Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Tarime Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa kunipatia nafasi leo ya kuchangia kwenye Kamati hizi, nami nitajikita zaidi kwenye Kamati ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa miaka ni 50 baada ya uhuru wetu tunapozungumza suala la umeme. Rafiki yangu Mheshimiwa Kalemani nampenda sana kwa sababu ni mtu msikivu, lakini tunapozungumza suala la umeme nchi hii, Watanzania waliounganishiwa umeme ni 2,800,000; yaani kwa miaka yote ambayo CCM wako madarakani wameunganishia umeme Watanzania 2,800,000. (Makofi)
SPIKA: Chanzo cha data yako Mheshimiwa.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Spika, hizi ni data za Kamati. Mimi ni Mjumbe, naomba nichangie, baadaye wataniuliza. (Kicheko)
SPIKA: Ni vizuri tuwe tunaelewana. Kaya 2,000,000 au watu 2,000,000?
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Spika, ukisema kaya, ukisema wateja, ndiyo wateja hao!
(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Spika, mimi nazungumzia wateja.
SPIKA: Kuna tofauti kubwa kati ya kaya na watu.
(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Spika, nazungumzia wateja ambao wameunganishiwa umeme na ndiyo takwimu tulizonazo. Mmeunganishia umeme wateja 2,800,000 tu.
SPIKA: Hiyo takwimu ina makosa makubwa ya kiuandishi.
MBUNGE FULANI: Ndiyo hivyo.
SPIKA: Kaya moja inaweza ikawa na watu 20 humo ndani na kila chumba kina umeme, lakini TANESCO watahesabu kwamba huyo ni mteja mmoja. Kwa hiyo ukichukulia kwamba ni watu milioni mbili kwa kweli is wrong lakini endelea. Mtunze muda wake. (Makofi)
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Spika, naomba sana muda wangu tafadhali.
SPIKA: Ninasisitiza muda tu.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Spika, hiyo ni taarifa ya Wizara kuhusu wateja waliounganishiwa umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukisema hata kaya, kwani nchi hii ina kaya ngapi? Ni nyingi tu. Ukichukua kama tuna wateja 2,800,000 na hapa hatuzungumzi kwamba tuna-shortage ya umeme. Hivi tunavyozungumza tuna excess ya umeme zaidi ya megawatt 200 na kitu au 300.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, watu wapo wanahitaji umeme na leo wakati Mheshimiwa Waziri wa Maliasili anajibu swali hapa, amezungumza kuhusu jinsi ambavyo nchi yetu misitu inakatwa kwa wingi sana, nchi inaendelea kuwa jangwa kwa sababu watu hawana nishati mbadala, wanategemea mkaa, kuni na hata Wabunge humu asilimia kubwa tunapika kwa kutumia mkaa na kuni kwa sababu hatuna umeme wa kutosha wa kupelekea watu nishati kule vijijini waache kupeleka hii nchi kuwa jangwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nafikiri huu ni mwaka wa uchaguzi na lazima mjipime kwamba kwa miaka 50 wateja 2,800,000 na umeme mnaufanya kuwa kitu cha anasa, yaani kwamba mtu akiunganishiwa umeme anaonekana yuko privileged. Watu wapo, wanahitaji umeme. Hata hili suala la kusema sijui kuna gharama ya kuunganisha umeme, hivi wewe TANESCO unafanya biashara, mtu yuko tayari umuunganishie umeme, unamuunganishia kwa gharama ya kufanyia nini? Mara sijui nunua nguzo, mara sijui; huyu si ni mteja atakulipa bili kila mwezi! Kwa nini umwambie kwamba kunahitajika gharama? (Makofi) (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, sasa haya ndiyo yanafanya tunasema CCM na Serikali yake mmeshindwa, mnapaswa kutoka madarakani waingie watu wengine ambao watapeleka umeme bure na watafikisha umeme kwa watu wengi kwa kipindi kifupi. Hilo la kwanza hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, hii nahamia kwenye masuala ya madini. Mheshimiwa Doto mwaka 2019 mwezi wa 12 mmewapa watu barua pale matongo…
SPIKA: Mheshimiwa kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Waziri.
