Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ismani
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nami nianze kuwapongeza Wenyeviti wa Kamati zote mbili na zaidi Kamati yangu ya Ardhi na Maliasili. Nakubali kwamba tumepokea ushauri wao waliotushauri.
Mheshimiwa Spika, lakini niseme mambo mawili; la kwanza nianze na National Housing. Kamati imeshauri juu ya mapendekezo yao ya ukamilishaji wa miradi ile mikubwa ya National Housing. Nataka kuwahakikishia kwamba miradi ili itakamilika.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema juzi mimi nilifanya uamuzi wa kusimamisha ukopaji wa zile fedha makusudi kwa sababu tulitaka kujiridhishe mambo fulani. La kwanza hatua ya kwanza nimeunda bodi mpya yenye ueledi yenye uwezo wa kusimamia, lakini kazi ya pili ya bodi ile nimewapa ni kuhakiki ile miradi na mikataba. Tumeanza kufanya mazungumzo na contractors, tunataka tuhakiki ili kuondoa mambo fulani fulani yatakayotuwezesha kupunguza gharama za ujenzi wa ile miradi mikubwa. Lakini tatu, tunazungumza na mabenki, tuna- renegotiate ili angalau tupunguziwepunguziwe hivi mariba yao yale. Na tumeanza kufanikiwa.
Mheshimiwa Spika, tukishamaliza haya yote tunajua sasa tutapata picha ni kiasi gani cha pesa kinahitajika ili kukamilisha ile miradi. Kwa hiyo, nataka niwahakikishie Kamati na Waheshimiwa Wabunge, Serikali iko makini sana, lakini kama tulivyo sisi kazi yetu ni kuhakikisha kwamba pesa yetu tunaitumia kwa madhumuni yaliyo sahihi, kwa hiyo hii miradi itakamilika. Tumeanza vizuri na ule mradi wa Morocco, utakamilika kabla ya Juni, na baada ya hapo tutaenda Seven Eleven ile ya Kawe.
Mheshimiwa Spika, lakini ipo miradi mingi ambayo inaendelea. Hapa Dodoma tumejenga nyumba 150 na tunaendelea kujenga nyingine 30 na mwezi ujao tutaanza kujenga apartments nyingine mpya 100; hii ni kwa fedha ya ndani.
Mheshimiwa Spika, kutokana na uhakiki huu na kubana matumizi, Shirika la Nyumba sasa linaweza likajenga miradi mingine kwa pesa yake yenyewe. Na Shirika la Nyumba sasa limeanza kuaminika kwa kutumia kampuni tanzu ya National Housing ya ujenzi, sasa tuna miradi 35 mikubwa ambayo tumeaminika tunajenga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, moja ya miradi hiyo ni Hospitali ya Rufaa ya Musoma na Hospitali ya Rufaa ya Mtwara, wanaotoka huko wanajua. Hii ni kazi ambayo ilikuwa haifanywi na National Housing, sasa tumeamua katika Awamu ya Tano Shirika la Nyumba halitatumia contractor katika kujenga majengo yake na litashiriki katika ujenzi wa majengo mengine ya nchi. Kwa hiyo, Shirika la Nyumba sasa awamu hii inaenda vizuri zaidi kuliko awamu nyingine.
Mheshimiwa Spika, nataka msitafsiri uwezo au uendeshaji wa Shirika la Nyumba kutokana na ile miradi miwili mnayoiona pale Dar es Salaam. Ipo miradi mingi inaendelea, shirika limetulia, muundo umekamilika, bodi yenye weledi imekamilika inafanya kazi yake vizuri na yale yote ambayo yalikuwa yameshindikana sasa yatawezekana.
