Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii

Hon. Deogratias Francis Ngalawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ludewa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii

MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia mjadala huu unaoendelea wa Kamati za Huduma ya Maendeleo ya Jamii pamoja na Kamati ya Ukimwi. Kwanza kabisa, napenda kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa na nzuri ambayo inaendelea kuifanya. Tumeona Vituo vya Afya vingi vikijengwa, tumeona Hospitali zikijengwa na tumeona Zahanati zikijengwa. Kwa kweli mambo yanaenda vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nijikite kwenye eneo la kinga. Tuna tiba na kinga. Ukiangalia Wizara ya Afya imejikita sana kwenye eneo la kitabibu, lakini ni Wizara hii ambayo inashughulika pia na kinga. Kwa hiyo, napenda sasa kuishauri Serikali, ifike mahala tuweke concentration kubwa kwenye maeneo ya kinga ambayo yatazuia gharama kubwa kutumika katika maeneo ambayo ni ya tiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo mifano ya nchi kama Rwanda ambako tumeenda. Wapo Maafisa Maendeleo ya Jamii ambao kazi yao kubwa ni kuelimisha watu wale vyakula vya namna gani kwa maana ya lishe na kutoa elimu mbalimbali za kinga dhidi ya mimba, dhidi ya ujauzito na maeneo mbalimbali. Kwa hiyo, naamini kwamba tukijikita kwa kiasi kikubwa kwenye kinga, tutaokoa gharama kubwa zinazotumika maeneo ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumshukuru na kumpongeza Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu pamoja na Naibu wake, Mheshimiwa Dkt. Ndugulile; wametengeneza concentration kubwa kwenye hivyo vitu. Sasa naomba nguvu ile ile ambayo imetumika sana kwenye afya, tumeona Serikali ikiwa imeokoa hela nyingi sana za kupeleka wagonjwa nje ya nchi, kutoka 600 mpaka watu 50 kwenda nje, siyo jambo dogo. Hilo ni jambo kubwa sana nami nasema kwamba endeleeni kukomaa kwenye hilo ili mwisho wa siku ikiwezekana tupeleke watu sifuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nawapongeza, kazi mnayoifanya ni kubwa na Watanzania wanaiona. Pia tuwaimarishe watumishi wa ya Maendeleo ya Jamii ili waweze kutoa huduma kule vijijini ya namna ya Lishe na namna ya kujikinga na magonjwa mbalimbali ili tuweze kuokoa gharama kubwa inayotumika kwenye afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna masuala ya maboma ya Vituo vya Afya, Zahanati na Shule. Maeneo mengi ya Majimbo ambako tunatoka, wananchi wametumia nguvu zao nyingi na kubwa katika kuhakikisha kwamba wanaisaidia Serikali yao kujenga Zahanati na Vituo vya Afya. Sasa umeshafika wakati wa Serikali angalau kuwasaidia hawa wananchi kwa ajili ya kuezeka na baadaye kukamilisha. Wananchi wetu wakielimishwa wala hawana shida yoyote. Ludewa ninakotoka kuna zaidi ya maboma ya Vituo vya Afya 14 na mengine yameshaezekwa kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa hiyo, kinachoitajika tu pale ni kuwa-support ili kuweza kumalizia na baada ya hapo, utekelezaji wa Ilani wa Chama cha Mapinduzi kwamba Kila Kijiji kiwe na Zahanati na Kila Kata iwe na Kituo cha Afya, tutakuwa tumetekeleza kwa kiasi kikubwa sana, zaidi ya asilimia 90.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado tunajenga shule nyingi, kwa sababu tumeshasema kwenye kila kijiji tunatakiwa shule. Kwa hiyo, nadhani kuwekwe mpango madhubuti wa timu maalum ya kwenda kupitia maeneo hayo, yaje na taarifa ili tuweze kupata takwimu sahihi za kuweza kusaidia hiyo kitu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naamini kwamba Mheshimiwa Waziri na Watendaji huko Serikalini wana uwezo wa kuifanya hiyo kazi na mwisho wa siku tukaitekeleza ilani kwa asilimia 100, hiyo inawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la uhaba na watumishi kwenye maeneo ya afya. Uhaba huu umekuwa ni mkubwa sana. Kama wenzangu walivyokuwa wamezungumza huko mwanzo, ile hali ya uzalendo ni kama imepungua. Sasa tujiulieze, imepungua kwa kiasi gani, hasa wale watu kwenda kujitolea? Wasomi wetu wanaomaliza sasa hivi wengi wapo mitaani, lakini bado tunalalamika tuna uhaba wa walimu na watumishi wa afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani ifanyike program maalum ya kuhakikisha kwamba watu wanajitolea na wale wanaojitolea ndiyo wawe wa kwanza kuajiriwa. Kwa sababu wapo watu ambao wanajitolea, nafasi za kazi zinatangazwa, lakini wale wanaojitolea wanaachwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nadhani tungetengeneza utaratibu mzuri kwamba wale wanaojitolea, basi ndiyo wawe wa kwanza kuajiriwa kwa sababu wameonyesha uzalendo wa moja kwa moja kuanza kazi mwaka wa kwanza, miaka miwili, lakini kazi inapotangazwa, wanaachwa. Nadhani siyo jambo sahihi, maadam tu wana zile sifa ambazo zinahitajika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunao watu wanaoitwa uthibiti ubora. Kuna malalamiko makubwa sana kwenye uthibiti ubora hasa wa elimu. Zamani hawa watu tulikuwa tunawaita Wakaguzi. Hawa watu wanaoenda kukagua shule, maana yake wanakagua shule; na ile kazi ni kubwa. Ukijaribu kuangalia kwenye level ya wilaya, yuko Mthibiti Ubora Mkuu wa Wilaya na wapo Maafisa Elimu. Hawa watu bado wanalalamikia masuala ya nyongeza, zile fedha za nafasi; wanaita fedha za nafasi, kitu cha namna hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri Serikali ingejaribu kuangalia uwezekano wa hawa watu, yale malalamiko ambayo wanasema kwamba wanaonekana kama ni second class, yaondoke ili waweze kuwa sawa na wenzao na waweze kufanya kazi zile kiufanisi. Kwa sababu kazi wanayoifanya ni kubwa, kuna uhaba mkubwa wa magari, kuna uhaba mkubwa wa vifaa na umbali wa maeneo wanayokwenda. Kwa hiyo, wanajikuta kwamba wanafanya kazi kubwa na ambayo kwa kweli wanahitaji kupewa msaada.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na ahsante kwa nafasi na ninaunga mkono hoja zote zilizotolewa hapa na Wenyeviti wote wa Kamati, ahsante. (Makofi)