Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Saada Salum Mkuya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Welezo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. SAADA MKUYA SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu. Kwanza naunga mkono hoja, lakini nachukua fursa hii kumpongeza kwa dhati kabisa Rais a Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuhakikisha kuweka mikakati madhubuti kwa ajili ya kuendeleza sekta ambazo ziko katika Wizara hii. Nampongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri pamoja na viongozi wote katika Wizara hii kwa kufanya kazi zao kwa weledi na ufanisi mkubwa, hongera sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda mimi nitajikita katika eneo moja tu, nalo ni uvuvi wa bahari kuu. Specifically nitajikita katika kuboresha mazingira ya utendaji kazi wa Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu (Deep Sea Fishing Authority).

Mheshimiwa Mwenyekiti, taasisi hii ni taasisi ambayo kwa kweli ikiweza kufanya kazi vizuri inaweza ikachangia kwa kiasi kikubwa mapato ambayo Serikali zote mbili zinapata. Vilevile mazingira mazuri yatasababisha wavuvi, wananchi ambao wanajishughulisha na shughuli za uvuvi katika bahari kuu nao kuweza kufanya kazi zao kwa ufanisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa wengi walizungumza kuhusiana na suala la some percentage ya hao wanaojishughulisha na uvuvi, lakini ukiangalia Zanzibar, kwa maana ya Unguja na Pemba asilimia 100 kwa sababu ni visiwa ambavyo, kama definition ya visiwa, vimezungukwa na bahari, sasa uone kwamba, taasisi hii kwa kiasi gani ni muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini taasisi hii imekuwa ikikusanya mapato kutoka katika vyanzo mbalimbali zikiwemo leseni na mambo mengine; lakini katika mwaka 2017 hii royalty au mrabaha wa senti 40 za dola zimesababisha kwa kiasi kikubwa taasisi hii kupungua kwa mapato yake ya kujiendesha kama mamlaka, lakini hata mchango wao kwenda katika Serikali Kuu umetoweka, hususan kwa mwaka 2019 hakuna leseni ambayo imekatwa kutokana na tozo hii. Na cha ajabu, maana si kama tumeweka tozo hii kwamba ndiyo tunaimarisha mapato ya ndani, mapato yameondoka na hawa wawekezaji katika sekta hii wanakwenda nchi nyingine ambazo hazina tozo hii. Kwa maana hiyo mapato ambayo sisi tulikuwa tunatarajia kuyapata tunayapeleka katika nchi nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nadhani umepata concern za Wabunge lakini vilevile na za wadau mbalimbali kuhusiana na tozo hii. Hii tozo si kwamba uifute moja kwa moja lakini unaweza ukatoa space ili tuweze kufanya review kuona kwamba je, tunaweza tukaangalia maeneo mengine tupate mapato?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kwa kinachoonekana sasahivi inaonekana ni kwamba labda utendaji mzuri wa Wizara yetu hii ni kutokana na mapato, lakini utendaji mzuri, yaani mafanikio ya Wizara yetu ni kuona productivity katika maeneo mbalimbali imeimarika na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa kwenye Pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Deep Sea Fishing Authority mapato yake kwanza inatakiwa asilimia 50 ijiendeshe yenyewe, kama tunavyojua ni mamlaka, lakini asilimia 30 inaingia katika Mfuko wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na asilimia 20 inaingia katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anafahamu, asilimia 20 kwa namna yoyote, kwa mapato ya aina yoyote ni significant contribution kwa ajili ya Bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Ikiwa Mheshimiwa Waziri bado una-resist ku-review hii kanuni, maana siyo sharia, ni kanuni, kwa ajili ya kuondoa tozo hii maana yake unaumiza Serikali hizi. Unaumiza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, unaumiza na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Sisi Mheshimiwa Tizeba nakwambia Zanzibar tunalia, tunalia kwelikweli, tunalia kwelikweli na tumeshazungumza muda mrefu. Mheshimiwa Waziri hii tozo iondoshe kwa muda ili uwape nafasi mamlaka wafanye review waweze kuangalia maeneo mengine. Sisi tunakosa wenzetu wanapata, na si kwamba tunakosa kwa wananchi tu bali unakosesha mapato kwa Serikali zote mbili; Mheshimiwa Waziri liangalie hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri aje na majibu ambayo yataleta matumaini. Otherwise tutashika shilingi tuone kwamba kwa ujumla wetu sisi kama Wabunge tunalichangia hili maana yake pesa zinaondoka, mapato yanakosekana na hata hao wavuvi, wawekezaji ambao tunatarajia wawepo wanaondoka wanakwenda sehemu nyingine ambapo wenzetu hawana tozo ya aina hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, otherwise naunga mkono hoja na ninaomba sana Mheshimiwa Waziri utakapokuja utueleze kwa kina ni kwa sababu gani tozo hii inaendelea kuwepo na impact yake kuendelea kuwepo kwake. Ahsante. (Makofi)