Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafinga Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Niseme wazi na pengine naweza nisieleweke lakini ndiyo ukweli; kama kuna Wizara zilikuwa pasua kichwa, basi Maliasili na Utalii, Nishati na Madini siku za nyuma, lakini mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni; toka Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla ameingia hapo kwa kweli, tuwe wakweli wa nafsi za ukweli; Wizara imetulia, Wizara imekuwa ina mwelekeo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla ana timu nzuri. Nikiona Katibu Mkuu Profesa, Naibu Katibu Mkuu Dokta, TFS yuko Profesa, lakini pia hata Wenyeviti wake wa Bodi wengi ni Mabrigedia, ni Majenerali. Kwa hiyo bila shaka kazi hii, pamoja na msaidizi wake, Mheshimiwa Kanyasu, wataendelea kuifanya ili Watanzania waweze kupata neema na pato linalotokana na utalii liweze kuongezeka. Napongeza hili kwa dhati ya moyo wangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizi, nipende kupongeza pia uongozi wa TFS, lakini pia na uongozi wa Shamba la Sao Hill pale Mafinga na Wilaya ya Mufindi kwa jinsi ambavyo tunashirikiana. Zamani kulikuwa na shida sana ya mambo ya vibali, ujanja ujanja ulikuwa mwingi, lakini taratibu tumekuwa na vikao vya pamoja, tumekuwa na vikao vya wadau na mambo kiasi fulani yamekwenda katika mstari ambao unastahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, katika Sekta ya Misitu na mimi niseme mambo makubwa mawili; kwanza, sisi tunaotoka ambako misitu inatuongozea maisha kwa asilimia siyo chini ya 50 mpaka 70, tulikuwa tumependekeza na kuishauri Serikali iweze kuondoa lile zuio la kusafirisha mazao ya misitu saa 24. Nilitarajia Mheshimiwa Waziri kwa jinsi ambavyo namwamini, toka tukiwa DARUSO, mimi niko Mlimani yeye yuko Muhimbili, tukiendesha gurudumu la kuhakikisha kwamba mambo ya cost sharing yanakaa vizuri, namwamini katika hili na naamini atalitekeleza na wananchi wa Mafinga na maeneo mengine watalisikia katika hotuba yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu gani? Nime-peruse kitabu hiki kutoka ukurasa wa kwanza mpaka ukurasa wa 97, nilitarajia nitaikuta kauli inayohusiana na jambo la kuruhusu mazao ya misitu kusafiri saa 24, kwa hiyo natarajia Mheshimiwa Waziri atakapokuja katika kujumuisha atatueleza lolote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kama nilivyosema, sisi wananchi wa Mufindi, Mafinga, Iringa, Njombe na Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini tunaendesha maisha yetu kwa kutegemea mazao ya misitu. Sasa kuna watu ambao wanavuna katika Msitu wa Sao Hill. Nimwomba Mheshimiwa Waziri, wakati umefika sasa, kama ambavyo walifanya katika Sekta ya Madini ambapo kuna mikopo kwa wale wachimbaji wadogowadogo, hebu sasa tuwe na utaratibu wa kuwapa mikataba hata ya miaka mitatu mitatu wavunaji wetu ili waweze kukopesheka katika mabenki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ya kutoa kibali ni utaratibu mzuri, lakini tunawomba Mheshimiwa Waziri tunakoelekea sasa watu hawa wapate mikataba ili kwa mikataba ile kwanza, watakuwa na uhakika wa kuajiri watu, lakini pia watakuwa na uhakika wa kupata mikopo na mwisho watakuwa na uhakika wa kuchangia Pato la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende pia kusema katika suala zima la Chuo cha Misitu Olmotonyi; Mheshimiwa Waziri, tumekuwa tukiomba na hiki ni kilio chetu watu wa Mafinga na maeneo yale, kwamba walau tungekuwa hata na campus kwa ajili ya chuo cha misitu katika Nyanda za Juu Kusini na bahati nzuri pale Sao hill majengo yapo. Jambo hili ni mwaka wa tatu sasa nalisema. Nimwombe Mheshimiwa Waziri, kwa jinsi ambavyo anajituma katika kufanya kazi na wasaidizi wake; hebu waone kwamba sasa ni wakati wa Chuo cha Misitu kuwepo Nyanda za Juu Kusini na pale Mafinga, Sao Hill, tayari majengo yapo. Hii yote itakuja kuleta tija katika uvunaji wa misitu, lakini katika kuchakata mazao yanayotokana na misitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie utalii; sisi hapa Tanzania tunasema ni wa pili baada ya Brazil, hii hapa tunaita ni comparative advantage, lakini Mheshimiwa Waziri ili tunufaike na utalii lazima tufanye kitu kinaitwa competitive advantage. Kwa sababu kama ni wa pili tayari ni wa pili, sasa kuwa kwetu wa pili tunanufaika vipi? Kweli nimeona hapa katika takwimu za Mheshimiwa Waziri ameonesha ambavyo ongezeko la watalii kwa mwaka huu tunapoelekea ni watalii milioni 1.5. Kwa ongezeko hili tumepata fedha za kigeni dola bilioni 2.5 mwaka 2017 na sasa imeongezeka mpaka Dola za Kimarekani bilioni 2.4. Sasa tukisema dola pengine mwingine haelewi, hizi fedha kwa Kitanzania ni zaidi ya trilioni 5.2.