Mheshimiwa Spika, na zile nyumba ambazo zilikuwa zimejengwa kule mikoani tumebadilisha utaratibu sasa, watu watakuwa wanapanga zile ndogondogo zilikuwa zimejengwa muda mrefu lakini zilikuwa hazipati wanunuzi, tumeamua sasa kutengeneza utaratibu wa mpangaji mnunuzi. Kwa hiyo, mwananchi atakuwa na uwezo wa kupanga lakini hela yake mwisho wa yote atakabidhiwa nyumba. Tumeanza Kahama na sehemu nyingine, kwa hiyo zile nyumba ndogondogo kote kule tutaenda kwa utaratibu wa tenant purchase. Shirika la Nyumba nataka kusema linakwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini nije kwa baadhi ya mafanikio mengine ambayo yamezungumzwa kwenye Sekta ya Ardhi. La kwanza, Mheshimiwa Mch. Msigwa, katika miaka hii minne tumeweza kutatua migogoro zaidi ya 10,000 kwa njia ya utawala, maana yake nini? Kama wananchi hawa tusingewafikia na kutatua hii migogoro, wote wangekuwa mahakamani. Sasa wewe uniambie, wale wananchi wakiwemo wa Iringa niliowafikia juzi, miezi miwili iliyopita 500, leo wangekua kwenye mahakama wanatozwa hela na mawakili lakini leo wamepata nafuu kwa sababu Mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Tano wamekwenda kuwasuluhisha kiutawala, wame-save gharama wananchi lakini pia wamewatua mizigo na kuleta amani na utuivu. Na hivi sasa nina mwaliko wa Iringa tena, wanachama wako 200 wananchi wameomba niende kule, na wewe unajua. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo utatuzi wa migogoro kwa Wizara ya Ardhi iko kisheria. Pia tunatumia utatuzi mwingine kutumia mabaraza ya ardhi. Lakini pia Mheshimiwa Rais ametusaidia kutatua mgogoro ambao ulikuepo maisha, huu aliozungumza Mheshimiwa wa Maliasili. Vijiji 975 vilijikuta vimesajiliwa kwenye hifadhi za taifa, hifadhi za misitu, kwa miaka yote. Wamesajiliwa humu hati za TAMISEMI wamepewa, hati za ardhi wamepewa lakini bado kwenye GN za maliasili wanaonekana kama ni wavamizi. Na wakati huohuo baadhi ya watumishi wasio waaminifu walikuwa wanawatishatisha ili waondoke. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais kwa kutumia usuluhishi wa namna hii wa kutatua migogoro ameamua kuumaliza kabisa mgogoro huu kwa mara ya kwanza katika nchi hii. Vijiji 920 ambao walikuwa hawana matumaini ya kuishi katika vijiji vile sasa wamepewa matumaini mapya, watamilikishwa ile ardhi na hawataondoka katika ardhi yake. Haya ni matumaini mapya ambayo yamejengwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa hili angelijuaje maana nao huu ni usuluhishi. Sasa kama nao huu kuwapa matumaini mapya vijiji 920 vikiwepo vya Iringa, ipo mitaa minne pale Iringa Mjini ambavyo vilikuwa kwenye msitu lakini navyo mitaa ile imeambiwa ibaki pale. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka kuwaambia kwamba utatuzi wa mgogoro umetusaidia sana katika kuleta utengamano, amani na utulivu katika nchi hii. Siyo hayo, Mabaraza ya Ardhi nayo yamesaidia katika kutatua migogoro. Kuna kesi zaidi ya 112,243 zimetolewa maamuzi kati ya kesi zilizofikishwa kwenye mabaraza 139,943. Pia tumefanikiwa katika kipindi hiki kutayarisha Hati Miliki nyingi zaidi. Katika mwaka uliopita mwaka 2019 tumeweza kutayarisha Hati Miliki 325,000 ukilinganisha na hati zilizotolewa mwaka 2015 hati 54,000. Maana yake nini? Tumewapa matumaini watu zaidi ya 300,000 kumiliki ardhi yao na hivyo sasa wameweza kukopesheka katika mabenki.
Mheshimiwa Spika, zoezi la urasimishaji limefanywa kwa huruma ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli katika Awamu ya Tano. Watu waliokuwa wamejenga katika maeneo mijini bila kuwa na vibali, bila kuwa na hati, bila kuwa na viwanja vilivyopangwa na kupimwa, mara zote walikuwa wametishiwa usalama wao na Manispaa na Halmashauri za Miji kwamba waondoke, lakini Mheshimiwa Dtk. John Pombe Magufuli amesema hawa ni Watanzania walijenga tukiwaona, warasilimishiwe wapewe hati zao katika makazi yao mijini. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante, malizia Mheshimiwa Waziri.
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, zoezi hilo limefanikiwa sana tumetoa hati zaidi ya 500,000. Kwa hiyo, nakushukuru sana. Nataka niwahakikishie Wajumbe wa Kamati ile ya Maliasili na Ardhi kwamba tutaendelea kushirikiana na yale mapendekezo mengine yote tumeyachukua, tutayafanyia kazi.
Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, kama kuna wanachi wenye kero waleteni tu, sisi kazi ya Serikali ni kusikiliza kero za wananchi, hatutachoka. Tutafanya, hii ni kazi yetu ya kuwahudumia wananchi kama tulivyohaidi.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana.(Makofi)