Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Mbozi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. PASCHAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia. Nami nitachangia Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji na nitaanza na utekelezaji wa kusuasua wa bajeti ya maendeleo ya Wizara ya kilimo.
Mheshimiwa Spika, sasa imekuwa ni kama mazoea Serikali kutekeleza bajeti ya kilimo kwa kusuasua. Hivi navyozungumza kwa taarifa ambazo ninazo kwa sababu mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Kilimo Mifugo na Maji, kwa taarifa ambazo zilitolewa kwenye Kamati yetu ni kwamba kati ya pesa za maendeleo ambazo zilikuwa zimetengwa karibu shilingi bilioni 143.57 hadi sasa fedha ambazo zimeshapokelewa ni kidogo tu, ni kama shilingi bilioni 21.4 tu sawa na 14.9%. Kama tutaenda hivi tafsiri yake ni kwamba mpaka tunafika mwezi wa sita mwishoni kwa kweli sidhani kama tutafika asilimia 40. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama hatuwezi leo kutekeleza bajeti ya maendeleo kwa kupeleka fedha tafsiri yake ni kwamba Wizara hii kuna shida na shida hii ni kubwa siyo ndogo. Kama shida hii ipo ni vizuri Serikali ituambie tatizo liko wapi? Kama Bunge tunaidhinisha fedha lakini fedha ambazo zinatolewa ni asilimia kidogo tu ambayo ni asilimia 14. Katika asilimia 14 hii fedha za ndani zilizotolewa ni kama shilingi bilioni 5 tu lakini fedha za nje ni bilioni 15. Yaani leo fedha za kutoka nje zinakuwa nyingi kuliko fedha za ndani. Hivi uzalendo uko wapi kati ya hao watu wan je wanaotupatia pesa nyingi na fedha zetu za ndani ambazo zinakuja kidogo? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hapa kuna tatizo hatuwezi tukaendelea kuendesha nchi kwa kutumia fedha za nje tu. Kama zitaendelea kutokuja fedha za nje, kwamba, kama zisingekuja Bilioni 15 maana yake tungekuwa na Bilioni 5 tu ambazo ni fedha za ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa mimi nataka nijue, kwa sababu Serikali imekuwa ikijinasibu kwamba makusanyo yanazidi kuongezeka kila mwezi, lakini leo utekelezaji wa Bajeti ya maendeleo, sekta ambayo inaajiri Watanzania zaidi ya asilimia 70 utekelezaji wa Bajeti yake ndiyo namna kama hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kweli ni vizuri Wizara hii wajipime waone kama wanatosha, na kama hawatoshi siyo dhambi kuwapisha wale ambao wanadhani kwamba wanaweza wakafanya vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hili jambo si la kwanza na huu mwaka si wa kwanza maana yake mwaka jana mwaka wa fedha ilikuwa hata asilimia 50 hawakufika. Mwaka uliotangulia, nyuma kidogo, ilikuwa asilimia 16, na miaka ya nyuma ilikuwa asilimia tatu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa tukienda kwa trend kama hii kwa sekta inayoajiri Watanzania walio wengi tutakuwa hatuwatendei Watanzania haki. Ni vizuri tuangalie namna ya kuweza kufanya, na Serikali ione kwamba Watanzania hawatendewi haki hata kidogo.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kuhusu pembejeo. Hivi ninavyozungumza hapa mbolea aina ya UREA kwa Mikoa inayozalisha chakula; wanaozalisha mahindi kwa wingi, Mikoa ya Songwe, Rukwa, Ruvuma, Iringa na maeneo mengine, mbolea aina ya UREA imeadimika; yaani mbolea kuipata ni shida kweli.
Mheshimiwa Spika, sasa Serikali ituambie, kwamba kwa kutumia mfumo wa kununua mbolea kwa pamoja (bulk procurement) tutaweza kutatua tatizo hili la upatikanaji na bei? Leo mbolea aina ya UREA imeadimika, na kipindi hiki msimu huu, kwa maana ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, ndio muda ambao wakulima wanatakiwa waweke mbolea ya kukuzia mahindi.
Mheshimiwa Spika, inawezekana msimu unaokuja kukawa na tatizo la chakula kwa sababu wananchi hawana mbolea ua kukuzia aina ya UREA. Hata hivyo hata hiyo kidogo ikipatikana bado bei elekezi haifuatwi. Kwa mfano kutoka shilingi 54,000 kwa mfuko wa UREA leo umefika shilingi elfu 68. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa Serikali hii ni Serikali ya wanyonge gani?, kama mbolea inapanda kutoka 54,000 kwenda 68,000 ni mnyonge yupi anayesaidiwa hapa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nadhani Wizara hii ya Kilimo kuna tatizo. Bila kujali Itikadi ya Vyama vyetu ni vizuri Wabunge wote tuangalie namna ya kuweza kuiwajibisha Serikali ya namna hii. (Makofi).
