Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nsimbo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa hii nafasi na nashukuru Mungu ametuwezesha tuko salama mpaka muda huu. Kwanza nianze kupongeza watendaji ndani ya hii Wizara wakiongozwa na Mheshimiwa Dkt. Hamisi Kigwangwala, pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Constantine Kanyasu; na nipongeze watendaji wote na taasisi zilizoko chini ya Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni leo tu Mkurugenzi wa TFS ametatua kero ambayo iko kwenye Jimbo langu naomba nimpongeze sana Professor Dos Santos Silayo kwa kuitikia kilio hicho kwa haraka, na kazi ambazo unazifanya ndani ya ndani ya muda huu uko kwenye hii taasisi unaleta mambo mazuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuchangia kuhusiana na Hifadhi ya msitu wa Msaginia wenye ramani JB 215 ulotokana na GN 447 ya tarehe 24 Disemba, 1954, maana yake ni kabla ya Uhuru wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna changamoto katika msitu huu kama ifuatavyo;
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza katika mawasilisho ambayo tumewasilisha kwenye ile kamati ambayo iliundwa na Mheshimiwa Rais; na nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kusikiliza kilio cha sisi Wabunge na wananchi kuhusiana na maeneo haya na kuunda kamati hii ambayo inamshauri namna ya utatuzi; kuna vijiji ambavyo vilipimwa ndani ya msitu huu, kijiji cha Igongwe na Matandarani, na ramani namba 48870 ilitoka. Vilevile katika ramani hii ya msitu wa Msaginia kuna vijiji ambavyo kwenye ramani vimekatwa lakini GN hii 447 bado haijabadilishwa, na vijiji hivi kisheria bado vinasoma viko ndani ya hifadhi. Vijiji hivyo ni Msaginya, Mwenge, Songambele, Mtakuja, Kapalala, Magamba, Makongoro, Isanjandugu pamoja na kijiji cha Namba moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika Msitu huu wa Msaginia nikienda sambamba na Hifadhi ya Wanyama ya Katavi, chini ya hifadhi hiyo, inapakana na Kijiji cha Stalike; sasa kuna eneo la Kitongoji cha Stubwike ambapo kuna sehemu Serikali iliwatoa wananchi kwasababu mbalimbali tu za kiusalama dhidi ya wanyama wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Maombi Yangu. niombe sasa Serikali tuone namna ya kubadilishana sehemu ya kitongoji cha Stubwike na hifadhi ya msitu ambao uko chini ya TFS. Yaani Stubwike tuwamegee Katavi National Park, lakini kwa ukubwa huo hata mkitoa na bonus mmege sehemu ya msitu wa TFS ili sasa mwingiliano kati ya wananchi na Katavi National Park tuupunguze, na mpaka itakuwa ni barabara ambayo inayoelekea Mpimbwe kwenye Jimbo la Kavuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwenye Msitu wa North East Mpanda. Msitu wa North East Mpanda tulivyokaribisha wakimbizi kutoka nchi ya Burundi mwaka 1972, tuliweka makazi pale ya wakimbizi, ambayo ni ya Katumba. Niiombe Serikali iendelee kushughulikia eneo hili kwasababu ni ndani ya hifadhi ya msitu uolimegwa. Wananchi wanaishi mule kwa miaka hii mingi zaidi ya miaka 40, na shughuli na ujenzi na sasa TAMISEMI imeingia, tunaboresha miundombinu tunapeleka umeme na tunapeleka maji. Niiombe Serikali, muone namna bora ya kutatua jambo hili kwa haraka. Kama tuwe na mpango wa matumizi bora ya ardhi na kupima mipango mji basi lifanyike kwa haraka ili tuondoe hali ya sintofahamu kwasababu wananchi hawa wamekuwa sasa hawawezi kufanya maendeleo kwasababu bado mamlaka ziko zinasimamia maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo ndani ya makazi hayo hayo kwa ufadhili ya UNHCR ilijengwa shule ya msingi ambapo ina vyumba vya madarasa sita nzuri kabisa matundu ya vyoo na nyumba