Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Marwa Ryoba Chacha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Serengeti

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana. Naomba nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri anayofanya katika Wizara hii. Anafanya kazi kubwa sana Mungu ambariki sana. Niseme Mheshimiwa Waziri kuna jambo atakumbukwa sana ni jambo la ujenzi wa barabara ya kuanzia lango la Loduare kule Ngorongoro mpaka pale Golini Serengeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii barabara ya Ngorongoro ni barabara ambayo Waziri anafahamu udongo wake ni volcanic, katika matengenezo ya kawaida ilikuwa imeshindikana. Kwa hiyo niseme, Mungu ambariki sijui nimpe nini? Wamefanya kitu kikubwa ambacho watakumbukwa milele na milele, kujenga barabara ya lami katika eneo hili na tena kizuri zaidi wameruhusiwa na UNESCO. Niseme Mheshimiwa Waziri Mungu ambariki yeye pamoja na Ndugu Kijazi. Maana ilikuwa sio kazi rahisi kuruhusiwa na UNESCO kujenga barabara hii, lakini niseme Mungu ambariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kidogo, kwenye eneo hili la barabara kilomita 88, ni bora waka-extend ikafika Ikoma gate kwenye ile gate la Serengeti ili ikae vizuri. Hata hapa niseme wamefanya jambo kubwa na Mungu awabariki sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni mapendekezo nimesoma kwenye kitabu cha Waziri ukurasa wa 33, ile namba 75 kuhusu masharti ya wajumbe wanaounda WMA, nimeisoma vizuri kwamba kwenye kanuni ambazo zilikuwa zimetengenezwa, kwamba wale wajumbe ambao ni darasa la saba walikuwa hawaruhusiwi kugombea na kwenye maelezo ya kitabu cha Waziri amesema imeleta mgongano, sintofahamu kidogo na nimeona Wizara wapo tayari kufanya marekebisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri alisimamie, wafanye marekebisho kwa sababu kanuni hii kimsingi inapingana na katiba ya nchi. Katiba ya nchi inasema mtu ajue kusoma na kuandika ndio achaguliwe sasa tukiweka kwa wale Wenyeviti wa WMA, bahati nzuri tuna kina Musukuma hapa ni Mbunge, lakini si darasa la saba? Kwa hiyo, nadhani ni vizuri kanuni ile irekebishwe ili darasa la saba na wao wapate fursa ya kugombea kuwa Wajumbe wa WMA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni mgogoro wa mipaka kati ya vijiji ambavyo vipo Serengeti na Serengeti National Park, tunafahamu, tumeongea mara nyingi mimi na yeye na ameonesha positive response na aliahidi kwamba tutaenda na yeye Serengeti. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, nimwombe sana rafiki yangu akipata nafasi hebu twende kwenye Vijiji vya Merenga, Machochwe, Mbalibali, Tamkeri, Bisarara, Bonchugu angalau aone uhalisi wa kile kinachozungumzwa, kwa sababu kuna maeneo vigingi vimewekwa kwenye maeneo ya vijiji kabisa katikati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kibaya zaidi kuna siku moja nimekwenda kwa Mheshimiwa Waziri, akikamatwa na ng’ombe kwenye maeneo hayo anafilisiwa ng’ombe na anafungwa. Kwa mfano kuna mama mmoja alikamatwa ni mjamzito, ngo’mbe walitaifishwa wameunzwa wote, amefungwa, amepigwa faini na sasa hivi amejifungulia yupo magereza. Nimwombe Mheshimiwa Waziri yeye anatokea maeneo ya wafugaji na bahati nzuri mwenyewe ni mfugaji anafahamu ninachokiongea, sio vyema kuwafanya watu wetu kuwa maskini, ni vema tuwasaidie watu wetu kujali Hifadhi ya Serengeti, kwa sababu kama una jirani ni lazima uishi naye vizuri, sio kwa kugombana. Kwa hiyo nimwombe twende Serengeti akaone.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambao nataka niongee ni jambo la utafiti umefanyika, inaonekana kama Serengeti hoteli kama zinakuwa nyingi vile. Huku nje hakuna hoteli, nimwombe pamoja na tatizo la single entry, ni bora tusaidie watu wajenge hoteli nyingi nje ya hifadhi, kukiwa na utitiri wa hoteli ndani ya hifadhi kutakwamisha migration ya wanyama kwenda kule Masai Mara. Kwa sababu kutakuwa na utitiri wa hoteli, tuweke nje hoteli zitasaidia wananchi wanaozunguka hayo maeneo kukua kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa najaribu kuangalia kwenye kitabu cha hotuba ya Kambi la Upinzani, ukurasa wa tano ile namba 13; wanasema Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kufuta agizo lake la kuzuia biashara ya viumbe hai nje ya nchi na iwalipe fidia wafanyabiasha kwa hasara na usumbufu waliowasababishia wafanyabiashara hao. Maana yake kambi ya Upinzani inasema Serikali iruhusu wanyama wauzwe nje ya nchi. Sasa nakumbuka mwaka fulani tukiwa nje ya Bunge waliokuwa wanapiga kelele wanyama kuuzwa nje ya nchi walikuwa ni Kambi ya Upinzani au nasema uongo jamani?

WABUNGE FULANI: Kweli.

MHE. MARWA R. CHACHA: Walikuwa wanapiga kelele twiga amepandishwa kwenye ndege, walikuwa ni akina nani, si ni akina Msigwa hawa?

WABUNGE FULANI: Kweli.

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Mheshimiwa Msigwa anakuja na maoni hapa kwamba wanyama wauzwe, maana yake leo Upinzani wangepewa nchi hii wangeuza wanyama wote wakaisha. Mheshimiwa Waziri asiingie kwenye huo mkenge, akatae hiyo biashara, azuie wanyama wasiuzwe, kwa ajili ya manufaa ya vizazi…

T A A R I F A

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Marwa.

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikia mchangiaji nilikuwa nadhani angechukua muda kidogo kujielimisha. Wanyama tunaozungumza warudishwa hawa wananchi wanaouza ni tofauti kabisa na hao wanyama anaosema twiga, tembo. Wanaozungumziwa ni mijusi, konono, vipepeo ambavyo havihusiani kabisa na wanyama anaosema.

MWENYEKITI: Ahsante. Taarifa hiyo Mheshimiwa Ryoba.

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa huyu Mchungaji nini asichoelewa, wewe si unasoma maandiko unalewa vizuri. Mmesema inataka kufuta agizo lake kuzuia biashara ya viumbe hai, viumbe hai ni wapi? Sasa ungekuwa unamaanisha konono, ungekuwa unamaanisha mijusi ungetaja lakini hujataja. Kwa hiyo hapo usijifiche hapa, nilikuwa najaribu kushangaa nimwombe Mheshimiwa Waziri, wasamehe maana hawajui walitendalo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni jambo la KfW, Mheshimiwa Waziri na hususan Mheshimiwa wa Fedha naomba anisikilize, tumepata msaada kutoka Ujerumani, kwa ajili ya kusaidia Ngorongoro na Serengeti kwenye barabara kwenye afya na maji. Leo kuondoa exemption miradi hii ifanyike imekuwa ngumu, mpaka leo tunaongelea mwaka wa tano miradi haijafanyika. Nimwombe Mheshimiwa Waziri bado asichoke, nimwombe Waziri wa Fedha jamani wakae waangalie hili jambo, hivi mtu anakuletea msaada wewe unaukata eti alipe kodi, hiyo ya wapi jamani, hiyo haiwezekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo sikuwa na mambo mengi. Ahsanteni sana. (Makofi)