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kuhusu suala la kulipa mawakala walio-supply pembejeo mwaka 2015. Mawakala walikopa pesa Benki wakapeleka vocha kwa maana ya ku– supply zile pembejeo kama mbolea pamoja na mbegu hawajalipwa pesa zao ninavyoongea hadi leo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wako Mawakala hawa waliokopa pesa Benki wameuziwa nyumba zao na wengine wamefariki kwa sababu ya pressure kwa sababu anauziwa nyumba hana mahali pa kukaa lakini hadi sasa Serikali imejificha kwa mwamvuli wa kwamba tuko kwenye uhakiki; hivi ni uhakiki gani ambao hauishi? Mbona Serikali haituambii? Hata kama wamehakikiwa watu wako watano iwalipe hao watano waliohakikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo watu wanafariki kwa sababu ya pressure ya kuuziwa nyumba Serikali haijatuambia itawalipa lini watu hawa ambao wamehakikiwa, na ni watu wangapi?
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha atuambie wangapi wamehakikiwa hadi leo. Vilevile watuambie mpango wa kuwalipa; kwamba watawalipa lini? Kwa sababu wanaendelea kupotea hawa. Wanasomesha wana watoto na wana ndugu wanaowategemea, leo hawajalipwa. Hawa ndio wanyonge ambao waliisaidia CCM hata kuipa kura. sasa hili jambo Mheshimiwa Waziri aangalie kama Serikali imeshindwa kuwalipa iwaambie kwamba tumewadhulumu, hatutawalipa; kwa sababu kama ni tangu 2015 hadi leo tafsiri yake ni kwamba Serikali haina dhamira njema ya kuweza kuwalipa Mawakala hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lambo lingine kuhusu suala Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kutoa gawio Serikali Kuu. Jambo la kustaajabisha, Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko hivi karibuni ilitoa gawio Serikali Kuu, takriban mlioni karibu milioni mia tano. Jambo la kusikitisha ni kwamba leo Wizara inazungumza hapa utekelezaji wa Bajeti wa kusuasua lakini Serikali Wizara ya Kilimo kupitia Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko wanatoa gawio Serikali Kuu milioni mia tano.
Mheshimiwa Spika, sasa sijui inakuwaje, yaani mgonjwa ambaye inatakiwa uongezewe damu inafika mahali nawe unataka kumtoa damu, hili ni jambo la ajabu sana. (Makofi)
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Spika, taarifa.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, yaani mgonjwa unatakiwa uongezewe damu na wewe unaamua ku toa damu kwa mwingine.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Spika, taarifa.
T A A R I F A
SPIKA: Mheshimiwa Haonga kuna taarifa unapewa subiri kidogo. Naomba umpe taarifa, ndiyo endelea.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Spika, naomba tu nimpe taarifa Mheshimiwa anayezungumza, kwamba kuna suala la mchanganyo wanaposema gawio watu wengi wana confuse. Nadhani Mheshimiwa Haonga hajaweza kutofautisha kati ya gawio na mchango.
Mheshimiwa Spika, tunaposema gawio ina mambo matano ndani yake. Kuna suala la dividend, kwa maana ya gawio. Kwa mashirika na taasisi ambazo zinafanya biashara per se inaitwa dividend, ndiyo maana ya gawio. Kuna asilimia 15 ya pato ghafi ambayo ni mchango wa Taasisi kwa Serikali.
Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo naomba nimpe Mheshimiwa Haonga taarifa kwamba hiyo iliyotolewa si gawio ni mchango wa Taasisi kwa Mfuko Mkuu wa Serikali. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Haonga unapokea taarifa hiyo ya Mheshimia Chegeni?
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, mimi naomba niendelee. Huyu bwana wananchi wake wakulima wa pamba kule wanadai Serikali takriban Bilioni 4.4, sasa nadhani angepata nafasi ya kuweza kuchangia angeweza kuzungumzia mambo ya pamba ili kule kidogo aweze kuwasaidia wakulima wa pamba. Naomba nimuache, nimempuuza tu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ninachozungumza hapa ni kwamba, leo kama Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko hizo fedha kama zilikuwepo nyingi kwa nini wasingepeleka kwenye angalau wangepeleka NFRA basi wakanunue hata mahindi; kwa sababu bado zinazunguka kwenye Wizara hiyo hiyo. Leo wanatoa pesa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko unapeleka Serikali Kuu halafu mwisho wa siku….
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, taarifa.
