Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Iringa Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niungane na wenzangu. Kwamba Wizara hizi ni Wizara nyeti kama alivyosema Mheshimiwa wa Bukoba; ni Wizara Mtambuka ambazo ni muhimu sana kwa uchumi wetu.
Mheshimiwa Spika, lakini mimi leo sitakuwa na huruma kwa Mawaziri. Asilimia kubwa ya Mawaziri tulionao katika Serikali hii wanafanya kazi ambazo ni ad hoc au wanashughulika na kero wanaacha suala la msingi na majukumu ya Kiwaziri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, majukumu ya Kiwaziri ni kushughulika na Sera, usimamizi na tathmini, lakini muda mwingi utawakuta Mawaziri hawa wako barabarani. Utamkuta Waziri huyu anachukua ruler anapima samaki; wanafanya kazi za operational ambazo inaonekana kwamba mifumo ya nchi hii imefeli. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Waziri anapoanza kufanya kazi za operation maana yake mifumo imefeli. Unamchukua Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi naye anaenda mahali na camera kutatua mgogoro wa Kiwanja sijui cha Juma na Hadija, maana yake mifumo imefeli. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, unamkuta Waziri wa Kilimo naye anahangaika sijui nani ameuza nini wanaenda kwenye kazi za operational wameacha majukumu yao ya kazi na hii inamuwia Rais kazi ngumu sana, inafika mahali na yeye mpaka anaanza kusuluhisha na ndoa barabarani. (Makofi/Kicheko) [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]
Mheshimiwa Spika, hatuwezi kuendesha nchi kwa namna hiyo kwa sababu kazi zenu Mawaziri mmeacha kushughulika na masuala ya Sera; na mimi nataka nijikite zaidi Maliasili kwa sababu mimi ni Waziri Kivuli wa Maliasili, lakini mnashughulika zaidi na kutatua migogoro na mnapenda sana kutatua migogoro kwa sababu mnaunda Kamati, ikiisha Kamati mnaunda nyingine, kwa sababu kuna hela huko; mmeacha majukumu yenu ya kutengeneza Sera. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hatuwezi kutoka kwenye maendeleo kama hamsimamii Sera zenu; kazi za migogoro kuna watu wanaofanya kazi hizo; na hatuwezi kuwaonea huruma lazima tuwaseme ndiyo kazi yenu mliyoitiwa hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Wizara hii ya Maliasili pamoja na kwamba ina vivutio vingi katika nchi yetu lakini bado haiko katika tano bora za kuwa destination ya watalii katika nchi hii; hilo ni tatizo kubwa kwa sababu tumeyaacha masuala ya msingi. (Makofi)
MHE. MBONI M. MHITA: Mheshimiwa Spika, taarifa.
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, leo unamkuta Waziri anapiga kelele kwamba anataka kurogwa ameacha kuleta ideas za kutuhamisha kutoka hapa tulipo twende hapo mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye mitandao kila wakati anasema wanataka kumroga badala ya kukaa chini.
MHE. MBONI M. MHITA: Mheshimiwa Spika, taarifa.
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, apate ideas namna gani ya kukuza watalii katika nchi hii. (Makofi)
SPIKA: Mchungaji kuna taarifa unapewa.
T A A R I F A
MHE. MBONI M. MHITA: Mheshimiwa Spika, nashukuru nilikuwa naomba nimkumbushe Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa mfumo wa kiutawala nchini Mawaziri wetu ni Wabunge pia ni Parliamentarians; na kama ambavyo sisi Wabunge hatuna mipaka kwenye kufatilia kero za wananchi basi ni hivyo hivyo Waheshimiwa Mawaziri ambao pia ni parliamentarians kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hawana mipaka kwenye ku-implement nafasi zao za Kibunge; ahsante sana.
SPIKA: Mheshimiwa Msigwa unapokea taarifa hiyo ya Mheshimiwa Mboni.
