Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Hamoud Abuu Jumaa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibaha Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. HAMOUD A. JUMAA: Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mungu kwa kuniwezesha kuwepo mahali hapa nami niweze kuchangia hotuba hii ya Bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya Mwaka 2019/2020. Halikadhalika nitumie nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri na watendaji wake wa Wizara kwa kuandaa hotuba nzuri. Hotuba hii inakwenda kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi kwa kuhakikisha sekta nzima ya mifugo na uvuvi inaendelea kuimarika kama ilivyoainishwa.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kuanza kwa kutoa pongezi kubwa kwa Serikali kwa kuendelea kuimarisha sekta ya mifugo na uvuvi kwa kushirikiana na sekta binafsi. Aidha, katika mwaka 2018/2019, Serikali imetuambia ilianzisha dawati la sekta binafsi kwa ajili ya kutatua changamoto zinazowakabili wawekezaji katika sekta za mifugo na uvuvi. Lengo la Serikali ni kuongeza uwekezaji wenye tija utakaowezesha wafugaji na wavuvi kuongeza kipato, kuzalisha malighafi za kutosha za viwanda na kuongeza mchango kwenye Pato la Taifa. Hatua hiyo ni muhimu sana kwa maendeleo chanya ya sekta hii.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo Serikali imeendelea kuhakikisha kwamba sekta ya mifugo na uvuvi inakua na mnyororo mpana wa ongezeko la thamani kwa kutoa kipaumbele katika ujenzi wa viwanda vya kusindika mazao ya mifugo na uvuvi, hatua ambayo inakwenda moja kwa moja kuazimia ile hoja ya kuwa na Tanzania ya Viwanda. Hadi sasa viwanda 99 vya kusindika mazao ya mifugo vimeanzishwa vikiwemo viwanda 17 vya nyama, 76 vya maziwa na sita vya ngozi, hatua ambayo itawasaidia wafugaji na wavuvi hasa kupandisha thamani ya bidhaa zao. Vilevile katika mwaka 2019/2020 Serikali imeendelea kuweka msisitizo katika kuwezesha sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika uwekezaji kwenye viwanda, kuimarisha usimamizi wa rasilimali katika ukanda wa uchumi wa bahari na bahari kuu; na kuimarisha miundombinu na kukuza biashara ya mazao ya uvuvi. Aidha naishauri Serikali kutoa elimu kwa wavuvi wetu hasa katika Nyanja ya uvuaji wa Bahari Kuu ili sasa na wao waweze kushiriki kwa namna moja katika kukuza uchumi wa taifa letu.

Mheshimiwa Spika, Sasa Naomba Nizungumzie Changamoto Zinazotukabili Kibaha Vijijini. Katika Jimbo letu tumeendelea kuwa na migogoro ya wafugaji na wakulima, migogoro hiyo inasababisha kuzorotesha hali ya kiuzalishaji wa kiuchumi kwani muda mwingi wananchi wamekuwa katika migogoro hiyo. Ninaishauri Serikali kuchukua hatua kadhaa zitakazowezesha kupunguza migogoro hiyo, hasa kwa kufanya upimaji wa maeneo yote ya ufugaji wa Kibaha Vijijini ili yajulikane kwa kuweka alama maalum ili kuepusha mwingiliano kati ya wafugaji na wakulima. Aidha Kata ya Kwala kujengwe Ranchi ya kufugia ili wafugaji wakafugie mifugo yao huko. Kufanya hivyo kutapunguza migogoro iliyopo kati ya wafugaji na wakulima ambayo imeendelea kudumu kwa muda mrefu bila kupatiwa ufumbuzi.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.