Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ESTHER M. MMASI: Mheshimiwa Spika, kwa heshima na unyenyekevu mkubwa napenda kutoa pongezi zangu kwa Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Hasunga pamoja na Manaibu wake kwa wote wawili Mheshimiwa Bashungwa pamoja na Mheshimiwa Omary Mgumba kwa juhudi zao katika kuinua wakulima wa Taifa hili.
Mheshimiwa Spika, nitapenda kujielekeza mchango wangu juu ya ushiriki wa vijana kwenye kilimo cha biashara kama ajira mbadala na hatima ya ustawi wa kipato cha mtu mmoja mmoja.
Mheshimiwa Spika, Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007 sambamba na rasimu ya mwaka 2017 ya Sera ya Taifa ya Ajira ikisomwa pamoja na mkakati wa Kitaifa wa kuwezesha vijana kwenye sekta ya kilimo (2016 – 2021) instruments zote hizi zimetia mkazo wa kutosha juu ya umuhimu wa kuwezesha vijana kujihusisha na shughuli za kiuchumi ikiwemo shughuli za kilimo cha kisasa.
Mheshimiwa Spika, sambamba na miongozo tajwa ya kisera na kisheria ikumbukwe kuwa kwa sasa nchi yetu ya Tanzania inazalisha graduates zaidi ya 700,000 kwa mwaka na kwa bahati mbaya graduates si zaidi ya 40,000 sawa na asilimia (6 – 10) ndio wanaoingia kwenye soko la ajira rasmi, lakini haitoshi Serikali imekuwa iki-spend takribani shilingi bilioni 427 kugharamia elimu ya vijana vyuo na vyuo vikuu kupitia HESLB.
Sambamba na hili pia, Serikali imekuwa iki-spend takribani kati ya Shilingi bilioni 20 mpaka 23 kwa mwezi kwenye utekelezaji wa sera ya elimu bure. Nguvu zote hizi ni vyema zikaakisiwa kwenye ukuaji wa uchumi hasa tunapoangalia ushiriki wa vijana katika muktadha mzima wa ajira kwani kwa kufanya hivi ndivyo tunavyoweza kushabihisha uwekezaji mkubwa wa Serikali kwenye elimu na ujuzi wa vijana wetu na uchumi endelevu wa nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyokwishaandika hapo juu, juu ya sera ya mikakati ya kushirikisha vijana kwenye sekta ya kilimo ni dhahiri kwamba, bado tuna changamoto kubwa sana katika kutengeneza ajira za kilimo cha biashara kwa kundi kubwa la vijana. Changamoto tulizonazo kwa mantiki hii ni pamoja na yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza, kukosekana kwa mitaala ya somo la kilimo kwenye elimu ya awali, sekondari na hata kwenye baadhi ya vyuo vikuu visivyokuwa na mchepuo wa kilimo.
Mheshimiwa Spika, pili, kukosekana kwa usimamizi mzuri juu ya Mfuko wa Maendeleo ya Vijana chini ya Halmashauri zetu. Fedha zinazotoka (41%) kwa baadhi ya Halmashauri zetu zimekuwa zikitoka kama sehemu ya utamaduni na hakuna mechanism nzuri ya kuona fedha hizi zinakwenda kwenye kusudio la kuondosha tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana wetu. Mafungu haya yangeelekezwa kwenye kilimo cha biashara na hata usimamizi ukawekwa vizuri, naamini vijana wengi wangeondokana na adha ya ukosekanaji wa mitaji na hata wangeweza kushiriki kwenye shughuli za kilimo cha biashara.
Mheshimiwa Spika, tatu, kwenye Bajeti ya Wizara ya Ardhi ya 2016/207 Wizara ya Ardhi chini ya Mheshimiwa Waziri Lukuvi alielekeza Wakurugenzi wote wa Mipango Miji kutenga maeneo maalum na mahususi kwa ajili ya vijana wetu ili waweze kushiriki kwenye kilimo. Pamoja na maelekezo na mikakati ya Wizara ya Ardhi katika kuona vijana wanapata maeneo ya kilimo, lakini bado hakuna kilichotekelezeka mpaka sasa. Vijana wamekosa hatima ya ajira zisizo rasmi pamoja na maneno mazuri ya baadhi ya waajiri.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2018/2019, Wizara ya Viwanda na Biashara ilitenga fedha kupitia Mfuko wa NEDF kiasi cha shilingi bilioni 17, ili kusaidia wajasiriamali wadogowadogo kama startup capital, lakini hakuna kilichotoka hata tunapokwenda mwisho wa mwaka wa fedha 2018/2019. Vijana wamekosa fedha za kushiriki kwenye sekta ya kilimo cha biashara kupitia Mfuko huu. Hata hivyo, vijana wamekosa kutumia fursa mbalimbali za kilimo biashara, mfano mwaka 2016/2017, Wizara ya Viwanda na Biashara ilitangaza kufungwa dirisha maalum kwa kundi la akinamama na vijana kushiriki kwenye zabuni za Serikali.
Mheshimiwa Spika, zipo taasisi mbalimbali za Serikali zinazonunua biashara za mazao mfano FNRA na hata Taasisi za Ulinzi na Usalama, Jeshi na Magereza ambazo zimekuwa zikitangaza tenda mbalimbali kwa kuwa vijana wetu hawajaandaliwa inakuwa ni vigumu vijana wetu kuweza kutumia fursa mbalimbali. Fursa za AGOA pia bado hazijatumiwa kutokana na kukosekana na mipango madhubuti ya Wizara ya Kilimo katika kushirikisha vijana kwenye masuala ya kilimo cha biashara.
Mheshimiwa Spika, ifuatayo ni sehemu ya ushauri wangu kwa Serikali:-
Mheshimiwa Spika, kwanza, mradi wa kuwainua vijana kupitia mradi wa kilimo cha vizimba (greenhouse) chini ya Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ipitiwe upya na badala yake mradi huu ulenge zaidi katika kilimo shirikishi cha biashara. Pia mradi utoe dira na mwelekeo sahihi juu ya masoko ya bidhaa inayolengwa kufundishwa kupitia mradi huu.
Mheshimiwa Spika, mradi ulenge kutoa elimu ya mnyororo wa thamani ya mazao ya kilimo biashara, mradi ulenge kutoa ajira za kudumu kwa kuelekeza vyanzo vya fedha ambazo ni tengeo la vijana kwenye Wizara mbalimbali, mfano, Mfuko wa Vijana wa Taifa, fedha za vijana kupitia halmashauri zetu (4%). Serikali kupitia halmashauri zetu ielekeze kila halmashauri itoe sheria ndogo itakayotaka halmashauri zetu kutenga sehemu maalum ya ardhi ili vijana wapate mahali pa kuendesha shughuli za kilimo.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Elimu iandae mtaala maalum wa kilimo na vijana wetu wafundishwe nadharia ya kilimo cha biashara kutokea ngazi ya chini ya elimu.
Mheshimiwa Spika, pia Wizara iharakishe katika kutoa mkakati wa kitaifa wa kuhusisha vijana kwenye Sekta ya Kilimo. Mkakati huu bado unasomeka kama rasimu na siyo mkakati rasmi wa kitaifa.
Mheshimiwa Spika, kwa haya machache naomba kuunga mkono hoja ya bajeti Wizara ya Kilimo. Ahsante.