T A A R I F A
SPIKA: Taarifa Mheshimiwa Haonga unapewa. Mheshimiwa Getere.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, ahsante; naomba nimpe taarifa. Tufike wakati sasa humu tuangaliane kwamba tunafikiri kwa kiasi gani. Kama Wabunge humu ndani tunatunga sheria za mashirika kwenda kutoa dividend kwenye maeneo mbalimbali na mambo mengine ya kisheria. Tumetunga sheria humu ndani sisi wenyewe; kwamba kila wewe ukiwa Spika hapo ulipe hiki, ukiwa Shirika ulipe hiki. Sasa inakuwaje leo Mbunge aliyetunga sheria anasema hili ni la hovyo? Tunamuambia Mheshimiwa Haonga alete sheria humu Bungeni ya kuahirisha haya mambo aliyoyasema yeye.
MBUNGE FULANI: hayo yakwake.
SPIKA: Mheshimiwa Haonga pokea taarifa hiyo.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, nadhani watu wengine kama hawa itabidi tuwasamehe tu kwa sababu hawafahamu vitu vingi. Atuambie ni sheria namba ngapi, lakini pia nadhani tu ni vizuri afuatilie mambo mengine. Nadhani ameamua kunipotezea muda tu, tumsamehe tu anapoteza muda wa walipa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hapa ninachoshauri, ni vizuri Serikali iangalie, isiwe inakunywa uji wa mgonjwa kwa sababu kufanya namna hii huku ni kunywa uji wa mgonjwa; kwa sababu Wizara hii inachechemea, inatakiwa isaidiwe na si Wizara tena ianze kutoa gawio huku inafanya hivi. Sasa mambo kama haya ni mambo ambayo kwa kweli hii Wizara inatakiwa isaidiwe. Tunayazungumza haya si kwamba labda tunaichukia sana Wizara, tunapenda kuisaidia Wizara, lakini inaonekana kwamba Serikali haiko tayari, Wizara hii iweze kusaidiwa, Wizara ambayo inaajiri Watanzania zaidi ya asilimia 70. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kuhusu suala la Serikali kutoangalia vipaumbele vya wananchi; na hapa nazungumzia suala la maji.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais alipozunguka kwenye ziara mbalimbali nchini maeneo mengi wananchi wetu walizungumzia kuhusu maji. Alikuja Mbozi wananchi walizungumzia kuhusu maji, wanataka maji amekwenda Momba wanataka maji, amekwenda Tunduma wanataka maji, amekwenda Rukwa nai maeneo mbalimbali wananchi wanataka maji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi nashauri, ni vizuri Serikali ikaangalia vipaumbele vya wananchi badala ya kwenda kwenye vipaumbele ambavyo si vya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo ukienda nchi nzima hakuna sehemu ambayo wananchi wamesema wanahitaji ndege, wanasema wanataka maji. Kwa hiyo mimi nashauri, kama Bunge lako hili Tukufu ambalo unaliongoza wewe; ninashauri kwamba ni vizuri Serikali…
T A A R I F A
SPIKA: Mheshimiwa Haonga kuna taarifa sijui wapi! Kuna taarifa pale!
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, napenda nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge. Pamoja na kazi kubwa ambayo inayofanywa na Mheshimiwa Rais lakini hata katika Jimbo lake kuna Miradi dhahiri shahiri ya maji inayotekelezwa katika kuhakikisha wananchi wa Mbozi wanapata maji. Hata hivyo kikubwa nataka nimwambie kwamba ukisoma maandiko ya dini yanasema yapaswa kushukuru kwa kila jambo ahsante sana. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Haonga utakataa na hilo nalo la kwamba maandiko yanasema kushukuru kwa kila jambo.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, mdogo wangu Aweso afahamu kwamba zile fedha si fedha za msaada, ni fedha za walipa kodi wa Tanzania na watu wa Mbozi pia wanalipa kodi; afahamu siyo msaada. Ndiyo maana hata maeneo mengine ambayo hakuna Madiwani bado pesa zinakwenda kwa sababu ni kodi za Watanzania; kwa hiyo afahamu hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia afahamu kwamba pamoja na kodi zetu kulipa vizuri aelewe kwamba kwenye Jimbo langu pamoja na Miradi ya maji ambayo ilitakiwa imalizike imechelewa kumalizika, kwa maana hiyo hizi kodi zetu hazitendewi haki vizuri, maana wakandarasi wame- raise certificates ili waweze kulipwa hawajalipwa, na Mradi wangu wa maji pale Itewe wa Bilioni 1.5 Wakandarasi wame-raise certificates hazijalipwa hadi sasa; Aweso anafahamu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata pia visima vinne ambavyo Mheshimiwa Waziri aliahidi alipokuja Mheshimiwa Rais pale Mloo bado hujakamilisha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunapokuja hapa tunashauri ni vizuri Serikali ikaangalia vipaumbele vya wananchi.
Mheshimiwa Spika, tuangalie; nina uhakika hata ukienda Jimboni kwako wewe kule wale wananchi wanahitaji maji zaidi kuliko ndege. (Makofi/Kicheko)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)