Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Mbozi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami naomba kuchangia na nitajikita zaidi kwenye hii Itifaki ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za SADC kuhusu Kulinda Hakimiliki za Wagunduzi wa aina mpya za Mbegu za Mimea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ni kuhusu asilimia moja ya pato ghafi la Taifa kutopelekwa kwenye utafiti. Ni kwa muda mrefu sana Serikali yetu haipeleki asilimia moja ya pato ghafi la Taifa kwenye mambo ya utafiti na leo tunaenda kuridhia Itifaki hii, kama fedha hazitapelekwa tafsiri yake ni kwamba tunaenda kuwanufaisha wale ambao watakuwa tayari kupeleka fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba nchi kama Afrika Kusini imeendelea sana na iko serious sana kwenye mambo ya utafiti, leo tunaenda kushindana nao hao kwenye suala hili lakini kwa sababu wao wako serious na sisi hatujawahi kupelekea fedha huko, Serikali ituambie baada ya kupitisha Itifaki hii watakuwa tayari sasa kuanza kupeleka fedha za utafiti ili tutakachopitisha leo hapa au tutaporidhia Itifaki hii isije mwisho wa siku tukashindwa kuwasaidia watafiti wetu. Kwa hiyo, nadhani hili ni jambo muhimu sana isije kuwa tunasindika wenzetu ambao tuko nao lakini wao wamejiandaa kuliko sisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kuhusu fedha za maendeleo ambazo mara nyingi hapa Bungeni tumekuwa tukizipitisha au kuidhinisha lakini fedha hizi hazitolewi. Kwa mfano, leo tunapozungumzia suala hili la Hakimiliki za Wagunduzi wa aina mpya za mbegu maana yake hizi ni fedha za maendeleo na tunajua kwenye fedha za maendeleo Serikali hii ya Awamu ya Tano naona haijajipanga kabisa kwa sababu mara nyingi sana imekuwa ikisuasua kupeleka fedha kama Bunge linavyoidhinisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mwaka 2016/ 2017, zile fedha za maendeleo zilizokuwa zimeidhinishwa na Bunge hili shilingi bilioni 100.527 zilipelekwa shilingi bilioni 2.2. Sasa kama zilipelekwa fedha hizo na hapa tunapitisha Itifaki hii, je, utekelezaji wa haya mambo inakuwaje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2017/2018 tulipeleka asilimia 11 tu ya fedha za maendeleo ambazo ziliidhinishwa na Bunge hili. Sasa leo tunapitisha Itifaki hii na kwenye Itifaki hapa tunaambiwa bajeti lazima itatumika, sasa inakuwaje kama hatutatenga fedha za maendeleo kwa ajili ya kwenda kutekeleza mambo haya ambayo tunaenda kuyapanga leo? Kwa hiyo, niseme tu kwamba kama Serikali haijajipanga kwenye mambo kama haya ni bora tukawa na subira ili mwisho wa siku tujipange vizuri na baadaye tuangalie namna ya kuweza kufanya lakini kama watatuhakikishia na Mheshimiwa Waziri yuko hapa kwamba fedha za maendeleo zitatolewa vizuri basi hii Itifaki itatekelezwa lakini kama hazitatolewa kama ambavyo miaka ya nyuma zimekuwa hazitolewi, nadhani tutaenda kugonga mwamba na hatutafanikiwa kwenye suala hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni suala la mbegu za asili. Serikali ituambie wamepanga utaratibu gani kuweza kulinda mbegu za asili. Nafahamu kwamba nchi yetu tumekuwa na mbegu za asili nyingi sana na nyingine zimeanza kupotea polepole. Tulikuwa na mchele mzuri kule Kyela na zamani mnakumbuka ulikuwa unanukia, ule wa Kamsamba leo Serikali imejipangaje kutunza mbegu hizi maana zinaingia mbegu hizo mpya na za kwetu za asili zinapotea.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.