T A A R I F A
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, napenda tu kumpa taarifa Mheshimiwa Mbunge anayezungumza, nimemsikiliza kwa makini sana kuhusiana na takwimu anazozitoa ambazo tunaamini zinaweza kupokelewa na wananchi zisieleweke vema.
Mheshimiwa Spika, kwanza ni kweli unapohesabu wateja haulinganishi na idadi ya watu, hilo ni jambo la kwanza. Unaweza ukawa na mteja mmoja lakini umeme unaotumiwa na watu katika mteja huyo mmoja wakawa 100 au 200. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hiyo taarifa ikae vizuri kwamba tunapozungumza wateja hatulinganishi na idadi ya watu. Hilo ni jambo la kwanza. Jambo la pili, access ya umeme kwa sasa mijini umeongezeka kutoka asilimia 97 mwaka 2015 hadi 92.2 mijini na umeongezeka kutoka asilimia 49.5 vijijini hadi asilimia 72.5. Hii ni access ya kutumia umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ili kuweka kumbukumbu pia vizuri kwamba Serikali pamoja na hayo; na pamoja na umeme wa access unaobaki wa zaidi ya Megawatt 280 siyo kwamba Serikali haiendelei kujaziliza ule umeme mwingine, tunaendelea kuzalisha umeme na ndiyo tumeanza na mradi mkubwa wa Julius Nyerere wa megawatt 2,215 ili kufanya sasa umeme nchini kuwa wa uhakika ili wananchi waweze kufanya shughuli za kiuchumi kwa ajili ya shughuli za viwanda.
Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Spika, amechukua dakika mbili uniangalizie…
SPIKA: Aah dakika zako nazitunza kabisa.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
SPIKA: Anakusahihisha tu kwamba umewahi kusoma takwimu huko nyuma, yaani ukaelewa statistics? Endelea kuchangia Mheshimiwa.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Spika, Mawaziri wakianza kujibu sasa hivi sijui watafanya kazi gani mwishoni wakija ku-respond! (Makofi)
SPIKA: Anaweka sawa sawa hesabu yako.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Spika, kwani amezungumza nini tofauti na nilichosema?
MHE. ESTHER N. MATIKO: Eti!
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Spika, amesema kuna wateja 2,800,000…
SPIKA: Amesema kwamba unaweza … Amesema kwamba …
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Spika, wateja 2,800,000 miaka 50 …
SPIKA: Subiri kidogo …
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Aje Waziri!
SPIKA: Amesema unaweza ukawa na mteja mmoja ana kiwanda lakini ana watu 500 ameajiri ndani ya kiwanda kile. (Makofi)
Kwa hiyo, ukimchukua huyo mteja kama ni mmoja na ukalinganisha na idadi ya watu, ulinganisho huo siyo sahihi.
(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Spika, naomba niendee, Watanzania watasikia. Wateja 2,800,000. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimemwomba Mheshimiwa Doto, watu wa Matombo mmewaandikia barua na sasa hivi Serikali ina hisa kwenye Barrick, mmewazuia kuendeleza maeneo yao, watu wanashindwa kuzika ndugu zao pale kwenye maeneo yao kwa sababu wakizika baadaye mtasumbuana.
Mheshimiwa Spika, wanashindwa kuendeleza nyumba zao tangu mwaka jana, 2019. Naomba muwalipe wale watu, msitengeneze mgogoro mwingine kama ile iliyokuwa inatengenezwa baadaye mnawaita tegesha. Lipeni wale watu tafadhali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, mwaka 2017 iliundwa Kamati ya Mruma na Mheshimiwa Rais. Kamati ikaenda kuchunguza baada ya makontena kukamatwa kwamba yalikuwa yanasafirisha madini yetu, wana-under revalue wanatoa gharama ya chini kuliko ambacho walikuwa wanauza na kupata mwaka 2017.