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, kama Waziri ni Mbunge achague kimoja anaweza akakataa Uwaziri afanye kazi ya Kibunge. Sisi ni back benchers, hawa wanatakiwa watupe majibu na wafanye majukumu ambayo wamepewa kwa mujibu wa kazi; lakini wewe unapoteza kodi ya wananchi tena usinipotezee muda kwanza tufanye kazi ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Wizara hii ya Maliasili ina majukumu mawili; kutunza Maliasili na kutangaza utalii. Kuna majukumu makubwa sana ya kutunza Maliasili, nalo ni jukumu kubwa sana. Wako watu wa TANAPA, Ngorongoro, kazi yao ni hiyo. Tunategemea Waziri asimamie sera. Narudia tena, operational si kazi yake, kama ni kutangaza wako watu wa TTB wanatangaza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo kazi ya kuleta watalii hapa imebaki kuwa ya travelling agents si ya kwake tena, wao sasa wanaingia kwenye operational na wanaacha kazi zao; ndiyo maana kumekuwa na migongano mingi katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano takwimu zinaonyesha watalii wengi wanaokuja nchini kama nilivyosema wanaletwa na travelling agents lakini Waziri hasimamii zile sera ili kuhakikisha tu-boost huu utalii uje. Hawa wanaosema wameongezeka wengi wao ni wale ambao hata hao akina Esther na akina Heche wakipita pale Serengeti nao wanajumuishwa kwamba ni watalii, nao wanaongezwa kwenye idadi; halafu mnajaza idadi hapa kwamba watalii wameongezeka kwa sababu hatufanyi kazi ambayo tunatakiwa tufanye. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mfano Waziri ambaye ni makini kama tunataka tukuze utalii katika nchi yetu…
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Spika, taarifa.
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: …Mheshimiwa Spika, China peke yake mwaka jana….
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Spika, taarifa.
T A A R I F A
SPIKA: Taarifa Mchungaji unapewa.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba kuna watalii wa ndani na kuna watalii wa nje. Sasa kama hawatambui watalii wa ndani labda ni tafsiri ya kule Iringa.
SPIKA: Taarifa unapewa Mchungaji.
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, nampuuza huyu, angekuwa Mbunge nampuuza, angekuwa Mbunge makini angejua utalii wa ndani unaingiza shilingi ngapi katika nchi hii. Sasa kwa sababu hujui pamoja na kwamba unatoka Serengeti tusipoteze muda. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mfano naishauri Wizara ya Maliasili, mwaka jana China peke yake watalii kutoka China kuja duniani kote kutembea sehemu nyingine walikuwa milioni 150, lakini waliokuja Tanzania walikuwa karibu 11,000 tu. Kwa Waziri makini, hayo ndiyo masuala ya kukaa na kujadiliana na ku-capturise katika watu milioni 150 hawa Wachina, Tanzania nifanye nini ili hawa watu milioni 150 wangapi watakuja Tanzania. Lakini badala yake unawachukua akina Steven Nyerere mnaenda Mlima Kilimanjaro sijui unamtangazia nani. Alisema Mheshimiwa Lema juzi hapa, unaenda nao kule unafanya kazi za operation, mnapiga picha sijui unamtangazia nani? (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwaka huu China ilitegemewa kutoa watalii milioni 180 duniani kote, lakini huoni Wizara ikikaa kwamba hapa pana mtaji mkubwa tunataka Wachina waje, hakuna mkakati wowote. Bahati mbaya sasa hivi imekuja hili gonjwa labda watapungua, lakini hakuna mkakati wowote ambao kama Wizara inapanga, kwamba kwenye eneo hili hebu tu-capturise tunawaleta watalii wangapi, badala yake unaenda kutatua mgogoro wa Loliondo sijui na nani.
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, taarifa.
T A A R I F A
SPIKA: Taarifa!
