Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii

Hon. Prof. Jumanne Abdallah Maghembe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii

MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Kwanza naunga mkono hoja ambazo ziko mezani. Napenda sana kuzipongeza hizi Wizara ambazo tunazijadili hapa moja kwa moja na kuzilenga Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Wizara ya Afya. Kwa kweli wanafanya kazi nzuri sana na tuwapongeze wenzetu kwa sababu wanatumia muda mrefu na wanafanya kazi kubwa ambapo ni vizuri mtu akifanya vizuri tumwambie hongera, apate moyo zaidi wa kufanya vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, muda siyo rafiki sana, nitaongea na kukumbusha hapa Kamati zetu kwamba kwa miaka miwili hapa nimekuwa naongea na kupongeza juu elimu jinsi ambavyo inapata pesa nyingi. Nimesikia mtu mmoja anasema pesa hizo hazitoshi. Haziwezi kuja kutosha hata siku moja, lakini fedha ambazo zinatengwa na Serikali shilingi trilioni 4.4 ni sawa sawa dola bilioni 2.2. Dola bilioni 2.2 kwenye elimu peke yake, hebu angalieni nchi za Afrika, nchi ambayo inatumia dola bilioni mbili katika kutoa elimu ya watoto wake, ziko chache kweli kweli! Kwa hiyo, tuipongeze Serikali ya Tanzania kwa kazi nzuri hii ambayo inafanywa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kazi hiyo nzuri, napenda kukumbusha, bado kule Mwanga tuna walimu wachache sana. Walimu wa Shule za Msingi kule Mwanga ni wachache kweli kweli! Wastani wa walimu kwenye shule zetu za msingi kule Mwanga ni walimu wawili au watatu. Tuna madarasa nane kwenye shule moja ya msingi. Kwa hiyo, walimu watatu wakiingia kwenye madarasa matatu, watoto wengine waliobaki kwenye madarasa matano, wanaendesha soko huko na kucheza darasani. Kwa hiyo, kuomba tupate walimu zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda niseme pia kwamba kwa kweli Wizara ya Afya pamoja na kuipongeza, niipongeze tena, wamejenga Vituo vya Afya zaidi ya 300 katika kipindi kifupi hiki, wanastahili kupongezwa. Katika kazi hizi nzuri na watu tuko milioni 55 huwezi kudhani kwamba itakuwa kama maua, haiwezekani. Kutakuwa na shida shida kama hizi za wazee na hizi shida tutaendelea kuzitatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuendelee kuungana pamoja kama Wabunge na Serikali yetu tusaidie kutatua haya matatizo. Napenda nikumbushe kwamba huko nyuma tulikuwa tunajenga Vituo vya Afya sisi wenyewe; wananchi wenyewe na Serikali inatusaidia. Tunajenga Zahanati na Serikali inatusaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kule kwenye Wilaya yangu ya Mwanga nina Vituo vya Afya vitatu ambavyo vimejengwa na karibu vimekwisha na vimejengwa na wananchi njia ya msaragambo. Hivi vituo tunaiomba Serikali na sasa wakati huu ndiyo mnapanga bajeti, mtusaidie kuvimaliza ili vile sawa sawa na hivi ambavyo vimeletwa na Serikali na kupigwa mara moja na kumalizika; sasa vile ambavyo wananchi wamejenga karibu wanamaliza na nguvu zao zimetumika kiasi kikubwa sana, basi mtusaidie kuvimaliza. Tuna Kituo cha Afya cha Kileo na Kitu cha Afya cha Mwaniko ambavyo tunaomba Serikali itusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, tuna Zahanati sita ambazo tunaomba mtusaidie. Zahanati ya Kituri imekamilika na wananchi wamefanya juhudi kubwa, wamepaua na wamemalizia almost complete, lakini nasikia wametumia mabati gauge 30 na Injinia wa Wilaya anasema wang‟oe mabati. Sasa nafikiri kwamba jambo hili tulifikishe kwenye Wizara ya Afya. Maana hata kama wananchi walikuwa hawana mabati, wana nyasi peke yake, basi wamejenga kituo chao ndiyo hicho, waruhusiwe kukitumia, wasiambiwe wang‟oe mabati kwa sababu ni nyumba ya Serikali. Nyumba ya Serikali ingeng‟oa mabati kama Serikali ingeleta hayo mabati mengine. Kwa hiyo, tunaomba wananchi wasaidiwe Zahanati ifunguliwe mapema, maana wametumia fedha nyingi sana kuijenga.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna zahanati pia Lembeni, Mlingeni, Vanua kule Ndorwe, Buchama, Ndambwe na Kitoghoto ambapo Zahanati hizo karibu zimekamilika, lakini wananchi wanahitaji msaada kidogo tu wa Serikali ili waweze kuzitumia Zahanati hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, napenda nitoe mapendekezo hapa kwamba jamani tuna Shule za Sekondari sasa zinatosha, watoto wetu wa kutoka Shule za Msingi karibu wote niseme, wabaweza kwenda Sekondari, lakini kuna tatizo kubwa kwenye Sekondari zote hizi. Ni Sekondari chache tu ambazo wananchi wamemaliza ujenzi wa maabara. Ina maana kwamba wanafunzi wetu wanajifunza sayansi kwa nadharia tu, hakuna mahali ambapo wanajifunza physics kwa kufanya practical; hakuna mahali wanajifunza biolojia kwa kufanya practical; na hakuna mahali wanajifunza kemia kwa kufanya practical.

Mheshimiwa Naibu Spika, kujenga maabara siyo kitu rahisi na kuwapa wananchi wa vijijini kazi ya kujenga maabara na hawajui maabara maana yake ni nini, ni kutaka vitu vingi sana kutoka kwa wananchi wa vijijini. Tunaomba sana jamani, katika bajeti hii inayokuja, Serikali itenge angalau shilingi bilioni 200 imalize hizi maabara zote ili watoto wetu wa shule hizi za Kata waweze kufaulu mtihani wa Form Four kama wale ambao wanasoma kwenye shule za private, kwa sababu watoto wetu hawa wanafanya sayansi kinadharia.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo nataka nimalize nalo...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Profesa, ahsante sana.

MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Ooh, my goodness!

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)