Mheshimiwa Spika, baadaye ikaundwa Kamati ya Osoro ikiwa na wanasheria na wachumi kwenda kuangalia gharama halisi ya madini yaliyokuwa mle. Tukaambiwa baadhi ya madini ni ya thamani mno hata ambayo tulikuwa hatujawahi kuambiwa hapa na ikasemekana kwamba kwa miaka yote Barrick wametorosha, wamekwepa kodi dola bilioni 190 ambazo ni sawa sawa na shilingi tririoni 400 na kitu.
Mheshimiwa Spika, TRA wakafanya assessment wakathibitisha Kamati ya Osoro ilichokisema kwamba kumetoroshwa shilingi trilioni 420 na hiyo ikapelekea kuletwa sheria nyingi, baadaye nitazizungumza hapa. Sheria mbili; Sheria ya Permanent Sovereignty of Natural Resources na nyingine.
Mheshimiwa Spika, naanza na shilingi trilioni 426 tulizoambiwa. Juzi ambapo Mheshimiwa Rais alikuwa anasaini mikataba tisa walikuwa wanaingia agreement na Barrick, hatujasikia popote wanazungumza kuhusu shilingi trilioni 426. Sasa nataka wanijibu, hizo fedha mmezisamehe? Mmesamehe mabeberu shilingi trilioni 426 za Watanzania? Je, kama hamjasamehe, hiyo Kamati ya akina Mheshimiwa Kabudi iliyokuwa inafanya majadiliano, ina mamlaka hayo. Kwa sababu Sheria ya TRA Kifungu cha 14 kinasema, kama assessment imeshafanyika, hamwezi tena kufuta hiyo assessment mpaka Bodi ya TRA ikae na Waziri a- gazette. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Heche nakukumbusha tu, siyo wewe peke yako na wachangiaji wengine; ni vizuri sana kuzijua taratibu za Kibunge. Taarifa iliyoko mezani, aliyetoa hoja ni Mwenyekiti wa Kamati. Sasa baadhi ya michango: Je, huyo Mwenyekiti wa Kamati ndiye aliyeingia huo mkataba? Yaani kweli Mwenyekiti atakuja kujibu haya maswali unayosema au ni kitu gani? Kwa sababu hoja hii siyo ya Waziri, ni hoja ya Mwenyekiti wa Kamati kuhusiana na kazi za Kamati za mwaka mzima. (Makofi)
Kwa hiyo, tunapochangia hapa, tuwe tunaelewa hoja hizi tunazielekeza kwa nani. Kwa hiyo, nikumbushe tu, hoja hizi mbili tunapokuwa tunachangia tunazielekeza kwa Mwenyekiti wa Kamati, tunaishauri Kamati, tunalishauri Bunge na Serikali pia. Kwa hiyo, nilitaka tu kuweka hilo vizuri.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana…
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, naye ni mjumbe wa Kamati…
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Spika, najua Mawaziri wanapata muda wa kuchangia...
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mpaka dakika 20, 30...
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Spika, mpaka dakika 20, 30 Mheshimiwa Mkuchika alifanya hivyo jana hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati, haya ni mawazo ambayo nilitoa kwa sababu unajua wingi wetu mle kwenye Kamati. Kwa hiyo, naomba nichangie.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunahitaji majibu kuhusu hilo, kwamba shilingi trilioni 426 sita ziko wapi? Zimesamehewa au hazijasamehewa?
