Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ngorongoro
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia hoja za Kamati zote mbili. Naomba nianze kwanza kwa kuwapongeza sana Waheshimiwa Wenyeviti wa Kamati zote mbili pamoja na Wajumbe wao kwa kuwasilisha ripoti nzuri. Niseme mapema kabisa kwamba tunapokea ushauri wote ambao wameutoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niruhusu niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamechangia Hoja za Kamati zote mbili na kutoa ushauri, nao pia napenda niwafahamishe kwamba Wizara yangu itachukua ushauri wote na kuufanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya machache, napenda kutoa ufafanuzi kuhusu masuala machache ambayo yameibuliwa katika mjadala. La kwanza kabisa, Kamati ya UKIMWI imetushauri Wizara ya Elimu, Sayansi na Technolojia kujenga mabweni mengi zaidi kama moja ya njia za kuwasaidia watoto wa kike wasiweze kupata maambukizi ya UKIMWI. Napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa, kati ya mwaka 2016 hadi mwaka huu, Serikali imejenga mabweni 333 na tunaendelea kujenga mengine ikiwa ni sehemu ya kuwasaidia watoto wa kike waweze kusoma bila kuwepo na changamoto zozote.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati yangu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imetushauri na imezungumza kwa mapana na marefu pamoja na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge kuhusu kushuka kwa Bajeti ya Sekta ya Elimu. Takwimu ambazo zipo zikitafsiriwa vibaya zinaweza zikaonesha kwamba bajeti ya elimu imeshuka katika miaka ya hivi karibuni, lakini bajeti ikisomwa katika muktadha sahihi ukweli wa mambo ni kwamba bajeti imeongezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, Bajeti ya Wizara ya Sekta ya Elimu kwa sasa ni bajeti ambayo ni halisia na imejikita katika mahitaji halisi ya Watanzania katika Sekta ya Elimu. Baadhi ya bajeti za huko nyuma zilikuwa zimejaa makokoro mengi, huko ndiko kulikuwa na fedha za kusafiri kiholela kwenda nje, fedha za mikutano na warsha ambazo hazina tija, fedha za chai ambazo hazisaidii chochote na fedha ambazo zimewekwa ajili ya upigaji. Kwa hiyo, kilichofanyika ni kwamba bajeti ile imetengenezwa katika uhalisia na hivyo kuweza kukidhi mahitaji halisi ya Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata katika kuangalia tu bajeti yenyewe, bajeti ya Sekta ya Elimu haiwezi ikawa imeshuka kwa sababu kuanzia mwaka 2016 Serikali inatekeleza Mpango wa Elimu bila Malipo. Mpango ambao Serikali inatumia shilingi bilioni 23.85 kwa mwezi. Kwa hiyo, katika miaka minne tu pekee Serikali imetumia zaidi ya shilingi trilioni moja kwenye item moja ya elimu bila malipo. Katika hali ya kawaida haiwezekani bajeti ambayo ina ingizo jipya la shilingi trilioni moja ikaonekana kwamba imeshuka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia hata tukiangalia baadhi ya matumizi mengine ya kawaida; mwaka 2015/2016, bajeti ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ilikuwa ni shilingi za Kitanzania bilioni 327. Leo hii tunavyozungumza, ni shilingi bilioni 450. Kwa hiyo, kuna ongezeko la karibia shilingi bilioni 100. Kwa hiyo, ukiangalia tu items hizo mbili, kwa vyovyote vile siyo uhalisia tukizungumza kwamba bajeti imeshuka. Kilichofanyika ni kwamba tumefanya realistic budgeting na kujaribu kubana matumizi na kuondoa matumizi ambayo hayana msingi, huku tukiongeza fedha kwa ajili ya maeneo ambayo ni ya kipaumbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nilitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba kiuhalisia bajeti ya Sekta ya Elimu imeongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati yangu pamoja na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wamependekeza kwamba wigo wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu upanuliwe ili wanafunzi wanaosoma katika vyuo vya kati au vyuo vya NACTE nao waweze kunufaika. Wizara yangu inabeba mapendekezo haya, lakini nataka nitoe taarifa tu, ifahamike kwamba pamoja na kwamba kwa sasa inaweza ikaonekana kwamba wanafunzi wa vyuo vya kati hasa vyuo vya ufundi wanalipa gharama au wanalipa tuition kuweza kuingia kwenye vyuo hivyo, hali halisi ni kwamba kwa kweli wanalipa token na bado gharama nyingine zote zinabebwa na Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, mwanafunzi anayesoma kwenye Chuo cha Ufundi kwa mfano Arusha Technical College, analipa ada ya kama shilingi 140,000/=, lakini akienda kwenye mazoezi ya viwandani, Serikali inampa shilingi 500,000/=.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, unaweza ukaona. Bado malazi yake, chakula na gharama nyingine zinabebwa na Serikali. Kwa hiyo, hata kama hawapati mikopo, lakini siyo kwamba Serikali haiwasaidii kusoma. Kwa hiyo, bado Serikali inabeba jukumu la kuhakikisha kwamba vijana hawa wa vyuo vya ufundi na vyuo vya kati nao wananufaika na msaada wa elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na pendekezo vilevile ambalo limetolewa la kuboresha vyuo vya ufundi kwa ujumla wake na kufanya maboresho ya sera na sheria. Pendekezo hili limepokelewa, lakini naomba tu nitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba Wizara imechukua jitihada kadha wa kadha kuhakikisha kwamba tunaboresha elimu ya ufundi. Kwa wale ambao wameenda kwa mfano kwenye, Chuo cha Ufundi Arusha hivi karibuni, ukifika pale Serikali imeweza kuweka vifaa vya kisasa kwenye karakana, vyenye thamani ya shilingi bilioni 15; na ni vifaa ambavyo havipatikana katika nchi nyingine yoyote ya Afrika isipokuwa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiacha hilo, Serikali sasa imeanza ujenzi wa chuo kipya cha ufundi cha Dodoma, ambacho kitakuwa na hadhi sawa na DIT na Arusha Technical College. Wote ni mashahidi kwamba Serikali kwa sasa inajenga vyuo 46 vipya vya wilaya na vya mikoa vya VETA. Nina hakika Waheshimiwa Wabunge nyie wenyewe ni wanufaika. Serikali imetenga shilingi bilioni 100 na ujenzi uko katika hatua mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia wote ni mashahidi, Serikali imefanyia ukarabati mkubwa vyuo 54 vya wananchi vya FDCs ili viweze kuwa katika hali bora zaidi. Kama vile haitoshi, Serikali imejipanga kununua vifaa vya vyuo hivi vya ufundi vyenye thamani ya shilingi bilioni 26 kimsingi ili elimu yetu ya ufundi iwe ya kisasa kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati yangu imependekeza iundwe Tume ya Elimu ili kuweza kupendekeza namna ya kuboresha elimu. Naomba nilitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa kwa sasa Wizara imeanzisha mkakati wa kuhuisha Sera ya Elimu. Kwa hiyo, tunategemea kwamba Waheshimiwa Wabunge pamoja na Watanzania wengine watahusishwa katika zoezi hilo. Kwa hiyo, naomba mshiriki kikamilifu ili muweze kutoa mawazo ya namna gani ya kuboresha elimu yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa lakini siyo kwa umuhimu, kulikuwa na hoja kwamba shule za binafsi haziwezi kupata vitabu kutoka taasisi ya elimu. Naomba nilitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba shule binafsi zinaweza zikapata vitabu kwa kununua kwenye maduka maalum ambayo yako kila mkoa. Kwa hiyo, naomba niwafahamishe kwamba inawezekana kabisa kupata vitabu vile na vyenyewe vya kwao havijaandikwa kwamba haviuzwi. Vile ambavyo vimeandikwa “haviuzwi” ni vile ambavyo vinatolewa kwenye Shule za Umma; lakini kila mkoa kuna duka mahususi ambalo Taasisi ya Elimu Tanzania imetenga kwa ajili ya kuuza vitabu kwa shule binafsi.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya machache, napenda kuunga mkono hoja. (Makofi)