Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Yussuf Salim Hussein

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Chambani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na mimi kwa kupata nafasi.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa masikitiko makubwa, na naomba katika hili utusaidie. Juzi nilimpa tatizo hili kabla ya kuwasilisha hotuba yao jana Mhehsimiwa Naibu Waziri kilio cha Wazanzibar kuhusiana na usafirishaji wa dagaa. Wazanzibar wanasafirisha dagaa kutoka Zanzibar kupeleka Congo, wana vibali vyote kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kusafirisha, lakini wanapofika ndani ya Tanganyika Tunduma wanakamatwa, wakishakamatwa dagaa wao wanazuiliwa wanalipishwa faini ya milioni mbili kila mtu mmoja na gari inapigwa faini ya milioni kumi; evidence zote hizo nimempa Mheshimiwa Naibu Waziri kabla ya kuwasilisha hotuba yao jana. Kama hilo halitoshi wanawekwa ndani wanapouliza kwa nini, sisi tuna vibali, hii ni transit tu tunapita kwa nini tunakamatwa? Wanawekwa ndani. Kuna msafirishaji anaitwa Ameir maarufu Mchezo amewekwa ndani kwa kuuliza swala hilo, kuna huyu agent wao pale Tunduma anaitwa Kibona amewekwa ndani kwa kuuliza swali kama hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaposema sisi Wazanzibar kuhusu masuala haya tunaambiwa tunasema maneno ya uchochezi. Mmetuzuilia sukari tusilete hapa tumenyamaza, mmetuzuilia maziwa yasiletwe hapa tunanyamaza, basi hata kupita? Kwa kweli hili linaumiza sana; na huu ni mwezi wa Ramadhan sitaki kusema sana lakini ni kitu kinachoumiza sana.

Mheshimiwa Spika, mimi nimwambie, na nilisema katika Bunge hili, kwamba Serikali ya Awamu ya Tano hii kuanzia Mheshimiwa Rais na Mawaziri hawa wanafanya kazi vizuri sana, wanakwenda mbio sana Mawaziri hawa kutatua changamoto hizi, lakini hapa katikati hapa ndipo penye matatizo, mpaangalie. Sasa hata magari yanakamatwa, kwa mfano kuna magari tisa yamekamatwa Mbeya yamepelekwa Tunduma; huko Tunduma kuna nini? Kwamba gari imekamatwa Mbeya, kama ni watu wa Fisheries wako pale, kama ni watu wa TRA wako pale lakini yapelekwe Tunduma, kuna nini huko?

Mheshimiwa Spika, sasa Wizara inajisifu imekusanya makusanyo mengi sana zaidi ya mpango wao kumbe ni dhuluma, maana hii mimi ninaiona kuwa ni dhuluma; Inauma, inauma, inauma kweli kweli. Tunaomba yale mambo wanayofanya hawa ndugu zangu hawa wa Kinyamwezi, yaani kila mnapotugusa sisi tunanyamaza, tunawaangalia tu; mnatugusa na hapa tunanyamaza tunawaangalia tu, tunataka ushahidi kamili.

Mheshimiwa Spika, naomba hili utusaidie; hawa ni watani wangu; we tulia wewe. Naomba niendelee. Naishauri Serikali katika suala la uvuvi wa bahari kuu. Kuna meli nyingi sana zinazokuja kuvua katika bahari yetu. Niko katika uwekezaji kandokando ya barabara Ukanda ule wa Kaskazini ya Pemba.

Mheshimiwa Spika, meli nyingi sana zinakuja zinafanya fishing, diving, na snorkeling lakini hakuna kazi yoyote, hakuna utaratibu wowote unaopatikana. Wakati huo huo Zanzibar inataka kusajili meli kwa ajili uvuvi kuna tatizo hili la kodi ambalo wamewekewa inakuwa ni tata.

Mheshimiwa Spika, tunaomba, kama sisi hatuwezi kulinda bahari yetu nani atatulindia? Na shida iliyopo hawa Askari wetu wa Marline Park, hawa wanaofanya, hawawezi kuzifikia, zile meli, zile meli ni kubwa vyombo walivyonavyo wao kuwafikia wale ni vyombo vidogo. Kwa mfano iko siku moja watu wa TRA, ZRB na KMKM walienda na fiber boat, kuna meli ilikuwa inavua karibu sana na Manta Resort zote wakaenda. Walipokaribia wale waliwaambia tu huko huko mliko ishieni huko, waliwatangazia kwa spika lao kubwa lile wakafanya ubishi wakaenda. Ile meli ilizungushwa tu wale karibu wazame, kwa sababu kile ni ki-fiber boat na lile ni wimbi la kuzungusha meli.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tuiombe Serikali katika suala hili lazima tujipange. Watu wanatoka huko, wanakuja Tanzania kwenye bahari yetu wanavua wanaondoka na samaki halafu samaki hao hao wanarudi tunakuja kuuziwa tena hapa hapa. Katika hili hatujajipanga; hii bahari ni rasilimali moja moja kubwa sana na ambayo inatuletea tija kubwa sana kama tutajipanga lakini bado hatujawekeza vya kutosha. Niiombe Serikali iwekeze vya kutosha katika eneo hili.

Mheshimiwa Spika, achana na hapo sasa, hiyo ni bahari kwa upande huu wa Magharibi, lakini sasa nenda upande wa Mashariki ya bahari yetu. Kule kwetu sisi kuna upande wa Mashariki wa vile Visiwa, sasa hapo ndipo utaona meli ambazo zinavua haswa. Hizo meli kubwa zinakuja, zinavua kwa mwezi mmoja kisha zinaondoka; hakuna kule kwa sababu hata hizo fiber bolt haziwezi kwenda.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Yussuf.

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.