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, kuna kitu kinaitwa kishika uchumba, dola milioni mia tatu zaidi ya shilingi bilioni 600 na kitu, hizo mlisema kwamba zitalipwa na mabeberu haraka sana kabla ya mjadala. Hizo shilingi bilioni 600 Serikali imekubali sasa kwamba walipwe kwa installment kwa kipindi cha miaka saba na ukiangalia zaidi ya shilingi bilioni 240 zinakwenda kwenye VAT, refund hakuna cash yoyote inayoingia kwenye Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nauliza, wale wazalendo waliokuwa wanapiga vigelegele kwanza walipaswa waone aibu hapa kwa sababu walichokuwa wanasema hakipo na hakijapatikana. (Makofi)
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Wazalendo bandia hao!
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Spika, jambo la tatu, smelter. Tuliambiwa…
SPIKA: Ushakula nusu ya muda, sasa chunga huko unakoenda.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, tuliambiwa na sheria ikatungwa kwamba kuanzia sasa madini yote ghafi hayatasafirishwa nje ya nchi, smelter itajengwa hapa hapa na madini yatachakatwa hapa hapa ili tuyape value ndiyo yasafirishwe.
Mheshimiwa Spika, hiyo smelter iko wapi? Tunataka mtujibu hiyo smelter mmejenga wai?
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Taarifa.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba Mheshimiwa Heche ambaye ni Mjumbe wa Kamati anafahamu kila kitu kinachoendelea, kwa sababu amekuwa akiuliza maswali kwenye Kamati, mimi najua nia yake ni pamoja na kunogesha, na kuweza kupata fursa ya kusema. Nataka nimweleza kwamba smelter anayozungumza si kama kujenga kibanda, ni teknolojia kubwa ambayo ukishatoa leseni ujenzi wake hauhitaji wiki mbili au mwezi mmoja. Minimum requement ya time ya kujenga smelter moja kwa watalamu wote walikuja duniani kupresent Wizara ya Madini ni miezi 24. Sisi tumeshatoa leseni yakujenga smelter pamoja na kujenga refinery. Sasa kama tunataka kuzungumza kwa sababu tu tumeamua kuzungumza; mimi nataka Mheshimiwa Heche ajielekeze kwenye haya mambo kwa kusema ukweli walau kwasababu anaufahamu ukweli wenyewe.
MBUNGE FULANI: Mwongo huyo.
SPIKA: Ni ushauri huo ummepewa.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Spika, miezi 24 nafikiri tangu mwaka 2017 imeshapita sasa hivi tunaelekea miezi 26 na kitu. Mimi nichozungumza, kama smelter inajengwa hapa kwa nini juzi mnasema kwamba makontena yatafute mteja yasafirishwe? Kwanini msisubiri mpaka smelter yetu ijengwe makontena yote yale 117 yabaki Tanzania? Kama mnajenga smelter? Ilhali sheria iliyotungwa humu Bungeni kifungu cha 11 ilisema wazi kabisa, sheria, kwamba itakuwa ni marufuku kusafirisha madini nje ya nchi na juzi Rais amesema wateja watafutwe na madini yasafirishwe? Kwanini mnafanya hivyo wakati mnajua mnajenga smelter mnaijenga?...
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
MHE. JOHN W. HECHE:… No! no! no!
T A A R I F A
SPIKA: Mheshimiwa Waziri, Dotto Biteko, nimekuona.
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza sifurahi kujibizana hivi, lakini ikitokea uongo unasemwa hadharani inanisumbua. Nataka nieleze ni kweli sheria ya madini imezuia kusafirisha madini ghafi nje ya nchi, sheria hiyo hiyo kifungu cha 59 kimetoa mamlaka kwa Waziri wa Madini kutengeneza kanuni ya kusafirisha madini yaliyoongezwa thamani kwa kiwango fulani. Kanuni hiyo imechapishwa kwenye gazeti la serikali na kanuni hiyo hiyo imetoa kipindi cha mpito wakati hatujawa na hizo facility kuwe na utaratibu maalumu wa biashara hizo kuendelea, ndio maana biashara zinaendelea kufanyika ndani ya nchi. Ingekuwa ni sheria inayozungumza leo marufuku kesho tungekuwa tunazunguza habari nyingine. Mheshimiwa Heche na sheria hizo anazifahamu ninaomba azungumze kwa kusema ukweli. (Makofi)
SPIKA: Ndiyo maana siku moja niliwahi kuzungumza humu ndani kwamba hili neno upinzani lile neno lina shida, kwamba ni vizuri tukafikia mahala pa kuwa na ushindani badala ya upinzani. Kwa sababu upinzani hata kitu ambacho anakijua fika lazima apinge kwa kupotosha.
