavyo wafanyabiashara wengi wanahamia kwenye nchi za jirani na Tanzania. Ukiangalia wafanyabiashara wengi wa Tanzania wanakimbilia Malawi, wengine wanakimbilia Zambia, lakini pia wako wafanyabiashara wakubwa sana ambao sasa hivi wanahama nchi, wanakwenda kuwekeza viwanda katika nchi nyingine na Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi bado inaona wafanyabiashara kama ni watu ambao hawaaminiki. Hakuna nchi yoyote duniani ambayo inaweza ikapiga hatua kama itaona wafanyabiashara ni watu ambao hawaaminiki na siyo wadau wakubwa katika Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wajibu wa Serikali ni kuhakikisha kwamba wafanyabiashara mitaji yao inakua ili waweze kulipa kodi na Serikali iweze kupata fedha na kuhakikisha kwamba inatekeleza miradi mbalimbali ambayo inapendekeza katika Taifa hili. Leo Serikali hii inajinasibu kwamba inakusanya mapato mengi sana, lakini ukweli tu ni kwamba wafanyabiashara mitaji yao imeshuka na fedha ambazo zinakusanywa sasa hivi karibuni wafanyabiashara wanalalamika, wananyang‟anywa tu hizo fedha, siyo kwamba wanapenda. Ndiyo maana wafanyabiashara wengi ukienda Segerea na kwenye Magereza mbalimbali wamekamatwa wamewekwa kwa kesi za money laundering ambazo hazina ukweli wowote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaishauri Serikali iwajibike kuhakikisha kwamba biashara zinaboreka katika nchi hii ili kuhakikisha kwamba Watanzania wengi wanafanya biashara na mitaji inakua ili biashara Serikali iweze kukusanya mapato. Tunaamini kabisa katika mwaka unaokuja wa 2020/2021 tuna uhakika kabisa kwamba Serikali hii itashindwa kukusanya mapato ya kutosha kwa sababu wafanyabiashara wengi watakuwa wameshafilisika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu tulikuwa Uganda, tumeshangaa sana. Wafanyabiashara wote wa Dar es Salaam sasa hivi wanafunga bidhaa zao Kampala; wafanyabiashara wa Moshi, Arusha na Mbeya wameanza kufunga biashara zao Kampala pale badala ya Dar es Salaam. Sasa unashangaa, Jiji ambalo tulikuwa tunaamini kabisa kwamba ni soko la Afrika Mashariki, sasa hivi limeshakufa. Sasa hivi watu wanakwenda Kampala wanafanya biashara, wanafunga biashara kule, wanakwenda kufanya biashara Tanzania. Kwa hiyo, wanafunga mizigo ya madukani kwenye Mji wa Kampala. Sasa hivi Mji wetu wa Dar es Salaam umeshakufa kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunavyozungumzia biashara, tunazungumzia uchumi wa nchi. Tusipojua kwamba uchumi wa nchi ni biashara, tutakuwa tunapoteza muda. Nafikiri Waziri wa Viwanda na Biashara akae na Waziri wa Fedha wajaribu kuangalia matatizo ambayo yako Tanzania, ambayo tunaona yanaendelea kuua biashara na yatafilisi kabisa biashara za watu na biashara zitakufa katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza humu na ukijaribu kusoma unaona kabisa kwamba kuna mipango mizuri sana, lakini hakuna utekelezaji mzuri ambao unatoa mwanga kwa wafanyabiashara kufanya biashara katika Taifa hili. Ndiyo maana tunawaambia kila wakati kwamba bajeti ambazo tunatengeneza, Serikali hii inatekeleza bajeti hizi kwa kuangalia uchumi wa vitu na siyo uchumi wa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza kila wakati hamtuelewi. Ukiangalia bajeti ambazo zipo, kwa mfano bajeti ya miundombinu; ina-cost karibuni trilioni 4.6 lakini ukienda kuangalia kati ya hizo fedha, kwenye kilimo utaona kabisa wamewekeza shilingi bilioni 100, lakini inakwenda shilingi bilioni tatu. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Mwakajoka.