Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji Hadhi Sehemu ya eneo la Pori la Akiba la Selous kuwa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere

Hon. Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji Hadhi Sehemu ya eneo la Pori la Akiba la Selous kuwa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kwanza nianze kusema kwamba naunga mkono hoja na niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote ambao wametoa maoni na ushauri kwa hoja ya Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Spika, kama alivyosema Mheshimiwa Waziri kwenye wasilisho lake mapori yetu yote Hifadhi za Taifa na Mapori ya Akiba kinachotofautiana ni matumizi ya maeneo lakini yote yanasimamiwa na yanalindwa na yana ulinzi wa kutosha. Tunapopandisha hadhi pori la akiba la Selous na kuliita Nyerere National Park kinachobadilika pale ni matumizi tu ya eneo hilo, kwamba sasa tunakwenda kufanya zaidi utalii wa picha badala ya utalii wa awali ambao ulikuwa unaruhusu utalii wa picha na uwindaji, lakini matumizi mengine yote na namna ambavyo yanasimamiwa na ulinzi yanafanana. Kwa hiyo, niwatoe wasiwasi kabisa Waheshimiwa Wabunge ambao wameonesha kana kwamba kubadilika kwa hadhi sasa Wizara iende kuanza upya kufikiri namna ya kuhifadhi eneo hilo lakini na kuondoa wafugaji katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, wafugaji wote ambao tumewaona kwenye maeneo ya hifadhi na mapori ya akiba ni wavamizi na wamekuwa katika maeneo hayo kinyume cha sheria, kwa hiyo wawe ndani ya National Park au wawe ndani ya Game Reserve hawa wako kinyume cha sheria na wanashughulikiwa na sheria ile ya Uhifadhi ambao hawatakiwi kuwa katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, nijibu tu maeneo mawili matatu ambayo Waheshimiwa Wabunge wamesema na Kamati, moja ni la kushirikisha wadau, wadau wameshirikishwa na mchakato huu tangu Mheshimiwa Rais alipotoa maelekezo pale wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa bwawa la umeme wadau mbalimbali wameshirikishwa wakiwemo hao wenye mahoteli lakini pia wakiwemo wadau wanaofanya biashara za utalii na wananchi wa Mikoa ya jirani ya maeneo hayo. Kwa hiyo niwatoe wasiwasi kwamba suala hili halijakimbizwa kwa haraka, hakuna mdau ambaye hakusikilizwa.

Mheshimiwa Spika, katika wadau wakubwa ambao walikuwa katika maeneo yale, hasa ambao wanaathirika na ujenzi wa bwawa, Wizara kupitia Serikali wapo ambao wameguswa na wamepata fidia na wamepewa maeneo mengine ya kwenda kuwekeza.

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ambalo limeonekana lina shida kidogo ni kwamba eneo la hifadhi hii ni kubwa sana na kwa sababu hiyo yako maeneo ambayo hayatatumika kwa leo kwa faida, ni kweli kilometa za mraba elfu 30 ni nyingi na huwezi kuziendeleza na kuzitumia kwa mara moja. Kama mnavyofahamu tumekuwa na traditional product mbili sana Tanzania ni mbili tu ya kwanza ni Safari ambayo ni ya kupiga picha, na nyingine ni ya kupanda Mlima Kilimanjaro sasa maeneo haya ambayo yalikuwa yanatumika zaidi kwa uwindaji ni maeneo ambayo terrain yake hairuhusu utalii wa picha na wakati mwingine utalii wa safari tuliouzoea, lakini huu ni muda muafaka wa ku-develop aina nyingine ya product kwenye maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, labda tu nitoe mfano, ukienda leo Serengeti utakutana na balloons nyingi zipo mle ndani ambapo wawekezaji kadhaa wameingiza balloons ambazo zinaweza kutoa watu sehemu moja kwenda sehemu nyingine lakini pia tunafikiria hii milima mingi iliyomo katika pori la akiba la Selous tunaweza ku-introduce cable cars pamoja na maboti yanayopita kwenye maeneo ambayo sisi tunaona kwamba hayapitiki lakini kuna hiking na michezo mingi ambayo inatumika kwenye maeneo ambayo hayatumiki kwa utalii wa picha. Kwa hiyo, niwatoe wasiwasi kabisa Waheshimiwa Wabunge kwamba eneo hili tutakapolichukua litabaki bila matumizi.

Mheshimiwa Spika, la mwisho, imezungumzwa hapa kuhusu vivutio vingi vya utalii vilivyopo mikoa ya kusini. Ni kweli kwamba mchakato huu unakwenda kufungua Mikoa ya Lindi na Mtwara na tunakwenda kufungua ukanda wote wa mashariki (ukanda wa bahari) na kwa sasa hivi baada ya mchakato huu kukamilika, kwanza nilitaka nitoe taarifa kwamba maeneo yale ya Mikindani na Kilwa yote haya mwanzo yalikuwa hayajiendeshi vizuri kwenye shughuli za utalii lakini Wizara ilikaa na kufikiri na kuona kwamba ili yaweze kuwa sehemu ya package ya watalii wanaotembelea maeneo haya na kwa juhudi za sasa za kupandisha hadhi eneo hili kuwa hifadhi ya Taifa ambazo zitaongeza miundombinu na kufungua maeneo haya yote, tuliyaunganisha pamoja na taasisi zetu zote kama TAWA.

Mheshimiwa Spika, na juzi nilikwenda Mafia nimekuta TAWA wapo pale wanaimarisha miundombinu lakini Mikindani pale wapo na hata maeneo yote ambayo ameyasema Mheshimiwa Hawa Ghasia ni maeneo ambayo tayari tumeyaweka kwenye mpango kazi wa kuyafungua.

Mheshimiwa Spika, nimtoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge kwamba hata huu mradi wa REGROW ambao sasa ulikuwa sehemu ya juu ya Selous, awamu hii ya kwanza ya mradi huu wakati inaendelea kutekelezwa, Wizara imo katika mchakato kabambe wa Awamu ya II ya REGROW ambao sasa utaenda kuunganisha mikoa hii miwili ya huku chini na kuifungua kabisa na kuifanya iwe ni mikoa muhimu kwa ajili ya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwaondoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge kwamba tunatambua vivutio vingi vipo maeneo hayo, tunaamini kwamba tutakapoimarisha miundombinu na utangazaji wa maeneo hayo na tutakapokamilisha sasa uwekezaji, tutahamasisha biashara ya utalii ambayo imekuwa ni kivutio na chanzo kikubwa cha mapato kwa mikoa ya kaskazini.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)