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukipunguza vikwazo katika Sekta ya Utalii tunaweza sisi tukahakikisha ndani ya miaka michache tuna watalii wasiopungua milioni tano. Tukipata watalii milioni tano maana yake ni nini; ikiwa sasa kwa watalii milioni moja na laki tano tunapata walau trilioni 5.2 kwa mwaka, maana yake ni kwamba tutakuwa tunakadiria kupata mapato yasiyopungua trilioni 15, hiyo ni nusu ya bajeti yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tufike huko tusibaki tu kusema kwamba sisi ni wa pili, sasa sisi kuwa kwetu wa pili tufanye nini? Tumeona kuna vikwazo mbalimbali katika kuhakikisha kwamba biashara ya utalii inakua. Nimwombe Mheshimiwa Waziri, kama walivyofanya wenzetu wa madini, aitishe kongamano, nampongeza, alipoingia tu katika Wizara hii aliita mkutano wa wadau, lakini ulikuwa ni wa wadau wa Sekta nzima ya Maliasili na Utalii, namwomba waitishe mkutano maalum tu kwa ajili ya mambo ya utalii. Ikiwa hii ni sekta inayotupa fedha za kigeni zaidi ya asilimia 20, kwa nini tusiilee ili tuweze kuongezea pesa za kigeni na hivyo kuendelea kujenga uchumi wetu imara? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende pia kuzungumza kuhusu maeneo mahususi, historical sites; Mheshimiwa Waziri amesema ambavyo wameongeza maeneo na mazao mapya ya utalii, lakini nitatoa tu mfano, pale Kilolo kwa kaka yangu, Mheshimiwa Mwamoto, kuna Gereza la Mgagao, gereza hili walikuwa wanakaa, Walter Sisulu amekaa pale, Mandela amekaa pale na watu wa South Africa wangependa kuja kutembelea pale kama sehemu ya makumbusho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Balozi alipofika pale na kukuta tumefanya gereza akasikitika kwamba ninyi mnatukumbusha enzi za apartheid. Namwomba Mheshimiwa Waziri akae katika Serikali waangalie mambo ya historical sites, kule Iringa kuna maeneo ya Isimila, kule Kalenga kuna kaburi la Bismarck; haya yote kwa pamoja yanaweza kutuongezea sisi kuleta idadi kubwa ya watalii, lakini tukiendana pia na kuondoa vikwazo ambavyo kwa namna moja au nyingine vinarudisha sekta nyuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, wakati Simba inacheza, Klabu Bingwa Afrika, Haji Manara anasifika kwa kuhamasisha na watu kujaa Uwanja wa Taifa, zaidi ya 60,00; Taifa Stars ilipocheza na Uganda, zaidi ya watu 60,000 wameingia pale Uwanja wa Taifa. Mheshimiwa Waziri, aje na mkakati wa kuhakikisha tunahamasisha pia utalii wa ndani… (Makofi)
MWENYEKITI: Hebu rudia tena, klabu gani hiyo?
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la michezo, kuna msemaji anaitwa Haji Manara wa Simba Sports Club…
MBUNGE FULANI: Bodaboda!
MHE. COSATO D. CHUMI: …kuna msemaji anaitwa Thobias Kifaru, kuna msemaji anaitwa Masau Bwire; hawa watu wanaleta hamasa watu wanaenda viwanjani. Je, sisi kama Taifa kwa nini tusihamasishe watu wetu waweze kwenda kwenye mbuga ili tuwe na…
MBUNGE FULANI: Bodaboda!
MHE. COSATO D. CHUMI: ...tupate fedha za kigeni. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, Mheshimiwa Rais juzi amesema Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakurugenzi, wawe na laini za TTCL. Nami nitoe wito; familia zetu sisi viongozi ziwe za kwanza kwenda kufanya utalii wa ndani ili kuhamasisha na hivyo kujipatia fedha kwa sababu utalii wa ndani unaingiza fedha, mama anauza bagia, mama anauza sambusa, fedha inakwenda moja kwa moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno haya, naunga mkono hoja na Mungu atubariki sote. (Makofi)