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, mwenzetu kwanza amejikita kwenye kulalamika haoneshi solution, lakini yeye ni mojawapo wa pioneer wanaopinga ununuzi wa career zetu kwa sababu ameonesha watalii wa China ni zaidi ya 50,000 lakini waliofika Tanzania ni wachache. Maana yake wenzetu ambao wana career zao ndio hao wanapeleka watalii wengi wanaishia kwenye nchi zao. Yeye anatakiwa sasa afike mahali ile pioneering yake ya kupinga Tanzania kuwa na ndege zake kwa ajili ya kuboresha utalii, aanze kuanzia leo kuunda na kutupa mawazo mengine yatakayotufanya tuende mbele. (Makofi)
SPIKA: Pokea taarifa hiyo.
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, Waziri makini angefanya projection kwamba Tanzania nataka nifanye iwe destination Africa watalii waje wengi wanatoka wapi? Waziri makini angefanya projection kama hivyo angweza ku-capitalize kutoka China kuna watalii wangapi. Sasa hivi wanaongoza kuja Tanzania ni watalii toka Marekani. Waziri makini asingehanganika na kina Steven Nyerere, Waziri makini angewachukua watu kama wakina Roger Federer, sijui kama unamjua wewe Roger Federer. Unawatangaza duniani kama wenzetu Rwanda wameandika visit Rwanda hapa unamchukua…
MBUNGE FULANI: Kuhusu utaratibu
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, unamchukua wachezaji wazuri wa tennis au unamchuku huyu wa basket LeBron James unatangaza nchi yako…
SPIKA: Kuhusu utaratibu.
KUHUSU UTARATIBU
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Spika, kwa Mujibu wa Kanuni ni marufuku Mbunge kujielekeza katika jambo ambalo halipo mezani na…
SPIKA: Tumsikilize tupe kanuni gani halafu uweze kuendelea. (Makofi)
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Spika, Kanuni ya 28.
SPIKA: Hebu isome, naomba tusikilizane Waheshimiwa twende kwa utaratibu. (Makofi)
Naomba tusikilizane, Waheshimiwa tusikilizane kanuni 28 amesema.
WABUNGE WENGINE: Aaaah!
MBUNGE FULANI: Kwa kuheshimu muda asisome.
SPIKA: Naam!
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Spika, kwa kuokoa muda na sijafungua tablet naomba nisisome.
WABUNGE WENGINE: Aaaah!
SPIKA: Unaweza ukakaa tu Mheshimiwa, Mchungaji malizia dakika zako.
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, kama tupo serious na kuongeza utalii lazima tuwe serious. Rwanda baada kusema inavyotangazwa mpira duniani kule ime-double watalii kuja kwenye nchi yao. Kwa hiyo, unaita watu, unatangaza na watu wanojulikana kama vile akina Serena Williams. Unatangaza, unachukua watu wakina hawa wakina Steven Nyerere nani anawajuwa? Hata hapo Blataya ya Malawi hakuna anayewajua lakini Waziri ndio anaenda nao kuwatangaza nani anawajua? We are not serious, anapanda mlima hata hatua mbili hafiki unamtangazia nani? (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama tupo serious na biashara hii nimshauri Waziri tumieni pesa watafuteni watu ulikuwa haupo, watafute kama watu akina Roger Federer, akina Djokovic wanajulikana akipiga tennis pale wanaandika visit Tanzania dunia nzima inaona. Na usiogope kurogwa hamna atakaye kuroga tangaza nchi vizuri. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Msigwa unaniacha hoji. Kuroga roga ndio kitu gani? Maana yake unaonge vitu ambavyo Spika havielewe. (Kicheko)
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, vilikuwa kwenye mitandao Mheshimiwa. Sera, sera ya utalii ilikuwa ni low volume high yield ambayo ni mwaka 1976. Lakini ukienda katika utendaji na jinsi Waziri anavyofanya sasa hivi ina-contradict. Sasa hivi wanataka mass tourism, lakini ukiangalia wanavyo practice hii ya low volume na high yield na hii ya mass tourism katika implementation yao kuna contradiction fukwe hamjaziandaa, hakuna vitanda ukingalia maeneo mengine…
SPIKA: Hiyo kengele ya pili Mchungaji.
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, wamenikatisha katisha Mheshimiwa.
SPIKA: Kengele ya pili.