Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa ulinzi wake kwetu sote. Ninaomba sasa na mimi nitoe mawazo yangu katika Wizara hii mumhimu ambayo ndio uti wa mgongo wa taifa. Pamoja na umuhimu mkubwa uliopo ndani ya Wizara hii iliyobeba asilimia zaidi ya 65 ya wananchi wa Tanzania. Bila Wizara hii uhai wetu unakuwa mashakani kwani hii ndiyo Wizara ya chakula. Hivi karibuni imethibitika kuwa hata mazao tuliyokuwa tunayatambua huko nyuma kama mazao ya chakula kama maharage, mahindi na mpunga sasa yamekuwa sehemu ya mazao ya biashara. Kama ndivyo basi naomba nishauri Wizara yafuatayo;
Mheshimiwa Spika, kuongeza idadi ya Maafisa Ugani ili waweze kuwasaidia wananchi kulima mazao haya muhimu kwa tija. Kutoa elimu juu ya kilimo cha kisasa ya mazao haya muhimu. Kujenga maghala ya kutosha ya kuhifadhia mazao haya. Njia pekee ya kujihakikishia usalama wa chakula nchini ni kufanya kilimo cha umwagiliaji. Hata hivyo, kwa bahati mbaya sana huko ndiko ambako Serikali haipeleki fedha za kutosha ambazo zingeweza kutekeleza azma hiyo. Kama hili halitoshi wakulima wamekuwa wakicheleweshewa pembejeo, jambo linalowasababishia hasara kubwa wakulima wetu.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa sisi wote tunahubiri suala la Serikali ya Viwanda. Zaidi ya asilimia 60 ya malighafi ya viwanda hivi tunategemea kutoka mashambani. Ni vyema sasa tuone umuhimu wa kuanzisha vituo vya ushauri na kuondoa changamoto zote zinazowakwaza wakulima wetu ili tuweze kufanikiwa kama taifa kufikia uchumi wa viwanda ifikapo 2025. Kwa kuwa Wizara hii ndiyo Wizara pekee ya kututoa mahali tulipo ili kufikia malengo ya Serikali ya Viwanda tuliyojiwekea ni dhahiri kuwa bajeti ambayo imekuwa ikitengwa imekuwa ndogo sana kiasi cha kutotosheleza mahitaji makubwa yaliyopo.
Mheshimiwa Spika, Wizara hii pia ina changamoto kubwa ya upungufu wa watumishi, jambo ambalo limekuwa kikwazo katika utekelezaji wa kazi nyingi katika Wizara hii. Ni rai yangu sasa Serikali ione ni kwa njia gani tunawekeza katika Wizara hii ya Kilimo ili kuweza kufikia malengo tuliyojiwekea ya kuondokana na uhaba wa chakula pamoja na kupata malighafi toshelevu kwa ajili ya viwanda vyetu.
Mheshimiwa Spika, nipende kuishauri Serikali yangu kuwekeza katika kilimo cha mazao mkakati kama kahawa, Pareto, tumbaku na kadhalika ili tuendelee kujenga uchumi wetu lakini pia kujipatia fedha za kigeni.