Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

Hon. Rehema Juma Migilla

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ulyankulu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi nami nichangie kidogo kwenye hii Wizara. Awali ya yote napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu wataala, kwani bila yeye sisi hatuwezi.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda naomba moja kwa moja nijikite kwenye mada. Ni ukweli uliowazi kwamba sekta ya kilimo inachangia kwa asilimia kubwa sana katika kutoa ajira kwa watu wenye elimu na hata wasiokuwa na elimu. Hata hivyo, sekta hii imekumbwa na changamoto kubwa sana hususan kwenye changamoto ya masoko especially mazao ya biashara.

Mheshimiwa Spika, nitajikita zaidi kwenye zao la tumbaku. Mkoa wa Tabora kama ilivyo mikoa mingine inayolima tumbaku umekumbwa na tatizo kubwa kabisa la zao la tumbaku kuwa linadorora siku baada ya siku. Yote hii inasababishwa na kauli mbalimbali kwamba zao hili linasababisha kansa na kauli nyingine mbalimbali ambazo hazina tija kwa mkulima. Mimi naona tatizo kubwa sio hizi kauli, tatizo kubwa lipo kwenye Serikali na nini kinasababisha, kinachosababisha mpaka hili zao kuzorota ni kupotea kwa hawa wanunuzi wa zao la tumbaku baada ya kuwa kuna milolongo mingi ya kodi na tozo zisizokuwa na faida kwa hawa wanunuzi.

Mheshimiwa Spika, mfano, ni hii export levy; sasa hivi export levy imepanda kutoka 0.25% mpaka 1% kwenye export value sasa kama hii tozo inapanda kwa kiasi hicho inamkandamiza sana na kumuumiza huyu mnunuzi hali inayopelekea mpaka aamue asinunue mazao yetu. Hii impact yake ni nini? Tumeona kuna kampuni moja ya kununua tumbaku sasa hivi imefunga oparesheni kutokana na kwamba imeshindwa ku-afford hizi gharama.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni Serikali kushindwa kurudisha hii VAT returns, suala la VAT returns ni suala ambalo lipo kisheria na kikatiba na inapaswa kila mwaka lirejeshwe kwenye haya makampuni ya net exporters, lakini sasa hivi kwa miaka kama mitatu mfululizo huko nyuma hii VAT returns hairudishwi. Sasa tunajiuliza kama huko nyuma VAT returns ilikuwa inarudishwa nini kimesababisha mpaka dakika hii VAT returns ambayo ndiyo ilikuwa inawa-bust hawa wanunuzi waweze kununua tumbaku kwa wingi zaidi.

Mheshimiwa Spika, sasa tunaomba Wizara ituambie je, hii export levy ambayo imepanda kwa kiasi hicho itairudisha lini lakini vile vile hii export value na yenyewe itarudishwa lini na VAT kwa sababu tunaona wakulima wetu hawajui hatima yao ni nini, leo makampuni ambayo yanafunga operesheni zao tunaona kuna redundancy kubwa ya wafanyakazi, lakini tunaona pia halmashauri nyingi mfano Tabora Mjini, Urambo wapi zinakosa cess, lakini pia wakulima sasa hivi mpaka wanapewa limitation, badala ya kulima kama walivyokuwa wanalima zamani sasa hivi anaambiwa lima tani kadhaa au kilo kadhaa kitu ambacho kinaikosesha hata Serikali yetu mapato ya forex.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni kwenye korosho; korosho ndiyo limekuwa zao mbadala kwa Mkoa wa Tabora baada ya kuonekana zao la tumbaku linasuasua kwa kiasi kikubwa sana. Hata hivyo, zao hili linapelekwa kisiasa siasa zaidi hali ambayo inawakatisha tamaa wakulima kuingia kwenye hicho kilimo cha korosho. Naomba sasa hii Wizara ili zao hili liweze kulimwa na wengi na liwe lenye tija basi kwanza tunaomba elimu itolewe juu ya zao la korosho. Pia suala lingine hii miche kule kwetu inauzwa sasa kama inauzwa watu wanashindwa kununua badala ya kupewa bure, leo wanauziwa mche mmoja ni shilingi 1,000. Kwa hiyo tunaomba hii kama inawezekana wapewe bure ili waweze kupata moral.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni vitambulisho vya wakulima na hii bima ya wakulima. Hili suala ni zuri sana kwani litawawezesha wakulima wetu kuwa na wenyewe wanatambulika juu ya kilimo chao, lakini tunaona tu kuna story story tu kwenye hiki kitabu cha Waziri kwamba mpaka dakika hii hakuna kanzidata inayoonesha ni wakulima wangapi wa tumbaku ambao wamesajiliwa kwenye hiyo kanzidata yake.

Mheshimiwa Spika, pia suala lingine ni kwenye hii bima ya wakulima. Tunaelewa kabisa kwamba sasa hivi kuna mabadiliko makubwa sana ya hali ya hewa, mafuriko yamekuwa ni mengi, ukame umekuwa wa kutosha, sasa hivi wakulima wetu wanalima kilimo cha mashaka mashaka sana. Kama kweli hii bima itatolewa kwa hawa watu wetu basi nina uhakika kabisa hili suala ni zuri na namwomba Waziri waliendeleze ili wakulima wetu sasa pindi wanapolima wawe wana uhakika kwamba hata ikitokea janga Fulani, basi wawe na uwezo wa kufidiwa.

Mheshimiwa Spika, lakini suala lingine ni kwenye suala la pembejeo...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)