Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati Kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

Hon. Mariamu Ditopile Mzuzuri

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati Kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa hii ya kuweza kuchangia kwenye taarifa ya Kamati hizi mbili. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu aliotujalia afya na uzima kuweza kukaa kwenye kikao hiki leo.

Mheshimiwa Spika, mimi ni mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini lakini pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati. Kwa hiyo nipende kumshukuru sana na kumpongeza Mwenyekiti wetu wa Kamati Mheshimiwa Kitandula kwa uongozi wake mahiri na kutuongoza vema. Tunamuombea afya na uzima ili aendelee katika majukumu yake. Pia nipende kuwashukuru sana wajumbe wa kamati hasa wale wanashiriki katika vikao na ziara kikamilifu; lakini pia niwatie joto wale ambao wanategatega katika kazi za kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kamati yetu inafanya kazi na wizara mbili, Wizara ya Nishati pamoja na Wizara ya Madini, nipende kuwapongeza sana sana Waheshimiwa Mawaziri wa Wizara hizi pamoja na Manaibu wake, pamoja na Makatibu Wakuu lakini bila kuwasahau wataalam wa wizara hizo. Kwa kweli wanafanya kazi kubwa katika kutafsiri maono ya Mheshimiwa Rais ya kuleta uchumi wa kati na Tanzania ya viwanda. Pia kubwa lile la kutaka sisi kujitegemea kama taifa huru. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sekta ya nishati, nirudie kuunga mkono kauli ya mchangiaji aliyepita Mheshimiwa Peter Serukamba ambaye amesema kwa uthubutu wa Viongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano kweli yanafanyika mapinduzi makubwa na ya kihistoria. Kwenye sekta ya nishati leo hii mtu anavyosema kwamba tuna umeme wa ziada, ndivyo taifa linatakiwa liwe kwa sababu ulichonacho na huku una mipango endelevu lazima uwe na ziada na uwe na mipango ya kuongeza zaidi na zaidi. Huwezi kusema ninahitaji thelathini na nina hiyo hiyo thelathini halafu ukasema wewe ni taifa linaloendelea. Kwa hiyo tunapoongea kwa sababu wamesema ooh, wateja ni hawa tu na huku tuna umeme wa ziada. Taifa lolote lenye mipango endelevu na ambalo liko katika process ya maendeleo lazima liwe na ziada. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeona mafanikio makubwa ya miradi hii ya umeme vijijini, awamu ya kwanza, awamu ya pili na sasa tuko kwenye awamu ya tatu ambayo ina mafanikio makubwa. Ilipanga kupeleka umeme kwenye vijiji 4,651; miezi 19 ya utekelezaji tayari vijiji 3,269 vimeshafikiwa na umeme ambayo ni sawa na asilimia 70 ya malengo waliyojiwekea. Wilaya ya Tarime ambayo ina majimbo mawili ina vijiji 88, kwenye vijiji 88 tayari vijiji zaidi ya 46 vina umeme, vijiji zaidi ya 26 vimeshaingia kwenye bajeti ya mwaka huu kazi zinaendelea kusimamisha nguzo na nyaya ili umeme uwake kwenye vijiji hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini katika nchi za Afrika ni takribani mataifa kama manne tu ikiwemo Nigeria ambao wanafanya process hii ya ku- electrify rural areas. Lakini kati ya yote sisi Tanzania tuko bora hata Angola wamekuja nyuma yetu wamekuja kujifunza Tanzania kufanya electrification kwenye vijiji vyao, kwa hiyo kazi inafanyika na sio kazi ndogo ni kazi kubwa kweli kweli.

Mheshimiwa Spika, zipo changamoto lakini uzuri wa viongozi wetu ni wasikivu. Tuliwaambia wigo (scope) ni mdogo ndio maana Wizara kupitia REA wakasema tulete awamu ya tatu mzunguko wa pili ili kufanya ujazilizi kwenye maeneo ambayo yamerukwarukwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zipo changamoto za vifaa kwamba hawa wakandarasi wanakuwa kidogo wana uzito katika kutekeleza majukumu na visingizio kwamba hawapati vifaa, lakini nashukuru kwa ushauri wa Kamati Serikali tumesikia juzi walikuwa na mkutano na wakandarasi kwa maana sasa wanachukua maoni yetu na kuyafanyia kazi. Bunge kazi yake ni kuisimamia na kuishauri Serikali, ukiacha kupitisha bajeti. Mafanikio mema ya Serikali ndio mafanikio yetu sisi Bunge. Sasa leo hii ukisimama kama Mbunge na kubeza mafanikio ya Serikali labda kwa vile ndio uki upande wa kukataa, lakini ukweli upo na unaonekana.