Kwa hiyo mnapokuwa ninyi ndio wajumbe wa Kamati ambao mmekaa huko mwaka mzima, Mheshimiwa Heche na wewe ukiwa mjumbe wa Kamati halafu mnatoka baada ya mwaka mnatupotosha sisi ambayo hatukuwa wajumbe wa Kamati sasa where we are going to? Itakuwa ni jambo lisilofaa hata kidogo. Lakini endelea tu, malizia dakika zako.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Spika, mimi nasikitika kwamba sheria ya kifungu cha 11 inaweza kufutwa na kanuni ya Waziri hivi hiyo ya wapi hiyo? Unaojua tunaozungumza huku sio kwamba hatuna akili tunajua hivi vitu tuna akili timamu. Wala hatupigi makofi sisi, tunazungumza jambo mlilolileta hapa na sisi tukawaambia na Lissu akawambia hamtapa hata mbuni iko wapi mbuni mliyopata hapa iko wapi kati ya tirion 400 mlizoandika tukawa laughing stock huko duniani; ipo wapi mbuni moja mliyopata muwaambie watanzania hapa. Sasa mnakuja kama kawaida mnayumba kama upepe kama kesho mpo huku mnapiga makofi tu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tulisema hapa, kwamba mlitunga nyie wazalendo mkasema ninyi you’re a sovereign country; kwamba hakuna kesi itakayokwenda kufanyika nje ya nchi, mlisema humu ninyi wenyewe, tukawaambia nyie mmesaini mikataba mmesaini MIGA na hamtaweza ninyi. Sasa hivi mmeleta Sheria ya Arbitration Act mnakuja kuondoa, mmeruhusu na wamewapa Barrick waiver ya kwenda kutushitaki popote wanapotaka. Sasa hayo mambo Heche akisema kwamba...
SPIKA: Hivi unajua kuna Waheshimiwa Wabunge nawatafuta siwaoni. Mheshimiwa Mwita Waitara yupo wapi leo? Samahani Mheshimiwa Heche endelea bwana. (Makofi/Kicheko)
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Spika, mimi chuma usinione hivi. Unajua wazungu wamekwenda mwezini wamerudi, sisi Waafrika bado tupo kijiji hata aliyeko mjini mawazo yake yapo kijiji vilevile. Sisi tunachozungumza hapa ni mambo tuliyojadili humu; kwamba tulikuja hapa tukatamba tukawatangazia Watanzania.
Mimi nilitegemea juzi mnaposaini mikataba msimame pale pale muwaambie Watanzania eeeh! Trilioni 420 hizi hapa noah kila mtu apate. Sasa mmekosa mpaka kishika uchumba, kishika uchumba mmekosa. Sheria ambazo mlituambia you’re a sovereign country hamuingiliwi mmekwenda kupiga magoti kwa mabeberu mmerudisha sheria humu kuja kuzibadilisha. Nilitegemea Wabunge wengi wa CCM, ambao ndio wengi, muone aibu kwa sababu nyie mliyumba kipindi kile. We told you, tuliwaambia hapa, mkasema oooh sisi tunatumiwa na mabeberu. Sasa sisi na nyie nani anatumiwa na mabeberu?... (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Mheshimiwa Heche muda wako umeisha.