Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Tanga Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nianze kwa kuzipongeza Kamati zetu mbili; Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii inayoongozwa na Mheshimiwa Peter Serukamba na Kamati ya UKIMWI na Madawa ya
Kulevya inayoongozwa na Mheshimiwa Oscar Mukasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba tumepokea maoni na ushauri wa kamati na pia ushauri wa Waheshimiwa Wabunge katika michango yao, lengo letu likiwa ni kuhakikisha kwamba wananchi wanakuwa na afya bora ili kuwawezesha kushiriki katika ujenzi wa Tanzania ya viwanda lakini pia katika kuboresha maisha yao. Kwa kweli tunazipongeza Kamati, wametoa maoni na ushauri mkubwa na kamati hizi zimekuwa msaada mkubwa kwetu sisi Wizara katika kuboresha huduma za afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maoni makubwa ambayo yametolewa na Kamati, suala la kwanza ni kwamba tuhakikishe tunaongeza watumishi katika sekta zote mbili; Sekta ya Afya na Sekta ya Maendeleo ya Jamii. Ni kweli tunakubaliana na maoni na ushauri wa Kamati, lakini niseme kwa nini tunao upungufu mkubwa wa Watumishi wa Afya? Ni kwa sababu ya uwekezaji mkubwa ambao tumeufanya wa ujenzi wa Vituo vya Afya, ujenzi wa Hospitali za Wilaya, ujenzi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa sita pamoja na Hospitali Maalum. Kwa hiyo, kadri tunavyopanua miundombinu ya kutoa huduma za afya ndivyo mahitaji ya rasilimali watu yanavyohitajika.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme, Wizara yangu pamoja na ya kaka yangu Mheshimiwa Kapt. Mstaafu George Mkuchika, tumekaa tukabainisha mahitaji halisi ya ongezeko la Watumishi wa Afya, tumeandaa mpango wa miaka mitano na tunajua ni kiasi gani tunahitaji ili tuweze sasa kuhakikisha vituo vyetu vyote vya kutoa huduma za afya vinakuwa na watumishi wa kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumejipanga, ikifika mwaka 2022 tupunguze uhaba wa Watumishi wa Afya kutoka asilimia 52 iliyopo hadi asilimia 30. Nami naamini hili jambo linawezekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile umetoka ushauri wa Waheshimiwa Wabunge kwamba tutumie watumishi wa kujitolea (volunteers); tumeanza katika Hospitali zetu za Rufaa za Mikoa tumeanza katika Hospitali zetu za Kitaifa. Nikitoa mfano, hospitali ya Dodoma, kila mwezi inatumia shilingi milioni 35 kwa ajili ya watumishi wanaojitolea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, changamoto ipo katika Vituo vya Afya na Zahanati, kwa sababu wao hawana makusanyo ya kutosha. Hawa watu watajitolea, wanahitaji posho ya kujikimu, wanahitaji usafiri. Hawawezi wakajitolea watoto wetu bila kuwapa motisha (incentive) ili waweze kutoa huduma za afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwathibitishie Kamati na Waheshimiwa Wabunge, kadri tutakavyopata Watumishi wa Afya, tutaweka kipaumbele kwenye huduma za afya ya msingi, kwenye Zahanati, kwenye Vituo vya Afya na Hospitali za Wilaya. Amesema vizuri kaka yangu Mheshimiwa Ndassa (Senator), kadri tutakavyoboresha huku chini, ndivyo tutakapopunguza mzigo katika Hospitali za Rufaa za Mikoa na Hospitali za Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ni la ugharamiaji wa huduma za afya (health care financing) na hili limegawanyika katika maeneo makubwa mawili. Kamati inatushauri tuongeze bajeti ya fedha za afya.
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, tuseme, suala la afya ni kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli. Serikali ya Awamu ya Tano inajali na kuthamini afya za Watanzania. Kwa sababu ya msingi bila wananchi kuwa na afya bora, hatutaweza kufikia Tanzania ya viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hata ukiangalia, nadhani kuna sintofahamu; tutofautishe bajeti ya Wizara ya Afya na Bajeti ya Sekta ya Afya. Bajeti ya Sekta ya Afya inapitia pia Ofisi ya Rais, TAMISEMI, inapitia katika vyombo vyetu vya ulinzi na usalama ambapo kuna Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali ambao ni Watanzania hawa hawa wanapata pia huduma za afya. Kutokana na jambo hili, Serikali ya Awamu ya Tano tukiiangalia, tumeongeza bajeti ya Sekta ya Afya kutoka shilingi trilioni 1.2 mwaka 2013/2014 hadi shilingi trilioni 1.8 mwaka 2019/2020. Sisemi kwamba fedha hizi zinatosha, lakini unaiona dhamira yetu ya dhati ya kutaka kuboresha huduma za afya. Matokeo chanya yameanza kuonekana, hatujisifii tu kwamba tumejenga majengo nilikuwa Kome kwa rafiki yangu Mheshimiwa Tizeba, mama mjamzito sasa hivi anajifungulia Kome bila ya kuvuka kivuko kwenda Sengerema kujifungua, rafiki yangu Mheshimiwa Allan Kiula Mkalama kituo cha afya mama mjamzito anapata huduma za uzazi za dharura pale pale, kwetu sisi Awamu ya tano haya ni mafanikio makubwa sana ya kuokoa maisha ya mama mjamzito lakini ya kuokoa maisha