Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Niende moja kwa moja kwenye hoja zangu za msingi. Hoja ya kwanza inahusu suala la utalii. Nichukue nafasi hii kuipongeza sana Wizara kwa kazi nzuri ya ubunifu ambayo inaifanya; mpaka sasa tunaona kwamba watalii wamekuwa wakija kwa wingi kutoka nchi mbalimbali; Israel, Malaysia, China na maeneo mengine, hongera sana kwa vijana ambao wanafanya kazi katika Wizara hii na siku moja Mheshimiwa Dkt. Kigwangwala alisimama hapa akasema yeye si wa mchezo mchezo; hii imejidhihirisha wazi katika utekelezaji majukumu yao ambayo wanayafanya pamoja na Naibu wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujua kwamba huu Mradi wa Utalii katika Mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma ni lini utapelekwa na unapita kwenye maeneo gani? Nataka kusema kwamba kule tuna Selous Game Reserve, tuna Liparamba, tuna Makumbusho ya Majimaji, lakini tuna zoo moja ya Ruhira pale ni zuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile pale Njombe tuna nyumbanitu, nyumbanitu ni maeneo ambayo yana vitu vya ajabu ajabu sana. Kuna kuku wapo mle wanaishi kwenye ule msitu hajulikana nani amewafuga na wapo humu wakiwa na rangi nyeusi. Pia wapo ng’ombe wanazunguka kwenye hilo eneo, hajulikani nani amewaweka, kwa hiyo ni nzuri sana watalii wakienda kwenye maeneo haya yakiwemo pamoja na maeneo hayo ya Mkoa wetu wa Ruvuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie Mto Ruvuma; mto huu umekuwa na mamba wengi sana ambao wamekuwa wakileta athari kubwa sana kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma. Niwaombe Wizara ije iwavune hawa mamba, lakini pia siku moja nilimsikia Mheshimiwa Mulugo alizungumza hapa kuhusu Ziwa Rukwa napo kumekuwa na mamba wengi sana. Wizara ifanye juhudi za makusudi kuwavuna hawa mamba ili wasiendelee kuleta athari.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika ukurasa wa tatu kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake, aya ya tatu lakini pale imeandikwa namba tisa, naomba niseme suala ambalo kimsingi linatia huzuni, lakini pia tumekuwa tukiwazungumzia sana ndugu zetu ambao wamekuwa wakiathirika na masuala hasa yanayozunguka kwenye maeneo ya wanyamapori. Tumekuwa tukisahau kuwazungumzia askari wetu ambao ndio wanasimamia na kulinda rasilimali hii ya Tanzania. Askari hawa wamekuwa wakijeruhiwa, wangine wamekuwa wakichomwa na mishale ya sumu, wengine wamekuwa wakujeruhiwa na hawa majangili, wamepoteza maisha, nimeona kwenye hii aya wapo zaidi ya 11.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana, hawa vijana wamejitoa wengine wanaumwa na nyoka, wanalala huko porini tuwatie moyo. Niombe sana Wizara hii, kwanza niwape pole kwa kupoteza hao vijana, lakini pia niombe stahili zao wanazostahili wapewe. Ikiwezekana waongezewe hata kiwango cha mshahara ili waweze kufanya kazi vizuri zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye suala ambalo Mheshimiwa Waziri amesema kwamba anatupa offer. Mheshimiwa Waziri tunakushuru sana kwa hii offer ya futari. Hata hivyo, niombe amekuwa akitupa futari kila wakati tunamshuru sana, lakini safari hii afanye kitu kingine mbadala, atualike Bunge zima kwenda kufanya utalii katika Mbuga ya Ngorongoro, Serengeti, Saadani na maeneo mengine, futari tumekula sana baba.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nichukue nafasi hii kuwapongeza sana Mawaziri wanafanya kazi nzuri sana, waendelee kuchapa kazi. Matarajio ya Mheshimiwa Dkt. John Joseph Magufuli anayoyatarajia kufikia mwaka 2020/2025 ni makubwa na wao ndio vijana amewaweka na amewaamini, waendelee kuchapa kazi. Kazi zao ni nzuri, wanasikiliza watu vizuri, wanatoa maelekezo vizuri, tunawashukuru hawajidai wala nini. Pia Makatibu Wakuu, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu wapo vizuri, nimekwenda ofisini kwa Katibu Mkuu amenisikiliza vizuri na tatizo langu likatatuliwa kwa haraka, nashukuru sana.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.