za walimu ziko mbili. Thamani yake ni si chini ya milioni 150. Sasa niombe Wizara tumesha iachia ile shule baada ya kufanyika ile eviction; lakini hebu tuombe muichukue ndiyo iwe moja ya makambi ya mafunzo ya vijana wenu, kwa aidha mtupe fedha au mtujengee shule kama hiyo hiyo katika maeneo ambayo tunauhitaji wa vyumba vya madarasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika msitu huo wa North East Mpanda tunaomba Serikali tunaomba Serikali ingalie namna gani huenda kwenye msitu North East Mpanda au Msitu wa Msaginia kuna maeneo ambayo yamekuwa na uvamizi wa miaka mingi. Wananchi wanalima pembezoni mwa Msitu huu wa Msaginia na eviction zilifanyika na niseme kwa bahati mbaya ilitokea tarehe 24 Disemba, mwaka jana kuna wananchi watano walijeruhiwa baada ya kuonesha kuwa walitaka kupambana na askari wa Usu na wakafyatua risasi ziliwajeruhi watu watano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ili kuondoa adha hii ya wananchi wetu kuumizwa kutokana na uvamizi hebu tuombe sehemu ya Msitu wa Msaginia kwa kipande cha kutoka Sitalike mpaka unakuja Maili Kumi watumegee maeneo ambayo tayari sasa hivi yanalimwa zaidi ya miaka 20, katika mpango huu ambao Rais anauruhusu ili wananchi hawa wapate maeneo ya kulima. Maana kwa upande mwingine kwa mfano Kijiji cha Mtisi katika Kata ya Sitalike ni shughuli za madini ambazo maeneo yale huweze kufanya shughuli za kilimo kutokana na ardhi ilivyo. Kwa hiyo tuombe sana Serikali tuondoe mgogoro huo wa wananchi basi kwa kumega hiyo sehemu wapate sehemu za kulima, itatusaidia sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo katika mpaka wa Kijiji cha Sitalike na hifadhi ya Katavi National Park kuna Mto wa Katuma. Sasa niombe serikali hebu tumege sehemu ya mto hata kama kilometa moja tuwape wananchi kwa ajili ya uvuvi wa samaki aina ya kambare. Hii itakuwa ni moja ya ujirani mwema ambayo inawasaidia sana wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie juu ya suala utalii, tumeona Serikali inafanya juhudi kubwa sana, watalii wanatoka 1.3 milioni mpaka 1.5. Sasa tuiamshe mbuga yetu ya Katavi tuna uwanja mzuri wa ndege wanaleta watalii kutoka nchi mbalimbali basi wapate wadau wa kuboresha, kujenga hoteli na mbuga yetu ni nzuri wanyama very natural na tembo wakubwa katika nchi hii wanatoka Katavi na kuna yule twiga chotara ambaye tupo kwenye Mbunga ya Katavi. Hebu tuletewe watalii ili tukuze uchumi na vijana wetu wapate ajira za kubeba na kuongoza watalii katika Mkoa wetu wa Katavi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho lakini si dogo, niombe sasa kwa Wizara hii pia halmashauri zetu zinahitaji kuongeza mapato ya ndani basi tuone kwa Sheria ya Misitu ya mwaka 2002, watumegee sehemu kwa ajili ya kuweka malisho na tuweke block za malisho sehemu ya msitu kwa ajili ya halmashauri yetu kuongeza mapato ya ndani kwa kuweza kuweka wafugaji na kuweka sehemu za malisho. Kwa hiyo, wakitumegea na sheria inaruhusu, tuombe Waziri awasilishe kwa mujibu wa Sheria ya Misitu, 2002, Na.14, halmashauri yenyewe ipate sehemu ya msitu, hii ikiwa ni sehemu ya kuongeza mapato ya ndani tukizingatia kwamba vyanzo vingi sasa hivi vimeshuka vya kimapato kwenye halmashuri zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, niseme tu napongeza Serikali, nampongeza Rais wetu kwa kusikiliza kilio na kuunda ile Kamati, nampongeza Mheshimiwa Dkt. Kigwangala, alifika Stubuiko yote, Makutanio alitembelea na pia Mheshimiwa Kanyasu ameenda amefunga mafunzo, ameona jinsi gani Katavi ilivyo, sasa waende wakainyanyue na iweze kunyanyua mkoa wetu kiiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)