ya watoto wa changa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge wa Kinondoni Mtulia amesema miaka minne iliyopita tulikuwa tunapeleka wagonjwa zaidi ya 600 kwa mwaka nje ya nchi, kwetu sisi siyo suala la kupunguza gharama sasa hivi tumetoka 600 mpaka 53 maana yake nini? Wananchi wengi zaidi wanapata huduma za upasuaji wa moyo ndani ya nchi, ukipeleka India utapeleka 600 ukifanya ndani ya nchi unafanya zaidi ya watu 3,000; kwa hiyo siyo suala la gharama lakini ni suala la kuhakikisha hata Mtanzania masikini anapata huduma bora za matibabu ya kibingwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwenye hili niahidi kwamba Serikali itaendelea kuongeza bajeti ya sekta ya afya kadri uchumi wetu utakavyoruhusu kwa sababu tunavyo vipaumbele vingi, tunavipaumbele vya maji, tunavipaumbele vya umeme, vya kilimo, lakini tutajitahidi kuongeza kuongeza bajeti kadri hali ya kiuchumi itakavyo ruhusu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la ugharamiaji wa huduma za afya, liko suala la wananchi kumudu gharama namshukuru sana Mheshimiwa Mwenyekiti Peter Serukamba na kamati yake kwa mara ya kwanza wameona mzigo mkubwa ya misamaha ambayo hospitali zetu zinabeba. Kwa hiyo tunavyokaa tukalaumu huduma mbaya na sisi ndiyo maana Wizarani tumesema tuje sasa na takwimu, misamaha kwa kila hospitali ni shilingi ngapi? Na hii ndiyo inajibu hoja mwananchi maskini sera inataka mwananchi kuchangia huduma za afya isipokuwa makundi matatu, lakini kama mtu hana uwezo tumeweka utaratibu wa kuchangia na ndiyo maana nikisoma haraka haraka, Kagera katika kipindi cha mwaka jana wametoa misamaha ya shilingi milioni 170, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa misamaha shilingi milioni 391, Mtwara Ligula misamaha shilingi 67 na Mbeya shilingi milioni 88.
Mheshimiwa Spika, nimesema Dodoma na Kamati imesema kwa hiyo ili suala la msamaha sisi ni jukumu letu kila Mtanzania apate huduma bila ya kikwazo cha fedha, lakini tumeangalia muarobaini wa kwenda nalo mbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwelekeo kama ilivyoshauri Kamati ni kuhakikisha tunakuja na bima ya afya kwa kila mtu ili aweze kupata huduma, siyo kwamba tumekaidi ushauri wa Kamati na Bunge, bado tupo katika taratibu na majadiliano ndani ya Serikali lazima tufanye-actuarial study (tathimini ya uhakika) kama kila mwananchi awe na bima je wachangie shilingi ngapi, wapate huduma katika hospitali za binafsi na hospitali za umma. Kwa hiyo siyo jambo la hararaka tumeelekezwa ebu tufanye tathmini ya kina tusije tukaanzisha bima kesho baada ya wiki mbili wananchi wanakosa huduma kwa sababu mfuko umefilisika.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ni suala la maendeleo ya jamii, tumepokea ushauri wa Kamati kuhusu kuboresha mitaala/kufanya review ya mitaala ya vyuo vyetu vya maendeleo ya jamii kwamba imepitwa na wakati tunalipokea na tutalifanyia kazi.
Lakini labda ;ingine la kusema amelisema vizuri Mheshimiwa Deo Ngalawa, Mheshimiwa Mbunge the way forward tusiwe pia ni taifa la kulilia tiba tiba, tiba sisi kama Wizara tumeona ipo haya sasa Serikali, jamii na wadau tukawekeza kwenye huduma za kinga, watu wanaumwa kwa sababu hawana vyoo, watu wanaumwa kwa sababu hawazingatii lishe bora, watu wanaumwa kwa sababu hawafanyi mazoezi, hawazingatii ulaji wa vyakula unaofaa wanavuta sigara, wanakunywa pombe kupita kiasi. Kwa hiyo,ili kupunguza mzigo wa fedha wa gharama za kutoa huduma za afya lazima wote kwa pamoja twende katika huduma za kinga badala tu ya kuwekeza katika huduma za kinga.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ni suala la Kamati ya UKIMWI ya Mheshimiwa Mukasa na mimi nimpongeze kwa kweli amekuwa ni msukumo mkubwa sana kwetu sisi Serikali kuhakikisha tunachukua hatua za kuhakikisha tunatokomeza virusi vya UKIMWI na UKIMWI ifikapo mwaka wa 2030 na inawezekana. Kwa hiyo, 90 ya kwanza...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kw amuda wa Mzungumzaji)
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA , WAZEE NA WATOTO: Ya pili au ya kwanza?
NAIBI SPIKA: Ni ya pili Mheshimiwa, lakini malizia dakika moja.
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Kwa hiyo, kwenye 90 ya kwanza nataka tu clarify sasa hivi asilimia 77 ya Watanzania wanoishi na virus vya UKIMWI tayari wanafahamu kwamba wanayo maambukizi ya UKIMWI na sasa hivi asilimia 98 ya wanaoishi na virusi vya UKIMWI tumewaingiza katika utaratibu wa dawa na asilimia 88 virusi
tayari vimefubazwa. Kwa hiyo, tunaenda vizuri Waheshimiwa Wabunge sina shaka kwamba tutafika lengo la kutokomeza UKIMWI Tanzania ikifika mwaka 2030 sambamba na kutokomeza kifua kikuu.
Mheshimia Naibu Spika, baada ya kusema hayo nawapongeza Kamati na ninaunga mkono hoja na Wizara tutatelekeza maoni na ushauri wa Kamati pamoja na wajumbe ahsante sana. (Makofi)