Mheshimiwa Spika, Shirika la TANESCO ni shirika la umma. Serikali hii ilipoingia madarakani Awamu ya Tano TANESCO ilikuwa ni shirika la madeni na shirika ambalo lilikuwa linaendeshwa kwa kupokea ruzuku kutoka Serikalini. Lakini leo tunavyoongea TANESCO inalipa madeni, TANESCO haipokei ruzuku, TANESCO haizalishi madeni, TANESCO inasonga mbele. Tunasema mapinduzi makubwa leo hii tuna ziada ya umeme, lakini bado Serikali hii kwa kutumia fedha za ndani ambazo Bunge hili ndio limeidhinisha tuna ujenzi wa umeme kwenye Bwawa la Rufiji la Nyerere. Kwa hiyo kwa kweli mambo ni makubwa na sisi kama Kamati/Wajumbe tuwatie moyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwenye sekta ya madini kwa kupitia sheria zile mbili za mwaka 2017 lakini pia mabadiliko ya sheria ndogo ya mwaka 2019 tujivunie, Tanzania leo hii madini ni mali ya Watanzania. Leo kuna masoko ya madini, leo kuna kipengele kwa kuanzisha Tume ya Madini, kuna kitu kinaitwa local content. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mpaka mayai, kabichi yalikuwa yanaingizwa kutoka nje ya nchi, leo mama wa kawaida pale nyumbani kwa Mheshimiwa Spika anauza mayai mgodini. Sasa kama hatutofurahi kuona kwamba haya manufaa yanashuka kwa wananchi wa chini tunalipenda Taifa letu, utabeza mambo yote haya ambayo yanamgusa mpaka Mtanzania wa kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii kule Geita inajenga refinery ambayo itaenda kutalisha haijawahi kutokea kwenye historia ya nchi. Kwanza hiyo refinery Afrika Mashariki ndio itakuwa ambayo ni modern kuliko zote, itaweza ku-process zaidi ya tani 100 ya dhahabu kwa mwaka. Dhahabu yote inayozalishwa Kanda ya Ziwa itakuwa inapandishwa thamani pale. Mambo ni makubwa nan i mengi lakini tumeona mapato, Mheshimiwa Rais alisema hatutaki sisi ndio haya mambo sasa hivi tunapiga watu wa Marekani. Wewe Marekani umemzuia sisi Mkuu wa Mkoa wetu ni mtu mkubwa, yule ni president appointee, sasa leo unamzuia asiingie nchini kwako na sisi tusijibu kisa wanatupa hela za msaada ndio maana tunataka kujitegemea ili mtu anapotoa kisu na sisi tunatoa panga msichukue tafsiri nyingine nimetumia mfano maana kwa kunani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii tuna shirika la Twiga Mining Company hayo siyo mafanikio? Kweli hatuendi kwenye uchumi wa kati. Leo hii Tanzanite kwa ujenzi wa ukuta ilikuwa inapatikana Tanzanite kilo 147.7 leo tunapata kilo 949; mapato kwenye madini yametoka kutoka bilioni 196 mwaka 2016 mpaka bilioni 310 inachangia katika pato la Taifa utasema mambo hayajafanyika! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huwezi kujua umuhimu wa hivi vitu kama hujatoka nje ya mipaka ya Tanzania. Ulinipa heshima kwenda kushiriki round table ya viongozi wa nchi wa SADC kwenda kutoa maoni namna gani ya kubadilisha policies na sheria ili kuboresha extractive industry iweze kutufaidisha sisi kama wazawa, kila nchi ilikuwa ina-present mawazo, Tanzania tulikuwa ni nchi mfano, a model country. Walisubiri sisi tuwasilishe ili wao waweze kupata dondoo. Nakushukuru na ahsante. (Makofi)